Duncan Mulu
Binadamu tuna nguvu, nguvu zenye miujiza
Tunapafanya angavu, pale palipo na giza
Ni ajabu ilo kavu, yale tunayotimiza
Nikikaa nashangaa, Binadamu navyong’aa.
Taaluma zinavuma, Kazi bora zinafanya
Magonjwa yakituuma, Dakitari ayaponya
Kwenye wodi wajituma, ndwele zetu kuzionya
Nikikaa nashangaa, Binadamu navyong’aa.
Dani Mulu nashangaa, Hosipitalini wodi
Wagonjwa wagaagaa, Kifo kinabisha hodi
Dakitari awafaa, Uzima warudi bodi
Nikikaa nashangaa, Binadamu navyong’aa.
Ndege nazo zinapaa, rubani ni mwanadamu
Kwenye hewa wakikaa, safari kuipa zamu
Furaha inawajaa, wakishafika sehemu
Nikikaa nashangaa, Binadamu navyong’aa.
Walimu mainjinia, wa ujinga na akili
Shuleni wanapania, maarifa kunakili
Kazi wanajivunia, ujinga kuukabili
Nikikaa nashangaa, Binadamu navyong’aa.
Kutoka hajui kitu, kusoma na kuandika
Ni kama mnyama mwitu, hajui hata kushika
Mwalimu hufanya kitu, Ujuzi kuubandika
Nikikaa nashangaa, binadamu navyong’aa.
Kusoma aweze soma, kusema na kuandika
Kusikiza hadi ngoma, na maana kuiweka
Shahada na Dipuloma, kielimu kujengeka
Nikikaa nashangaa, binadamu navyong’aa.
Binadamu ana dini, Mungu wake alomumba
Kamuwekea imani, moyoni kampa chumba
Akiomba huamini, kishetani kikayumba
Nikikaa nashangaa, binadamu navyong’aa.
Mtunzi: Duncan Mulu
Mahali: Lungalunga
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Diaspora Times Global Sep 19 – Sep 25, 2026
- Tibet’s glacial catastrophe: Behind Beijing’s wall of silence, a climate disaster reshapes a region
- Museveni says Uganda overpaid for fuel through Kenyan middlemen as new terminal breaks ground
- Court orders throw KPL season kickoff into doubt
- Can Kenyans abroad become the untapped force that transforms Kenya?