Wanjohi. P. Mugambi
Wana kwenu natamka, maneno yenye hekima,
Kwenu yasijewatoka, haya maneno kwa hima,
Yawe ndo nguzo hakika, kila mnaposimama,
Amani sawa na haki, bila moja ni balaa.
Bila moja ni balaa, amani sawa na haki,
Vyote vina manufaa, kama yale ya akiki,
Ili uitwe shujaa, vyote unaviafiki,
Amani, haki daima, moja haina mwangaza.
Moja haina mwangaza, amani, haki daima,
Moja imejaa kiza, pasi mwenzake nasema,
Ndiposa kukaangaza, vyote twahitaji ima,
Amani na haki pia, msije kuzilegeza.
Msije kuzilegeza, amani na haki pia,
Vitu hivi hupendeza, vikitetewa sawia,
Amani ombi kipaza, haki pia kalilia,
Amani na Haki kweli, tunahitaji wanangu.
Tunahitaji wanangu, amani na haki kweli,
Kulo na haki wanangu, pasi amani kukali,
Na kupo amani tangu, pasi haki ni kukali,
Amani na haki wana, huenda kweli pamoja.
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni
Nairobi Kenya
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER August 15-16, 2026
- Kenya’s dairy sector at a turning point as quality, growth and farmer welfare take centre stage
- From salary to student loans: New bill targets faster repayment of graduate debts
- The ballot must be mightier than the stone
- Engineer James Kemoni eyes Nyamira Governor’s seat on Jubilee ticket