Ezekiel Nzeke James
By: Wanjohi. P. Mugambi
- 1. Hebu tueleze mengi kukuhusu
Naam, jina langu ni Ezekiel Nzeke James almaarufu Karma ila kwenye utunzi ni “Mikoba ya Babu”, mtoto wa pili wa Bi. Jacinta Kamene na marehemu Bw. James Mutinda. Mimi ni mzaliwa wa mwanzo wa karne ya 21 kijijin Kivovwe, eneo bunge la Kibwezi magharibi, kaunti ya Makueni. Nilijiunga na shule ya msingi ya kutwa ya Sekeleni ambapo nilisoma hadi kumaliza darasa la nane na kufaulu kulingana na matarajio yangu nikifanya vizuri sana katika somo la Kiswahili nililofunzwa na Mwalimu mstaafu Bw. Lole. Baada ya hapo nilijiunga na shule ya upili ya wavulana ya Nguumo ilioko karibu sana na kwetu,shule yenyewe sikuipenda na hayakuwa matarajio yangu kusomea hapo ingawa nilijitahidi hadi nikamaliza kidato na nne na kupata alama ya D-, maisha yakawa magumu zaidi sasa, nikaingia mtaani na kufanya kazi sehemu kadha wa kadha kwa mwaka mmoja na baadaye kwa akili zangu na ushawishi wa mjomba wangu Jacob Komu nikarudi shule ya kutwa ya Mtakatifu Simoni ilioko Kibwezi katika kidato cha tatu na hapo ndipo nilijitahidi hadi kidato nne na kufanya mtihani wa K.C.S.E na kufanya vyema na ndoto ya kuingia chuo kikuu ikatimia. Hatimaye nilijiunga na Chuo Kikuu cha Murang’a ambapo nafanya shahada ya kozi ya ualimu wa somo la Kiswahili na Giografia. Nilijiunga na vikundi mbalimbali kama vile MUT debate club, MUKSA, MUTCU ila kuna kimoja kilifaa zaidi kiitwacho CHAKIMUT(Chama cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Kiteknolojia Cha Murang’a) nilichokijua kupitia Vincent Mutunga, Rafael Tuju na Samuel Mungai, kupitia hawa utunzi wangu wa mashairi ulipiga hatua kubwa sana na sasa mashairi kadha uchapishwa katika gazeti la Taifa Leo.
- Nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Ushairi huu kwangu una historia kwa kuwa niliujua kupitia mamangu mzazi aliyependa sana kunikariria mashairi ya enzi zake akiwa shuleni, kwanza nilijua kukariri bila kutunga nikiwa darasa la tatu, hapo ndio mwanzo wangu wa kupenda ushairi, kisha baadaye nilijipata kwenye utunzi nikiwa kidato cha pili na baada ya kurudia shule ya upili mimi na wenzangu tunaoshiriki kanisa la GFF Kiimani tukawa na kikundi kiitwacho”WANAMALENGA WA
KIBWEZI”. Washairi maarufu kama Fumau Bin Mjenje wa Tanzania na Nuhu Bakari pia wamechangia sana utunzi wangu.
- Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Kwa kuwa mimi bado mwanafunzi, masuala na shughuli za uanafunzi uniandama kila kucha pamoja na muda binafsi mimi hutenga wa vitu nivipendavyo kama kusoma magazeti haswa Taifa leo na kucheza kambumbu majioni kuifunga siku.
- Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Kuna vitu kadhaa vinavyonipendeza mojawapo ikiwa kujuana na watu wenye mizizi katika sekta hii wakenya na pia watanzania wenye singewajua kama vile Maige shidonge, Tuju, Fumau na Salim Rajab. Pia kule kuchapishwa kwa mashairi yangu katika gazeti la Taifa Leo hunifanya nijikaze kwenye utunzi.
- Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Sekta ya utunzi huitaji muda sana na kwa hali ya kuwa bado napambana na masomo chuoni hupata ugumu mkubwa wa kupata muda zaidi nizame kwenye utunzi asilimia mia.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi yako?Tuambie kuihusu
Naam, kama nisemavyo kuwa kila zimwi lina udhaifu, changamoto zipo kama kukosa kipato cha uchapishaji wa diwani ya mashairi miradi itokeapo na hivyo nakosekana kwenye diwani pia sekta ya utunzi ukumbwa na wizi wa mashairi na hili liliwahi kunipata.Wakati mwingine wasomaji wanaweza pia kuona jambo ulilobuni kwenye ushairi ni tukio halisi liliwahi fanyika kwako na kuleta fikra mpya kukuhusu.
- Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizi?
Cha muhimu zaidi ni kujipa muda na kutafuta mbinu mbadala zitakazonisaidia kwenye uchapishaji, kwenye wizi wa mashairi sijapata la kufanya ila kufuatilia mhusika na kufanya maelewano ya kiutu uzima! Kuhusu wasomi kutoelewa kisa ni halisi au la inabidi nitumie nafsi ya pili au ya tatu.
- Huwa unatangaza kazi zako?Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia
Naam, kazi yangu nazitangaza sana na kupitia hatua hii ninapata ujuzi zaidi haswa ikifikia watunzi waliobombea na wengine hunikosoa na pia kunipa mada za utunzi. Pia wengine kama Fredrick Muthami hunipa motisha sana na kunifanya nijihisi kukubaliwa katika jamii.
- Ni wosia gani utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe?
Maji akiyavulia nguo hayaoge! Na cha msingi ajue hatima yake na atakalo pia. Cha pili ni kuwa kila mtu aliyefika mahali kuna kitu amejinyima na haswa muda huitajika sana, asilaze damu!
- Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utaleta mabadiliko yepi?
Mwanzo zaidi nakifanya kiswahili kiwe lugha ya ulimwengu wote na kitumike kote duniani kisha ushairi niupe sura mpya na kusajilishwa kama sanaa zingine na pia kuwatambua watunzi chipukizi. Kwangu binafsi najibadilisha hadi majina mapya ya Kiswahili na hekima ya juu isiyohitaji kuandika mashairi ili niyakumbuke.
- Kwa yule angependa kuona kazi zako atazipataje?
Kwa yeyote angependa kuona kazi zangu anaweza tembelea kikundi changu cha fesibuku kiitwacho “Kisiwa cha mashairi na Bw. James E. Nzeke” pia kupitia nambari ya simu 0769540092 ama kupitia barua pepe jamesezekiel011@gmail.com.