Jina:Masika Derrick
Lakabu: Dokta Ziro 🇰🇪
Lugari, Kakamega- KENYA.
Simanzi Kenya simanzi, simanzi imetawala,
Ameondoka kipenzi, Kibaki ameshalala,
Yametufika majonzi, kotekote ni risala.
Viliyo Kenya viliyo, viliyo vinasikika,
Bila ya matarajiyo, taifa limekwazika,
Kote ni masimuliyo, ya shujaa kuondoka.
Machozi Kenya machozi, machozi yanamwagika,
Kuzuia hatuwezi, kuliya yatupasika,
Raisi mchapa kazi, mauti yametupoka.
Huzuni Kenya huzuni, huzuni twahuzunika,
Yani tumo taabani, moyoni twasononeka,
Ametuaga jamani, raisi wetu tajika.
Raisi wetu Raisi, Raisi wetu Kibaki,
Tewengu Kenya twahisi, majonzi yametulaki,
Hakika tutakumisi, Raisi usiye chuki.
Ulale pema ulale, ulale wetu shujaa,
Ulipoenda milele, kwetu ulikuwa taa,
Baraka kwako belele, zikuandame shujaa.
Kwaheri Mwai kwaheri, kwaheri ya kuonana,
Peponi pema safiri, kakupenda Maulana,
Hatunawe ni dhahiri, ni vigumu kulikana.