Mhakiki: Gitonga Brian
Kitabu: Doa la Ndoa na Hadithi Nyingine
Mchapishaji: Literary Editors Africa
Kurasa: 102
UTANGULIZI
Antholojia ya Doa la Ndoa na Hadithi Nyingine ni mkusanyiko wa hadithi fupi zilizoandikwa na waandishi tofauti wakiwemo Gitonga Brian Murimi, Maera Ezekiel, Hesbon Otolo, Kinya N. Gitonga, na James Situma. Japokuwa waandishi hawa ni chipukizi katika utunzi wa fasihi ya Kiswahili, wamedhihirisha ustadi mkubwa wa kuumudu utanzu wa hadithi fupi. Kwa mbinu, mitindo, na mitazamo mbalimbali, waandishi hawa wamesimulia visa tofauti, baadhi vikiwa vimechochewa na matukio ya kweli. Antholojia hii imehaririwa na Joy-rose Ochieng pamoja na Gitonga Brian na kuchapishwa na Literary Editors Africa mwaka wa 2024.
Mkusanyiko huu umechora taswira halisi ya hali mbalimbali zinazowakumba watu pamoja na jamii mbalimbali kote barani Afrika. Aidha, kazi hii imeweka wazi jinsi mifumo ya ufisadi na ukosefu wa maadili katika mataifa yanayoendelea inavyowasababishia vijana mahangaiko kila uchao. Waandishi wameonyesha jinsi mifumo hiyo inavyowasukuma vijana kujihusisha katika mambo haramu ili kufanikisha ndoto zao bila kujali hatari zinazowakondolea macho. Isitoshe, kupitia wahusika na mazingira mbalimbali, waandishi wamefanikiwa kusawiri tofauti za matabaka katika jamii nyingi za Kiafrika.
Antholojia ya Doa la Ndoa na Hadithi Nyingine imeangazia masuala magumu ambayo kiuhalisia huwasababishia wanajamii tumbo joto.Katika hadithi ya Doa la Ndoa, mwandishi ameangazia suala la unafiki katika ndoa. Petro anampenda mkewe Kicheche kwa dhati lakini Kicheche anamdhulumu kihisia na kumhadaa hadi Petro anampa mali yake yote. Aidha, Kicheche ana uhusiano wa kimapenzi na mhubiri aliyehalalisha ndoa yao. Hali inazidi kuzorota hadi Petro anapogundua kuwa Tinke, mtoto aliyemfikiria kuwa mwanawe, si wake halisi. Badala yake, Iskarioti, rafikiye wa kufa kuzikana, ndiye baba mzazi wa Tinke na ujauzito alioubeba Kicheche.
Halikadhalika, anthoilojia hii imeangazia nafasi ya mwanamke katika jamii nyingi za Kiafrika. Katika hadithi ya Minong’ono ya Uvumilivu, mwandishi Kinya N. Gitonga amemtumia mhusika Asha kusawiri hali ngumu zinazowakumba wanawake katika ndoa zilizotopea manyanyaso kwa sababu ya misingi duni ya ubabe dume. Asha ni mwanamke shupavu ambaye licha ya changamoto alizokumbana nazo katika ndoa yake na Omari, anajinasua na kuibukia kuwa mshindi. Hatimaye, anaanzisha warsha za kuwahamasisha wanawake kupinga dhuluma za kinyumbani.
Zaidi, antholojia hii imeakisi maisha ya vijana wengi jinsi yalivyo chuoni na ata baada ya chuoni. Mwandishi Maera Ezekiel kupitia hadithi yake ya Kisasa, ameonyesha jinsi vijana wengi hujipata wamenaswa katika mitego ya anasa na mapenzi ya kiholela yanayowatia taabani. Hii inadhihirika kupitia mhusika Anita, ambaye anajihusisha kimapenzi na Gavana Mateka Kuteka. Gavana anampachika Anita ujauzito ambao baadaye anaukana, kando na kumwambukiza ugonjwa wa UKIMWI. Kwa kutamauka, Anita anajitoa uhai kwa kuruka kutoka kwenye kilele cha majumba mojawepo ya chuoni.
