Tanzania plane crash

Salamu ninazitoa, kwa ndugu watanzania,

Machungu twayapitia, kilio metufikia,

Ajali lotufikia, ni Bukoba-Tanzania,

Poleni watanzania, kwa hi’ ajali ya ndege.

 

Hatuwezi kutabiri, ajali kinga haina,

Kwa vyombo vya usafiri, inakuja kiaina,

Kwenye ndege hata feri, magari pia safina,

Sisi ndugu wasafiri, tuzidi kuombeana.

 

Twayathamini maisha, hilo hakika mwandani,

Tena pasipo kubisha, tuna kilio cha ndani,

Ajali ndugu yatisha, yatutoa duniani,

Tuwaombee wenzetu, wale walotangulia.

 

Tuwafariji wafiwa, wababa pia wamama,

Na watoto walofiwa, lazima kuwatazama,

Wazidi kunyunyuziwa, sizo mipaka neema,

Poleni sana wapendwa, tulie kwa tumaini.

 

Tumshukuru Rabuka, loruhusu yatokee,

Na walionusurika, nazo nguvu awatie,

Ili wapone hakika, waje wamshuhudie,

Ewe Mungu Maulana, zishushe zako baraka.

 

Ajali si masihara, ila mimi nafikiri,

Tuzidi kuwa imara, kuepuka yalojiri,

Yasitoke’ kila mara, kwa vyombo vya usafiri,

Kwani hii ni hasara, ajali zikikithiri.

 

Na wapendwa marubani, sisi tunawaamini,

Mliketi masomoni, kutuendesha angani,

Hii ajali kazini, s’sa mwongeze umakini,

Muwe na moyo mkuu, msije nyuma kurudi.

 

Chonde simameni wima, ombi langu mlishike,

Muutunze usalama, tusafiripo tufike,

Tushikamane daima, na elimu itumike,

Mengine tumwache Mungu, ayatenda kwa ziada.

 

Naomba niwaageni, chozi linanizidia,

Poleni sana poleni, wandugu watanzania,

Huu sasa mtihani, ila tuziweke nia,

Ni mimi Stani malenga, mtoto wa Usangira.

Stanislaus Stephan Usangira

+255714325876/+255694091955

stanislausstephan8@gmail.com

Tabora-Tanzania.

By The Mount Kenya Times

We are The Mount Kenya Times. For customer care, 📨 info@mountkenyatimes.co.ke or 📞 +254700161866 For feedback to editorial, 📨 news@mountkenyatimes.co.ke or 📞 +254705215262 or WhatsApp +254714090155

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *