Wanjohi. P. Mugambi
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni
Nairobi Kenya
Mwanangu nakujulisha, hili langu kulishika,
Mkembe sitokutisha, kwa nisemayo hakika,
Ni suluhu ya maisha, sikiza uje pevuka,
Leo ni leo.
Lile nalomaanisha, jana imeshapita,
Weye kuilazimisha, kurudi hutoipata,
Leo itanabahisha, bidii ukainata,
Leo ni leo.
Usije jihangaisha, kuihusu kesho yako,
Mwana fanya kwa bashasha, leo ijae msuko,
Uisuke ikiisha, kesho ijae chereko,
Leo ni leo.
Juzi ilishaisha, nayo jana ikazaa,
Jana ndiyo lipitisha, leo uione paa,
Na leo yadhibitisha, ya jana uliyotwaa,
Leo ni leo.
Kesho itadhihirisha, uyafanyayo waama,
Uzembe ukianzisha, kesho utalia hima,
Siwe kujidhalilisha, pweke uje kulalama,
Leo ni leo.
Ndio hali ya maisha, ikwamie leo mwana,
Nawe utaizalisha, kesho iwe ya maana,
Shida utaziyeyusha, ufurahie kwa sana
Leo ni leo.
Anza sasa kuegesha, mazuri na yalo mema,
Yaliyo mawi ondosha, bukrata na mapema,
Ili leo ikapisha, mambo yaliyo nudhuma,
Leo ni leo.
Mwana ninahitimisha, shika leo kweli leo,
Leo kaibadilisha, ikakupe mwelekeo
Ili na kesho maisha, yaje yakuvike cheo,
Leo ni leo.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER October 23, 2026
- Ruto’s parting COMESA call: Remove the barriers, honour the commitments
- Direct hospital access to KEMSA cuts drug delays, says PS
- Africa can’t wait: Continent seeks $1 trillion for climate adaptation
- Ruto passes the baton as Africa’s trade bloc faces a fragmenting world