Momanyi Henry Rioba
Leo hii nawajia, zani nikiwabwagia,
Hili linanisumbua, ‘mebidi kuulizia,
Majibu natarajia, nipeni nitaridhia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
1.
Taswira najichorea, ila sijapendelea,
Hadhi imekushushia, na bado waendelea,
Kifua wakitanua, hukomi kuibugia
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
2.
Wanao wakushangaa, unavyo jikojolea,
Matusi unayatoa, pasi umri kujalia,
Na haja wajiendea, pasipo nayo kujua,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
3.
Majukumu yamejaa, huoni walimatia?
Kisha utatukujia, msaada kuombea,
Hila ukimiminia, shetani kumsingizia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
4.
Kweli imekuvutia, mwilini ‘mekuingia,
Familia ‘mepuzia, kilabuni waotea,
Pingu umejiwekea, mwenyewe kujitakia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
5.
Ni sumu unabugia, hata mwenyewe wajua,
Sikio pamba ‘metia, ushauri wapuzia,
Ni bure kwako wosia, hujali kutusikia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
6.
Hadhi unajishushia, jamii yakuchekea,
Hakika wajichimbia, kaburi kuiingia,
Na usipotusikia, ndwele zitakuvamia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
7.
Ombaomba umekua, mtaani wasumbua,
Na wote wamekujua, kwa mbovu hiyo tabia,
Rafiki wakukimbia, pekee utasalia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
8.
Kila tendo wakosea, huwezi makinikia,
Wazazi wawakosea, kwa kutowatembelea,
Huna cha kujivunia, ila unachobugia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
9.
Beti kumi nafikia, kadi tama ninatua,
Uliko we fikiria, jawabu kujipatia,
Iwapo wafurahia, kaburi wajichimbia,
Ina faida gani, pombe unayokunywa?
10
JINA: Momanyi Henry Rioba
LKABU: Malenga Mtanashati
ENEO: Kesogon