Leonard Mambo Mbotela
Kenya yetu inalia, inalia Kenya yetu
Ameiaga dunia, nchini mmoja wetu
Pengo alotuachia, hawezi mwingine mtu
Ameondoka Mbotela, Je huu ni uungwana
Kifo leo nakuliza, je huu ni uungwana
Wanakenya metuliza, na Mbotela kuachana
Umeshazima mwangaza, sisi tunalia sana
Ameondoka Mbotela, je huu ni uungwana
Hatukulijua jama, hili ndo lingetufika
Mmoja wa wale wema, kwetu sisi akauka
Yakini pengo waama, nani ataziba fika
Ameondoka Mbotela, je huu ni uungwana
Kinalia Kiswahili, kimepoteza mkweli
Mtetezi wake kweli, amemtwaa Jalali
Hivi kifo ni ukweli, yeyote unakabili?
Ameondoka Mbotela, Je huu ni uungwana
Inalia Tasnia, kwanza uanahabari
Kote wengi wanalia, amemaliza safari
Moyoni utasalia, na yako hekima heri
Ameondoka Mbotela, Je huu ni uungwana
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni