Mhakiki: Alfred Lobawoi
Mchapishaji: African Ink Publishers
Kuka na Kuku ni aina ya hadithi ya Hurafa. Hadithi za hurafa ni aina za hadithi ambazo wahusika wake ni wanyama. Ni kupitia wanyama wenyewe ambao hupewa tabia na vitendo vya kibinadamu. Katika muktadha huu tuna mhusika mkuu ambaye ni Kuka ambaye anawakilisha binadamu na Kuku ambaye anawakilisha ndege.
Mwandishi wa kitabu hiki ambaye ni Timothy Omusikoyo Sumba, ameteka msomaji kupitia anwani ya kitabu hiki ambacho ni cha fasihi ya watoto anapocheza na maneno. Namaanisha jinsi alivyofuatanisha maneno, ‘Kuka na Kuku’ haya ni maneno mawili ambayo ukitamka yanatatanisha. Ni vitate hasa. Watoto huvutiwa na maneno kama haya kwa kuwa huteka mawazo na hisia zao. Mathalan utampata mtoto akisomasoma anwani ya kitabu hiki na kutazama zaidi. Hadithi hii sisimuzi imetumia mtindo wa mazungumzo kwa wingi ambapo mhusika Kuka anazungumza sana akitaka kujua baadhi ya mambo, kuuliza maswali na majibu. Haya yanavuta makini ya msomaji kutaka kujua zaidi ni nini kinaendelea au kitakachotokea baadaye.
Hadithi hii imefaulu kuangazia baadhi ya mambo mengi ambayo yamejikita si tu kwa mhusika mkuu bali pia katika mazingira anayoishi. Mosi, Kuka anasawiriwa kuwa mhusika ambaye ni mbaraza na mtu ambaye anapenda kujua zaidi kuhusu vitu mbalimbali. Kuka ambaye anafanya urafiki na Kuku anaamua kumjua Kuku zaidi kwa kumwuuliza maswali. Mkabala huo wake unamfanya kuwa na jukwaa la kujifunza hata zaidi. Mfano ni mahali ambapo Kuka alikutana na Kuku kwa mara ya kwanza. Yeye mwenyewe alikiri kuwa mnyama anayempenda ni Kuku. Hapo ndipo alipata maelezo zaidi kuhusu Kuku na kufurahi ajabu.
Ubaraza wa Kuka unaonyesha kuwa katika jamii ndiyo baadhi ya hulka ambayo hutufanya tupate ujuzi wa mambo kupitia wenzetu. Kuna baadhi ya mambo hatuwezi tukayajua iwapo hatutajihusisha na watu. Pili, mwandishi ameonyesha wazi mapenzi aliyonayo Kuka kwa wanyama au niseme ndege. Mhusika huyu anathamini ndege kiasi cha kujua kunga za ufugaji wao hasa wakati ambapo Kuka anawalisha ndege nafaka, Wadudu, Nyasi na hata vyakula vya viwandani. Pia anawatilia maji safi kwenye vyombo safi. Yote hayo yanadhihirisha kuthamini ndege na hangetaka waishi bila kusaidiwa na kuangaliwa. Katika uzi huo huo pia anawashughulikia ndege kwa masuala ya kuchanjwa ili wasiugue magonjwa kama vile, Kideri ambao ni ugonjwa wa kuharisha na kufanya kuku kufa ghafla.
Mhusika mkuu pia amejifunza zaidi tofauti iliyopo baina ya kuku wa aina tofauti. Mfano baada ya Kuka kukutana na Mangisi alijua fika kuwa ni kuku ambaye ana manyoya yaliyosimama mwilini. Pia alijua kuwa jina jingine lake ni Nungu au Kinyaunyau. Mbali na hayo pia alijua tofauti kubwa iliyopo kati ya Kware na Kuku ambapo Kware huwa porini na si wa kufugwa nyumbani ilhali kuku hufugwa nyumbani.
Jambo jingine ni jinsi ambavyo mhusika mkuu alivyo na bidii. Kutaka kujua zaidi. Utafiti wake wa kina unatia moyo zaidi kwa watoto wa kiwango chake wakianza kuonyesha uelewa wa baadhi ya mambo na kuanza kudadisi. Huo unaonyesha jinsi watoto wanavyokuzwa katika mazingira mazuri ya ujifunzaji bila kuwekewa kikwazo cha kujifunza.
Kazi hii pia imeonyesha jinsi teknolojia inavyohusiana na kilimo hasa wakati ambapo mayai hutiwa kwenye viangulio ili kupata vifaranga. Mbinu hii husaidia sana wakulima hasa wanaotaka kukuza wanyama wao haraka ili kuwahi soko. Hapa mwandishi alitumia msamiati aliposema kuwa “Kuku huniangua baada ya kuotamia mayai kwa siku ishirini na moja. Wengine hutumia viangulio au vitotoa.” misamiati hii ni faafu mno kwa masuala haya ambayo yatawapevusha watoto waelewe zaidi misamiati hii ya ukulima wa kufuga wanyama. Pia ni katika hatua hii ambapo neno ‘lalia mayai’ badala ya ‘otamia mayai’ yatatokomea baada ya wengi kujua neno sahihi.