Mbali na hayo, katika Hatima ya Tamaa, mwandishi Gitonga Brian Murimi ameonyesha jinsi tamaa ya mafanikio ya haraka inavyoweza kuwaangamiza vijana. Zawadi, mhusika mkuu, anafuzu chuoni kwa shahada ya kwanza lakini anakataa kazi ndogo ndogo akiziona kuwa duni. Badala yake, tamaa ya maisha makubwa inamfanya kumsaliti Ntuma, aliyemsaidia kwa hali na mali, na kumfuata Marcson ambaye anamhadaa. Hatimaye, Zawadi anakamatwa jijini Heathrow kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya.
Isitoshe, swala la ubaguzi wa kijinsia limeangaziwa kwa undani katikia antholojia hii. Katika hadithi ya Nyumba ya Jahanamu yake Hesbon Otolo, suala la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto limeangaziwa kupitia mhusika mkuu, Melisa, anyenyanyaswa na baba wa kambo baada ya kifo cha babake mzazi. Hali hii inamfanya apoteze furaha ya utotoni na kumsababishia mahangaiko mengi. Hadithi hii inatoa wito kwa wazazi na jamii kwa jumla kutosalia kimya na badala yake kukemea dhuluma dhidi ya watoto.
Halikadhalika, kazi hii imeangazia unyanyapaa wa kitamaduni unaowakumba watoto kupitia hadithi ya Maotea, yake James Situma. Katika hadithi hii, mwandishi ametathmini mgongano kati ya mila potovu na maendeleo ya kijamii. Dhana ya maotea, inayomchukulia mtoto wa kwanza pacha kuwa nuksi, imeangaziwa kwa kina. Mhusika mkuu anapambana na unyanyapaa huu na hatimaye anafanikiwa kupitia elimu. Hadithi hii inalenga kuhamasisha jamii kubadili mitazamo potovu na kukumbatia haki za binadamu.
Mbinu mbalimbali za lugha zilizotumika katika antholojia hii zinaongeza ladha ya mkusanyiko huu. Baadhi ya mbinu walizotumia waandishi ni tashbihi, methali, misemo, chuku, sitiari bila kusahau taharuki inayomchochea msomaji kutaka kujua mengi zaidi.
Ni bayana kuwa antholojia ya doa la ndoa na hadithi nyingine ni kazi iliyojaa mafunzo chungu nzima kuhusu hali mbalimbali za maisha. Kando na hayo, ni mkusanyiko unaosisitiza umuhimu wa maadili mema, subira, elimu na nafasi sawa katika jamii.
Maudhui
Maudhui mbalimbali yamejitokeza katika antholojia ya Doa la Ndoa na Hadithi Nyingine. Maudhui haya yanaangazia masuala tofauti yanayoiathiri jamii kama vile ndoa, unafiki, ukosefu wa ajira, mila kandamizi, unyanyasaji wa kijinsia, na usaliti. Waandishi wamefanikiwa kuwatumia wahusika kusawiri hali mbalimbali zinazoikumba jamii kupitia maudhui yafuatayo:
(i) Ndoa na Unafiki
Katika Doa la Ndoa, mwandishi Gitonga Brian amebainisha unafiki unaojitokeza katika ndoa za Petro na Kicheche pamoja na Iskarioti na Waridi. Mwandishi ameonyesha jinsi mhubiri aliyepaswa kuishi kwa mujibu wa mafunzo ya kidini anavyogeuka kuwa mnafiki na hata kuazimia kuvunja ndoa ya Petro. Vilevile, Iskarioti anamsaliti rafikiye Petro kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kicheche na hivyo kumsaliti mkewe Waridi. Hali hii inaakisi taswira halisi ya ndoa nyingi zinazoathirika kutokana na ukosefu wa uaminifu na maadili.
ii) Tamaa na Madhara Yake
Katika Hatima ya Tamaa, Gitonga Brian ameangazia athari za tamaa ya kutaka kutajirika haraka miongoni mwa vijana. Kupitia mhusika Zawadi, mwandishi anaonyesha jinsi ukosefu wa ajira unavyowafanya vijana wengi kushawishika kutafuta maisha ya kifahari bila kujali njia wanazotumia. Baada ya kufuzu chuoni kwa shahada ya kwanza, Zawadi anapuuza kazi halali anazoziona kuwa duni. Tamaa ya maisha bora inamfanya kumsaliti Ntuma, aliyemsaidia kwa hali na mali, na badala yake kuolewa na Marcson ambaye anamhadaa. Hatimaye, Zawadi anakamatwa jijini London kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya.
(iii) Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji wa Watoto
Katika Nyumba ya Jahanamu, mwandishi Hesbon Otolo ameangazia suala la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto. Melisa, mhusika mkuu, anakumbana na unyanyasaji wa baba wa kambo, hali inayomfanya apoteze furaha ya utotoni. Pamoja na changamoto hizi, jamii inayomzunguka inakosa kuchukua hatua kumlinda, jambo linaloonyesha jinsi unyanyasaji wa watoto unavyopuuzwa katika jamii nyingi. Hadithi hii inatoa wito kwa wazazi na jamii kwa jumla kutokaa kimya bali kukemea dhuluma za aina hii.
(iv) Unyanyasaji wa Wanawake
Katika Minong’ono ya Uvumilivu, mwandishi Kinya N. Gitonga amemtumia Asha kuwakilisha wanawake wanaovumilia manyanyaso ya ndoa. Asha anakumbana na unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia kutoka kwa mumewe Omari. Licha ya mateso haya, anajikakamua kumlea mtoto wake katika mazingira magumu. Hatimaye, Asha anapata ujasiri na kujinasua kutoka kwenye ndoa ile dhalimu na kuanza maisha mapya. Mwandishi anahimiza wanawake walioko katika hali kama ile kuchukua hatua za kujikomboa badala ya kuvumilia mateso kwa hofu ya unyanyapaa wa kijamii.
(v) Mgongano wa Mila na Maendeleo
Katika hadithi ya Maotea, James Situma anatathmini mgongano kati ya mila potovu na maendeleo ya kijamii. Dhana ya maotea, ambayo inamtaja mtoto wa kwanza pacha kama nuksi na kulazimisha auawe ili kuondoa mkosi, imeangaziwa kwa kina. Mhusika mkuu anakumbana na unyanyapaa na dhuluma kutokana na imani hii ya kimila. Hata hivyo, anafanikiwa kujikomboa kupitia elimu. Mwandishi anatoa ujumbe wenye nguvu unaowataka watu kupinga mila kandamizi na kushinikiza jamii kukumbatia haki za binadamu na maendeleo ya kijamii.
vi) Umasikini na Athari Zake kwa Wasomi
Katika hadithi ya Kisasa, mwandishi Maera Ezekiel anazungumzia umasikini na athari zake katika maisha ya wasomi katika vyuo kupitia wahusika Anita na Olado. Anita, atokaye familia masikini anaingiwa na tamaa ya kuishi maisha makubwa na hivyo anajihusisha katika uhusiano wa kimapenzi na Gavana Mateka Kuteka anayempachika mimba na kumwambukia ugonjwa wa UKIMWI. Kinyume naye, Olado anawakilisha vijana wanaojitahidi kwa uadilifu na hulka njema Hadithi hii inaonyesha migongano ya maadili, tofauti za kimatabaka na madhara ya tamaa, huku ikisisitiza umuhimu wa kuwa na subira maishani.
HITIMISHO
Antholojia ya Doa la Ndoa na Hadithi Nyingine ni mkusanyiko wa hadithi fupi zinazoakisi masuala halisi yanayozikumba jamii nyingi za Kiafrika. Kupitia masimulizi ya waandishi, msomaji anapata fursa ya kutafakari kuhusu mambo mazito kama vile ndoa na unafiki, tamaa na madhara yake, ukatili wa kijinsia, unyanyapaa wa kitamaduni, na unyanyasaji wa wanawake.
Hadithi hizi zinaakisi matukio yanayoonekana katika jamii huku zikiwahamasisha watu kuyakabili kwa ujasiri, ukomavu na busara. Taharuki na ustadi wa lugha iliyotumika katika usimulizi iliniteka tangu mwanzo hadi mwisho wa kitabu hiki. Ninawahimiza wanajamii wote kujipatia nakala ya kitabu hiki na kushuhudia utunzi wa kipekee.