Naliweka paruwaja, hima mpate sikia
Siambi yenye vioja, makini mkatulia
Tukajifunde pamoja, mambo ya hini dunia
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Moja yake urafiki, ambao hima bandia
Ulojaa unafiki, hapa na pale tambua
Ukapaliliwa chuki, bila ya kutamania
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Niambe yale mabaya, watendayo walimwengu
Pasi kuwaza duniya, kesho itaketa ukungu
Wakasaliya kuliya, kilaani ulimwengu
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Kunao wale wenzetu, maovu wamevamiya
Ukiwaambia utu, ni kito kujivuniya
Wanasisitiza katu, nasaha kuambiliya
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Kuna wao viongozi, ahadi wanazijua
Maneno kwao ni ngozi, tamu nje mkijua
Ila zimeoza wazi, huwezi kutamania
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Mambo ya hini dunia, yataka kuangalia
Si ilimu, kazi pia, nazo pia familia
Sekta hizi mkajua, zataka kuangazia
Dunia hii ya leo, ina mengi nawambia
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Diaspora Times Global Sep 26 – Oct 2, 2026
- RS South Africa supports next-generation edge AI with NVIDIA Jetson Orin Nano 2
- AFRICLOUD opens Lagos region and local-currency payments across African markets
- Fine Spinners targets Kenya’s US apparel supply chain with $5m investment
- Nuclear energy debate must begin with public trust and shared responsibility