Kyelanzi Matei
Yeye ni mwandishi wa kazi bunulizi. Ameandika novela, riwaya, hadithi fupi na ametunga mashairi mengi ambayo baadhi yamechapishwa katika gazeti la taifa Leo. Amehitimu na shahada ya ualimu katika somo la kiswahili na historia kutoka chuo Kikuu cha Egerton bewa kuu la Njoro- Nakuru.
Baadhi ya kazi zake ni pamoja na novela ya Siri ya mwanachimba, tamthilia ya Waridi, ushairi komavu kitabu cha kudurusu. Diwani ya Tungo za Ukruba. Antholojia ya Majini wa Mijini na hadithi nyingine, Mwisho wake na hadithi nyingine, kijito cha Rehema na hadithi nyingine miongoni mwa hadithi nyingi ambazo zipo kwenye matbaa tofauti tofauti.
Kwa Sasa Matei anafundisha shule ya upili ya Tumaini katika kaunti ya Nyandarua – Olkalou.
Waliomchochea katika utunzi wake ni Assumpta K. matei Kwa umbuji wake katika fasihi hasa “Fani ya fasihi” kitabu ambacho kimejaa ukwasi wa lugha. Aidha, Timothy Sumba, Frank Orina, Alfred Lobawoi, Malenga kitunguu machoni, kaka Fred, Akinyi Odhiambo( mwalimu Tumaini) pamoja na marafiki wa karibu kama vile Sharon Obanda, Akuti, onesmus Katana miongoni mwa wengine.
MLALAO GARINI!
Yakera hii tabia, mlonayo pulikeni
Hata haujatulia, kichwa kimo kifuani
Tayari amesinzia, ang’orotea garini
Komeni hiyo tabia, hatuipati amani.
Hatuipati amani, mingurumo kila Kona
Mate yatoka kinywani, pono mmezama sana
Hata kijasho usoni, hutoka kutona tona
Kuweni macho njiani, hiyo huluka wacheni.
Hiyo huluka wacheni, utalala kitandani
Keti kitako kitini, usubirie mwendani
Kulala huku jamani, kumetuchocha yakini
Nzi atuapo ndani, utamlaumu nani?
Utamulaumu nani, vitu vyako kiibiwa
Garini wamo wahuni, hatari wa kuchukiwa
Wanashukia ndiani, hawafiki kwao juwa
Upweke utakupata, ukibaki bila kitu.
Ukibaki bila kitu, ni hiari yako wewe
Duniani Kuna watu, wanokutia kiwewe
Na hutowaona kattu, umeketi nao wewe
Tabia kulala ovyo, ikomeni abiria.
Ikomeni abiria, wenye urahibu huo
Pumzi mnashushia, tunashindwa na pumuo
Kuwa macho nawambia, tena nasema kwa tuo
Tuweni wema garini, tusilale ja maiti!
Tusilale ja maiti, zinatosha beti zangu
Isikupate laiti, naondoka wangu wangu
Shikeni japo katiti, niloyalonga ya kwangu
Tudumisheni nidhamu, tusafiripo vyomboni.
Mtunzi: Kyelanzi Matei
(Mwanakinda)
Tumaini, Olkalou, Nyandarua
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Humbelani Priscilla Nemanzemba: Building Africa’s entrepreneurial future, one business at a time
- Salary: The sweetest contraceptive ever invented
- The green tide: How Gachagua is reshaping Kenya’s political landscape ahead of 2027
- The power of small words
- The price of a job: How Kenya’s public employment system became a political marketplace