Huku ndiko nyumbani,
Safari yetu inakoanzia,
Ndiko tunakokutamani,
Kila tunapopawazia,
Mandhari ya vijijini,
Aghalabu hutuongoa,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
1.
Huku ndiko tumekulia,
Tangu hizo enzi za jadi,
Hatuna pa kukimbilia,
Ila papa kwenye chudi,
Inatupasa kufurahia,
Kupapenda yetu jadi,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
2.
Huku ndiko tulikosomea,
Hasa kuanzia chekechea,
Ndiko sisi tulikobobea,
Shuleni kuraukia,
Miguu kavu kujiendea,
Na baridi nyingi kutuingia,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
3.
Huku ndiko tulikolelewa,
Malezi ya kisawasawa,
Mawaidha tukapewa,
Tuwe waja maridhawa,
Wenye bidii na vipawa,
Na mienendo ya kisawa,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
4.
Huku ndiko tunakojivunia,
Kwa usuli wenye utajiri,
Utajiri wa kupapambania,
Kwa kujituma bila kiburi,
Ndiposa leo ninakiri,
Na ukweli kuwaambia,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
5.
Huku ndiko tunakopatambua,
Makao yetu kindakindaki,
Nje na ndani tunapajua,
Na pia kwa yake mikiki,
Huku kuna nyingi mvua,
Izalishayo mahindi na uki,
Kitale ndiko nyumbani, safari yetu ilikoanzia,
6.
MTUNZI: Momanyi Henry
LAKABU: Malenga Mtanashati
ENEO: Kesogon