Wanjohi. P. Mugambi
Sinayo ya samahani, wala eti kukuomba
Ni jukumu mtimani, kusikia nikiamba
Usiposhika yakini, sibiri meno ya mamba
Simtupe mama yako
Miezi kenda tumboni, safariyo lianzia
Alikuwa na imani, mwana akajifungua
Shida za uchunguni, mama alizivumilia
Simtupe mama yako
Alifika spitalini, siku ilipofikia
Ukafika duniani, mama akikwangalia
Ikamvaa usoni, tabasamu ya kimia
Simtupe mama yako
Alikulea jamani, mema akikupatia
Hakulegea ulezini, ulezi alikwamia
Hatua mbele shuleni, mama alikimbilia
Simtupe mama yako
Mama aliubaini, uzuri wake heshima
Hakukudekeza yani, ukakose taadhima
Alikukunja yakini, ukiwa mbichi jama
Simtupe mama yako
Umefika ukubwani, sababu ni yake mama
Ukapaa aushini, popote haukukwama
Uko sasa kileleni, wenzako kishika tama
Simtupe mama yako.
Mama yuko mashambani, msongeni amekwama
Nawe walia jijini, umemsahau mama
Anafia ugongwani, huku akishika tama
simtupe mama yako
Kukuona atamani, akupe macho angaa
Akakutie machoni,mamayo huyu shujaa
Amemtuma jirani, na wewe ukakataa
Simtupe mama yako
Namalizia mwandani, kataana na dunia
Tazama ya kisogoni, likotoka kumbukia
Rejea kwenu nyumbani, mama akusibiria
Simtupe mama yako
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni
Nairobi Kenya