Fatma Ali Mohamed
Wivu ni kubwa husuda, si mwema kwa mwanandamu
Tusiufanye ibada, kwetu sisi si muhimu
Wivu sio kawaida, kwa wengine kubwa sumu
Wivu wa donge haramu, wacha sitafute shida
Wivu huwa wavuruga, mahusiano ya watu
Yakawa yalegalega, kwa vishindo na papatu
Na urafiki huaga, kurudi usithubutu
Wivu kwetu sio utu, marufuku naupiga
Wivu huusha furaha, kwa mtu alionao
Moyo hujaa karaha, na chuki kila uchao
Ikashuka yake siha, uso hukosa mng’ao
Vyema kuachana nao, utakukosesha raha
Wivu kwetu makhuluki, husababisha mizozo
Huweza kuleta chuki, na msongo wa mawazo
Ndo mana siuafiki, una mengi matatizo
Hauachi mikwaruzo, hivyo si mwema rafiki
Wivu huweza athiri, akili ya mwanadamu
Kwa uchungu na kiburi, cha kukosa ufahamu
Kwamba wivu si nzuri, wengi umewagharimu
Kuuwacha ni muhimu, kuwa nao ni hatari
Ewe mja makinika, nakupasha tangu leo
Wivu wa chuki hakika, katu haupandi cheo
Wivu tunaoutaka, ule wa maendeleo
Tuzitupe mbali ndweo, za wivu wenye mashaka
Mtunzi: Fatma Ali Mohamed
Mahali: Pemba