DR Congo
Limeniliza nalia, linalofanyika Congo
Mwanadamu nasilia, na wingi tena msongo
Utu umeshasilia, jina lao songombingo
Naililia Congo
Nitazamapo runinga, mambo huko yanaliza
Japo Kenya yatuganga, huko kwataka mu’jiza
Hata watoto wachanga, vita havijawasaza
Naililia Congo
Alipotuumba Mungu, duniani kutuweka
Alitaka walimwengu, kwa amani kujengeka
Ila watu ni miungu, wengi wamebadilika
Naililia Congo
Wanjohi napiga dua, nikiililia Congo
Naiombea afua, ikaone bila tongo
Kilio wanacholia, Mungu waone Wakongo
Naililia Congo
Nikiomba E Rabuka, ikumbuke pia Kenya
Congo kusikokalika, Kenya nako kunasinya
Ni vifo vyaongezeka, uhai vinavyonyonya
Naililia Congo
Dr. Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni