Vincent Kemboi
By: Wanjohi. P. Mugambi

Jina langu ni Vincent Kemboi, mzawa wa kaunti ya Nakuru eneobunge la Kuresoi – kaskazini mnamo mwaka wa 1990. Nimelelewa kuko huko na hata kuanzia safari yangu ya elimu huko katika shule ya msingi ya Kiptororo. Hapo ndipo mustakabali wangu wa elimu ulipoanzia nilipopatana na walimu walioninoa nikapata makali. Maisha yangu ya shule ya msingi yalinipendeza kwa kujihusisha na michezo mbalimbali ambayo nilipenda kushiriki kama vile Kandanda, Riadha, Mchezo wa kuigiza na Voliboli. Kando na michezo sikuwa mchache pia darasani. Nilipenda sana kutia bidii masomoni ili nibadilishe mazingira ya nyumbani.
Aghalabu changamoto za nyumbani na kukosa karo kulinipa motisha ya kutaka siku moja nibadilishe maisha ya jamaa zangu na hata kwa vizazi ambavyo vingekuja baada yangu. Nilipokamilisha masomo ya shule ya msingi na kukwangura alama 355 uchechefu wa karo bado uliniandama na kutaka kuzima mshumaa wangu elimu. Hayo yaliwasukuma wazazi wangu kunipeleka shule ya kutwa kwa kutoweza kumudu gharama ya shule ya bweni. Kusoma kidato cha kwanza na cha pili kulikuwa balaa wakati mwingine babangu alimsihi mwalimu mkuu kuuza maharagwe na mboga nilikosomea ili nisifukuzwe shuleni ila nashukuru Mungu alisaidia baada ya Mimi kujitahidi nikafua dafu masomoni. Nilijua fika hiyo ndiyo fursa ya pekee kujikwamua kwenye lindi hilo.
Baadaye nilimaliza safari yangu ya masomo chuoni na kuhitimu kwa kupata Digrii ya Uanahabari na mawasiliano. Haya yanaoana na jinsi ambavyo nilivyokuwa katika shule ya upili, nilipopata motisha kutoka kwa rasi wangu; Joseph Tonui ambaye kwa sasa ni mbunge katika eneobunge la Kuresoi kusini. Alitutia motisha na wakati huo kutukaripia kwa ukali mno ila yote yalikuwa ni kwa ajili ya mema siku za halafu. Nakumbuka fika kabla sijajiunga na Chuo kikuu alinitabiria kuwa ninaweza kuwa mwalimu mzuri sana wa shule ya upili kwa kunihimiza na kunipa mwelekeo lakini ari niliyokuwa nayo katika tasnia ya utangazaji haikuruhusu. Baada ya kuwaza nikaona itakuwa vyema nikisomea uanahabari ila baadaye nije nikawe mwalimu wa kufunza uanahabari. Yote hayo yalitokana na uteuzi wangu wa kuchagua vyuo ambavyo ningejiunga navyo. Mathalan mtu huchagua vyuo tofauti kati ya nafasi nne, baada ya mimi kuchagua Chuo cha Nairobi kisha Chuo cha Chuka kikiwa ni chaguo la mwisho. Hata hivyo, sikutamatishia masomo yangu hapo baada ya kuhitimu. Mazoezi yangu ya mafunzo ya nyanjani yalianzia katika baadhi ya vituo vya redio nilipohudumu kwa mda mchache na kituo cha Kass FM pamoja na runinga ya Kaa TV kisha Tamboyat FM na pia kituo cha habari chini ya usimamizi wa Kanisa katoliki. Nafasi hizi za kuchapa kazi katika vyombo hivi vya habari ilikuwa ni kwa minajili ya kutangamana na taaluma yenyewe na nijue yafanywaje. Ukweli ni kwamba nilijua sitakawia sana kufanya kazi katika vyombo vya habari kwa kuwa tayari nilikuwa nimeyatimiza malengo ya kujua kufanya mambo mbalimbali na kujua yanayohitajika.
