Ngúgí Wa Thiong’o
1.
Nyoyo zimetuatua,habari za kifo chako
Ni zaidi ya tanzia,lakithiri sikitiko
Mengi umetuachia,nguli ulokwenda zako
Pumzika kwa amani,fundi Ngúgí wa Thiong’o
2.
Mbinu ya kalamu yako,ilitikisa miamba
Hukutoa neno lako,ovyo likenda kuyumba
Yasikitisha mauko,hapa mbolezi twaimba
Pumzika kwa amani, fundi Ngúgí wa Thiong’o
3.

Ujombani Mlimani,uliko usuli wako
Mila zetu na imani,pamoya nayo miiko
Uliweka vitabuni,tena bila babaiko
Pumzika kwa amani, fundi Ngúgí wa Thiong’o
4.
Wastahiki maziko,ya hadhi iso mfano
Mzee wetu uliko,Mola kakupe usono
Latukaba hangaiko,waandishi tu hapano
Pumzika kwa amani, fundi Ngúgí wa Thiong’o
5.
Maudhui ainati,ya vya taifa vituko
Yote uliweka kati,ukamwa wapenda choko
Kwenye zako harakati,hukutishwa na viboko
Pumzika kwa amani, fundi Ngúgí wa Thiong’o
6.
Ulitaka badiliko,katika siasa zetu
Ulipinga machafuko,ya kuvunja utu wetu
Wengi twapiga vidoko,twakupeza kito chetu
Pumzika kwa amani, fundi Ngúgí wa Thiong’o
Mtunzi: Paul Ndetei
Lakabu: Mshairi Msi Shari
Nairobi
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Diaspora Times Global Oct 17 – Oct 23, 2026
- Is social media a blessing or a curse for university students?
- Light at last: How electricity is reshaping Nandi and Uasin Gishu
- The triple squeeze: how EPRA’s fuel price hike is reshaping the survival equation for the common mwananchi
- Zelenskyy accuses Trump of rewarding Putin as Pope pleads for peace from a hospital bed