Mbali na hayo ni dhahiri shahiri kuwa pana uhusiano wa karibu mno baina ya ndege na binadamu. Kando na malezi mazuri ya ndege hao wanaoishi nyumbani, pia wanahusishwa na kuwatembelea majirani kwa minajili ya kusherehekea karamu. Huu ushirikiano unaonyesha umoja katika jamii. Ndege na binadamu hakuna yule ambaye amejitenga. Kuka alikuwa anatenga mda wake mwingi na Kuku ambaye alikuwa ni rafiki yake wa dhati. Kulingana na hadithi alikuwa anapendezwa sana na maelezo ya kuku wa aina tofauti kuhusu maisha yao na hata kujifunza mambo chungu nzima.
Utamaduni haujaachwa nyuma umedumishwa mno katika hadithi hii. Mwandishi anaposema kuwa Kuka aliwaandalia wageni wake vyakula vya kiasili. Inaonyesha kuwa katika familia ya kina Kuka inawezekana sana kuwa wanakuza vyakula hivyo shambani. Jinsi wanavyouenzi utamaduni kunawapa msukumo wa kula vyakula vya kiasili na hata kuwafuga wanyama wa nyumbani. Halikadhalika mazao wanayopata shambani ndiyo hiyo ambayo wao hutumia kuwapa ndege wanaowafuga nyumbani ambo ambalo linaonyesha jinsi jamii inavyopambana na ukosefu wa vyakula kutokana na gharama ya vyakula dukani.
Aidha, mbinu nyingi za lugha zimetumika katika ufanikishaji wa kazi hii. Si uhaishaji ambao unajitokeza wakati ambapo Yai lilikuwa linazungumza na Kuka likamwambia kuwa “Mimi hutagwa na kuku. Wengine hudai ndimi mzazi wa Kuku.” Mbinu nyingine ni chuku ambapo mwandishi ametumia baadhi ya kauli kuongeza ladha kwenye hadithi, taswira pia imetumika katika hadithi hii kwa kujenga picha akilini, maswali balagha na mbinu ya kisengere nyuma. Mbinu hizi zimefanya kazi hii kuwa na mashiko na mvuto wa kipekee kwa kuvuta hisia za msomaji anaposoma mwanzoni hadi mwisho.
Kwa jumla niseme ni kazi iliyosheheni ucheshi mwingi. Baada ya kila hatua Kuka kukubaliwa kuwa rafiki wa Kuku na wengineo katika kazi hii anafurahi mno. Mtindo wake wa kuuliza maswali utakuvunja mbavu. Ni kupitia mbinu hii ambapo Kuka alijifunza baadhi ya majina ambayo hakuwa anayafahamu. Ukweli ni kwamba alijichotea maarifa si haba. Kwa upande mwingine pia utashangazwa na kazi hii na jinsi mwandishi alivyomkuza mhusika mkuu kiasi cha kuwa mwepesi wa kutaka kujua vitu vingi. Si rahisi watoto wa kawaida kutaka kujuajua mambo haraka haraka hivyo. Hali hii inaonyesha jinsi watoto wa kisasa walivyoogelea kwenye teknolojia ya kisasa na kujifunza mambo mengi. Ubunifu kama huo wao utaifaa jamii kwa hali na mali na kurekebisha mambo mengi ambayo yalikuwa na utata hasa kimawazo.
Tamati, funzo katika kazi hii ni kwamba ukitaka kujua kitu kuhusu kitu lazima uwe tayari kukitafuta kitu hicho. Kuka amedhihirisha hayo katika kazi hii kwa kuonyesha ujasiri na bidii. Vilevile kutangamana kwake na Kuku na kuwa na mkabala mzuri kumemsaidia kujifunza mambo mengi. Hii ni kazi ambayo itampendeza yeyote yule anayezamia si tu watoto wa kitembo cha chekechea ambao ni hadhira lengwa bali pia mpenzi wa fasihi ya watoto. Michoro mizuri, lugha sahili pamoja na misamiati mizuri vyote hivyo vitamjenga. Watoto wadogo hawana budi kutanua wigo wao watakapodiriki kuonja hadithi hii.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Spain are world champions again as Torres shatters Messi’s farewell dream
- When the songs fade, the wounds remain: The human cost of Ol Kalou’s by-election
- From Sleepless Nights to New Beginnings: How Community Kindness Restores Hope and Dignity to Widows
- A voice of compassion, service, and hope
- New York’s mayor mulls Netanyahu arrest as UN summit looms — and the world holds its breath