Mnamo mwaka wa 2018, ndipo nilianza kutafuta nafasi ya kufunza na hapo nikafunzafunza mahali tofauti. Mwaka wa 2020 nikabahatika kujiunga na Taasisi ya Mafunzo ya NIBS kufunza kama mhadhiri wa Idara ya Uanahabari na mawasiliano. Yapata sasa miaka minne tangu nianze kufundisha hapa nilipo. Imekuwa ni safari kweli. Wasemavyo kuwa safari ni hatua. Basi kutokana na juhudi zangu ndipo nikateuliwa kuwa mkuu wa idara ya uanahabari baada ya miaka minne ya uhadhiri. Tangu niteuliwe nimefurahia sana kazi yenyewe.
Isitoshe, katika hali ya kuongeza hadhi yangu ya elimu nilijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea Uzamili katika Uanahabari na Mawasiliano ambapo nilihitimu. Masomo kwangu ni muhimu na kwa yeyote yule apataye fursa anafaa kukumbatia na kuendelea kusoma ili kuwa na ujuzi katika vitu vingi ambako ni kuzuri sana.
Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Nilichochewa na babangu mzazi kuipenda redio. Licha ya kuwa hatukuwa na redio kwa wakati wote babangu alipenda sana kusikiliza vituo kama vile Kass Fm, Chamgei FM na Radio Maisha. Hatua hiyo iliamsha ari ndani yangu nikavipenda vipindi vya vituo hivyo. Nakumbuka katika kituo cha Kass FM nilipenda sana kumsikiliza mtangazaji ambaye ni Joshua Arap Sang. Alikuwa ni mtangazaji mzuri sana na hodari aliyenichochea nitazamie kuwa mwanahabari ambaye ataifaa jamii.
Watangazaji wengine ni Michael Bowen wa kituo cha Chamgei FM aliyekuwa mtangazaji hodari wa soka, Bw Antony Ndiema (Radio Maisha) nilipokuwa namsikiliza enzi zile akiendesha kipindi cha asubuhi kilichoitwa Safari na Ndiema, Geoffrey Mung’ou niliyemjua kama ‘Sauti ya Simba’ ambaye mazungumzo yake yalinifanya nikakipenda Kiswahili na hata Hassan Kauleni ambaye amekilea Kiswahili vyema tangu nilipoanza kumsikiliza katika kipindi chake cha Nuru ya Lugha miongoni kwa wanahabari wengine hapa nchini.
Vilevile nimechochewa na wanahabari wa kimataifa kama vile, Christine Amanpower kutoka shirika la utangazaji la Aljazeera ambaye kazi zake mathalan makala yake yailinivutia mno pindi nilipokuwa nafuatilia. Sisahau BBC Swahili ambapo Mimi hufuatilia kipindi kama vile Amka na BBC. Huko wanahabari kama vile Sarafina Robi, Caro Robi na hata Roncliff Odit hunikosha kwa matangazo yao. Vituo vingine vya kimataifa vinichocheavyo ni VOA Swahili, Radio Uchina – CRI na DW (Deusteche Welle). Kwa kifupi Mimi hupenda sana kupata taarifa kutoka kwa aina tofauti ya vyombo vya habari, si redio si runinga na si magazeti. Mfano hai ni gazeti la The Guardian, Taifa Leo, The Standard, The Star nk. Nafasi hii ya uhadhiri inanipa msukumo wa kupenda kusoma ili nitaalamike katika taaluma hii ya uanahabari; nijue muundo wa jinsi wanahabari wanavyofanya kazi, mbinu zao ni zipi na mengineyo yanayohusu taaluma hii.
Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Kile ambacho kinanipendeza katika kazi yangu ni kazi yenyewe na fursa niipatayo ya kuwanoa vijana ambao wanataka kuwa na ujuzi katika taaluma ya uanahabari. Pia wanafunzi wengi kupitia mikononi mwangu na kutarajia wengine zaidi kupitia mikononi mwangu na kuhitimisha masomo ya chuo, hayo kwangu huwa nayaonea fahari kuchangia katika makuzi ya taaluma yao ya uanahabari.
