Alfred Lobawoi
Ni siku njema kwa kweli, nimeamka salama,
Bila ya moyo kufeli, au hata kutotoma,
Kwa kani nijihimili, nikaweze kusimama,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Siyo kodi nimetuma, nisakini duniani,
Wala mlango wa nyuma, nakataa abadani,
Hii kwangu ni rehema, zitokazo kwa Manani,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Mosi wapo ikhiwani, wale watu wenye jina,
Wajapo barabarani, kandokando twabanana,
Wote ni sawa jueni, pia wasojulikana,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Si usiku si mchana, uzima kuumiliki,
Kama mtoa dhamana, mwenyewe hatetereki,
Kwangu mimi ni amana, siku zote nasadiki,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Kulikokuwa kisiki, pagumu tena pabovu,
Pa bahati kila wiki, ikiwa mwezi wokovu,
Napaona ni mswaki, angalau nina nguvu,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Sikuonja tunda bivu, bichi ndiyo niliweza,
Haya ndo yangu makovu, ambayo yaliumiza,
Ila afadhali mbovu, yangu kesho ya Muweza,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Ule usiku wa kiza, ambao sikuujua,
Mwenzenu ulinitweza, Mkawini anajua,
Wala haingenisaza, leo hii singekua,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Beti nane napumua, nawakumbuka wandani,
Tuliopiga hatua, na kuwepo safarini,
Kabuti langu navua, daima nawathamini,
Lobawoi nashukuru, umbali huu ni Mungu.
Mtunzi: Alfred Lobawoi
Lakabu: Mweledi Chipukizi
Ruiru.