Samuel Mungai
By: Wanjohi. P. Mugambi

1.Hebu tueleze mengi kukuhusu.
Jina langu ni Samuel Mungai almaarufu Malenga Mhenga katika sekta ya ushairi. Nilizaliwa kijijini Maraigushu eneo bunge la Naivasha, gatuzi la Nakuru mwanzoni mwa karne ya 21 kama kifungua mimba wa Alice Wanjiru Mungai. Nilianza masomo yangu katika shule ya msingi ya Shindano mnamo mwaka wa 2009. Mapenzi kati yangu na ushairi niliyatambua 2013 nilipokuwa darasa la tano. Ilitokea ambapo niliibuka mshindi katika shindano ya kukariri shairi katika kanisa la Full Gospel Church of Kenya (FGCK) pamoja na kundi tulilokariri nalo. Jambo hili lilinipiga msasa na kuanza kukariri mashairi darasani kabla mwalimu wa somo hajaingia. Nilizidi kukariri mashairi katika kanisa la FGCK mpaka nilipotimia darasa la nane mwaka wa 2016. Nilijiunga na shule ya upili ya Mununga mnamo mwaka wa 2017. Walimu walipenda sana kutahini kazi ya ushairi mpaka nikapendezwa nayo. Namshukuru Bw. Njuguna , Bw. Kairu, Bi. Alice Weru, Bw. Mwaura (mwalimu wa kiswahili na pia mwalimu wa darasa) Bi. Stella (mkuu sekta ya uigizaji, nyimbo na ukariri), Bw. Waweru, Bw. Geoffrey Kamau, Bw. Chelule, Bw. Mugo, bila kusahau Bi. Veronicah kwa kunitilia makini hadi nikatimia walipotaka katika maisha yangu ya masomo ya shule ya upili. Nilijiunga na chuo kikuu cha Kiteknolojia cha Murang’a ninapoendelea kufanya shahada yangu ya ualimu katika Kiswahili na Jiografia ambapo nilizidi kukikuza kipaji. Katika semia ya kwanza mwaka wa kwanza, nilijihusisha na uandishi wa neno la muktadha (spoken word) chini ya Muungano wa Kikristo wa Murang’a (MUTCU) lenye mada Sexual Purity. Niliandika pia Fake Friend, My Lovely Mum na Out of Drugs.
katika semia ya pili mwaka wa kwanza ndipo nilianza rasmi uandishi wa mashairi. Nimeandika mashairi mengi sana nikizungumzia masuala ibuka ikiwemo siasa, mapenzi,mikasa nk.Nakumbuka shairi nililomwandikia mhadhiri wangu Dkt. Maithya lenye mada “Mwalimu Nimpendaye” na akanipa senti kadhaa.Mashairi yangu mengi yamechapishwa katika gazeti la Taifa leo.Wahadhiri wangu Dkt. Jane Maithya na Dkt. Miricho (mwandishi) wamenisaidia sana kujikuza.Ninapozungumzia kuhusu ushairi katika darasa, Daktari Maithya hunisifia sana na kunihimiza nizidi kupiga msasa na kupiga hatua. Namvulia kofia mamangu Alice Wanjiru Mungai na ndugu yangu mdogo Francis Chege Wanjiru ambao hunihimiza kila wakati nisife moyo siku moja nitafanikiwa. Pia shangazi yangu Mary Njoki Mbugua na mjomba wangu Moses Ng’ang’a Mungai kwa kunishika mkono na kuwa na mimi wakati wote ninapohitaji kitu.Rafiki yangu Tuju pia alinishawishi sana na kunipa motisha nilipoona shairi lake kwenye gazeti lla Taifa Leo.
- Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Kushinda kwangu katika shindano la mashairi lilinifanya nikaupenda ushairi.Pia, Walimu wangu walinipa mshawasha walipoona nina mapenzi na tasnia ya ushairi, hivyo basi walinipa maswali mengi ya ushairi na kupitia kwa hilo, mapenzi yangu na ushairi yakazidi kunoga. Nilipofika Chuo kikuu ndipo nilijuana na Raphael Mugi(Tuju) chini ya Chama cha Kiswahili Cha Chuo Kikuu Cha Kiteknolojia cha Murang’a (CHAKIMUT) na akanipa urari ule wa kuandika mashairi. Nilipoona shairi lake kwenye gazeti la Taifa Leo, nilipata nguvu tosha iliyoniwezesha kuandika shairi na likachapishwa pia. Pia, nilipendezwa sana na Nuru Bakari katika runinga ya Citizen ambaye hughani mashairi kila Ijumaa, kupitia kwake pia niliupenda ushairi kwa vile nilihisi huo mvuto anapokariri mashari.
- Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Siku yangu kwa mara nyingi huwa njema na tulivu ila wakati mwingine najikaza kiume haswa nikikumbuka wanaonitegemea na pia kama kifungua mimba. Wakati mwingine siku huanza kwa mikosi ila rehema za Mola zaniwezesha kupiga hatua.
- Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Mimi hupendezwa sana ninapoona nimelianza shairi na kulimaliza na baadae shairi hilo kuchapishwa katika gazeti. Pia, kupitia kuandika mashairi, nimapata kipato kutoka kwa watu ambao wameagiza mashairi.
- Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Kwa kawaida hakuna chochote kisichokuwa na ugumu wake.Maisha ya chuo si njia laini, kuna panda shuka mingi ambazo huwa napitia ikiwemo ukosefu wa fedha. Pia, dhihaka kutoka kwa wenzangu ambao huona kama ushairi hautanifaidi popote katika maisha yangu. Wakati mwingine wananikashifu ninapokatiza shughuli zao ili nikaandike mashairi ila najipa moyo siku yangu itafika na nitayalia malipo ya kazi yangu.Rafiki yangu Margaret Wanjiru huniambia kila wakati “ipo siku”.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.
Changamoto ninazopitia ni kama vile kutochukuliwa kama mwandishi kwa vile mimi wananijua na pia kufokewa na watu kwamba ninalolifanya halitanifaidi kwa vyovyote vile.Changamoto nyingine ni pale wengi hutaka tu kuandikiwa shairi bila malipo yoyote.
- Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Mwanzo ni mzazi wangu Alice Wanjiru ambaye hunisaidia kwa njia mbalimbali ninapokuwa na changamoto mfano upungufu wa kifedha. Shangazi na mjomba wangu Mary Njoki na Moses Ng’ang’a mtawalia pia hunipa moyo wakati wengine wananifokea na kwa njia hiyo najipa moyo na kuendelea kupiga hatua. Pia, rafiki yangu Margaret Wanjiru ambaye huwa na mimi wakati wote na ninapokuwa na changamoto hunisaidia kwa namna yoyote ambayo anaweza. Pia, Daktari wangu Maithya hunipa moyo kuwa siku moja itajipa na nitafaidika kutokana na kazi yangu.
- Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia.
huwa natangaza kazi zangu kupitia vikundi vya wasapu na pia katika hali yangu “my status” katika wasapu. Pia, ninapopata fursa ninayaghani mashairi yangu darasani huku chuo Kikuu. Pia, mtandaoni nina ukurasa wangu wa tiktok @Tr. Sam.
Hatua hii imenisaidia kujulikana na pia kueneza kazi zangu.
- Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe.
Yeyote anayetaka kuwa kama mimi na kufika ambapo nimefika naweza kumshauri aanze kwa vile kila safari huanza kwa hatua moja. Pia, kujituma ni jambo muhimu sana kwa chochote unachofanya na cha mwisho penda kazi unayoifanya hata wote wakiwa wanakupinga.
- Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?
Nikiweza pata nafasi ya kubadilisha ulimwengu naweza kukifanya Kiswahili kikajulikane kwote na pia kikaheshimiwa. Kama ni maongezi ya Kiswahili yafanywe kwa njia inayofaa yakizingatia kanuni zote. Pia, ningekitumia Kiswahili kuunganisha jamii zote na kuleta umoja ndani yetu.
- Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?
Yeyote ambaye angetaka kuona kazi yangu ama pia kuzungumza nami anaweza akanifikia kwa nambari yangu ya simu 0798919714 au katika ukurasa wangu wa tiktok @Tr. Sam na pia kwa facebook, Samuel Mungai.
Pamoja tuungane tukipiganie Kiswahili na tukikuze kwa mapana.