Mintarafu ya hayo masomo ambayo Mimi hupenda kuyafunza chuoni kama vile Media Law and Ethics, Sports for Journalism hunikosha sana. Mengine ni Online Journalism, Freelance and Feature Writing, Communication Research, Introduction to Media, Media Ethics, Media and Society, Radio Production na mengineyo.
Halikadhalika Mimi pia ni mwanachama chini ya usimamizi wa Baraza la Vyombo vya Habari hapa nchini (MCK) ambapo nimeidhinishwa rasmi na kupata nambari ya usajili jambo ambalo linanitia moyo kuchapa kazi vilivyo.
Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.
Natanguliza kwa kusema kuwa maisha yangu ya awali hayajakuwa mazuri sana. Yalikuwa mabaya. Ila yalivyo maisha kuwa na changamoto zake hazikosi popote pale. Kwangu nitangamanapo na wanafunzi wa aina tofauti wanaohitaji ushauri ambao ni wenye hulka mbaya ambapo hubidi kuwalete karibu na kutafuta mbinu ya kuwashauri wasipotee kimaadili. Baadhi yao huwa ni kana kwamba wameshurutishwa kusoma jambo ambalo hunitia jukumu la kuwasaidia wazazi ili wanafunzi waelewe lengo lao la kuwa shuleni. Wakati mwingine huwa ni vigumu sana mwanafunzi anapokataa kusoma naye mzazi kwa upande wake angependa sana huyo mwanafunzi asome, kusawazisha huko huniwia vigumu.
Kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Huwa ninashirikiana na mtaalamu wa ushauri nasaha chuoni hasa kuzishughulikia malalamishi ambayo yameletwa na wanafunzi. Nafasi ya kuzuru maeneo tofauti nje ya chuo pamoja na marafiki husaidia kuziepuka na kukabiliana na changamoto hizo. Hayo husaidia afya ya akili na kuyeyusha msongo wa mawazo.
Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe?
Ushauri wangu ni kuwa uanahabari ni taaluma nzuri sana lakini ni vizuri ufanye kama una ule msukumo ndani yako. Isiwe kwamba kuna mtu alikulazimisha kusomea kwa kuwa ni tofauti na taaluma nyingine. Ukilinganisha na taaluma ya Polisi au ualimu ambayo huwa rahisi kupata kazi, uanahabari unahitaji wewe mwenyewe kujitolea mhanga.
Teknolojia ya sasa pia imerahisisha mambo. Mitandao ya kijamii imetoa fursa ambapo sasa si lazima mtu asubiri ajira kutoka kwa shirika la utangazaji bali anaweza akufungua ukumbi wa YouTube na mitandao mingine ili kufanikisha kazi yake. Ni watu wengi hawataki kuajiriwa kwa sababu kazi za mitandaoni zawapa hela nyingi.
Yeyote asife moyo. Huenda ukapata usaidizi wakati ambapo hautarajii. Siku hizi hela za kufadhili masomo kwa vyuo vipo na pia huenda yeyote abahatike na wafadhili jambo ambalo litachochea masomo ya mtu hadi atakapohitimu.
Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?
Ningetamani sana kubadilisha uongozi. Viongozi ambao tuko nao ni wanaojali maslahi yao. Kwa yakini kama tungekuwa na uzalendo na kupendana au hata kuwajali wengine, iwe tunafanya jambo lakini lisiathiri wengine kwa njia mbaya basi ingekuwa sawa. Ukweli ni kuwa tukiwa na viongozi ambao nia yao sio tu kujitajirisha bali kuhakikisha wale wanaowaongoza wafanyiwe kazi vizuri tutakuwa tumepiga hatua.
Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?
Ninapatikana kwenye mtandao wa Facebook (Vincent Kemboi) Tiktok (Vincent Kemboi) Linked In (Vincent Kemboi)
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- When advocacy meets politics: Crystal Asige’s removal raises questions about representation and inclusion
- KEMSA chief reaffirms commitment to accountability before Senate health committee
- Lucy Muchoki champions strategic partnerships to unlock healthcare investment and private sector growth
- Gachagua steps up consultations as DCP intensifies recruitment drive
- Tharaka University lecturer honored after guiding to historic Huawei ICT global victory