Brian Oigara
Brian Oigara ni mzaliwa gatuzi la Kisii. Ni mwalimu, mshairi, mtafiti, mtafsiri, mhariri na mwandishi. Kama mwandishi, amechangia katika vitabu mbalimbali vikiwemo diwani za mashairi na hadithi fupi. Amechangia katika ‘ Kilele cha Mambo’ , ‘ Tasnia ya Mashairi ‘, ‘ Game of Wits’ , The poems from Africa’ na kazi nyinginezo. Kama mhariri, Brian amehariri kazi kama ‘ Simu ya Ajabu’ , ‘ Nahofia Kesho Yangu’ , Dreams of my Past’ na nyinginezo.Ameandika miswada mingi ambayo iko katika harakati za kuchapishwa.Kama mwalimu, Brian amefunza Kiswahili na Historia katika shule za upili. Amefunza katika Shule ya Mtakatifu Petero, Chironge.Kama mtafiti,Brian ameandika makala mengi ya kihistoria na ya lugha ya Kiswahili ambayo yamechapishwa kwenye magazeti mbalimbali nchini Kenya kama vile gazeti la Taifa Leo.Kwa sasa Brian Oigara ni mhariri na pia mtafsiri. Kielimu, Brian ana shahada ya sanaa katika.Kiswahili na Historia kutoka chuo Kikuu cha Chuka, Tharaka Nithi.
Mume wa Mama
Kutwa kucha huamini, vipi mambo yawe hivyo,
Najua humthamini, humheshimu vilivyo,
Ungelirudi zamani, hungekuwa mtu ovyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Ni mfupi wajameni, na mnene vivyo hivyo,
Hana pesa asilani, kakaukiwa vilivyo,
Kama si yule jirani, jana mngelala hivyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Ni mlevi kisirani, akishalewa ni hivyo,
Huwafukuza nyumbani, mkakikimbia kiovyo,
Huelewi ni kwa nini, mama achague hivyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Usiseme walakini, jinsi ile upendavyo,
Ukamweka kwa mizani, na kumpima visivyo,
Eti kapendewa nini? hebu muache alivyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Chunga usijilaani, nikuambiavyo ndivyo,
Uyaonayo utani, kesho yatakuwa sivyo,
Utakuwa taabani, kama baadhi walivyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Hivi wewe una nini?, au akiliyo rovyo,
Hebu ushike mpini, ukafanye wafanyavyo,
Uyawache ya nyumbani, yabaki jinsi yalivyo,
Mume wa mama jamani, ni baba na ni hivyo.
Mtunzi: Brian Oigara
Lakabu: Malenga Mla Leo
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER July 11-12, 2026
- Karua convoy attacked as police stand aside at Gatoto school
- Touch Ol Kalou poll and your credibility dies with it, Gachagua tells IEBC
- The three-pound organ Kenyans refuse to use during elections
- Merino breaks Belgian hearts as Spain march into World Cup semi-finals