MOMANYI HENRY RIOBA
By: Wanjohi. P. Mugambi
Kwa kifupi tuelezee kujihusu

Jina langu ni MOMANYI HENRY RIOBA. Mimi ni mwalimu wa kiswahili na fasihi na mwandishi wa mashairi na Hadithi fupi. Mimi ni mzawa wa gatuzi la Trans Nzoia. Nilisomea shule ya msingi ya Kesogon inayopatikana katika gatuzi la Trans Nzoia, kisha nikajiunga na shule ya upili ya wavulana ya Ortum kule Pokot Magharibi. Baada kumaliza kidato cha nne, nilijiunga na elimu ya sekondari ya juu (‘A’level) kidato cha Tano na Sita katika Shule Upili ya Kiadventista ya Bugema, Kampala Uganda. Nilifaulu vyema mitihani yangu ya kidato cha 6 na kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere kule Uganda. Chuoni Nilisomea kozi ya Ualimu nikijikita katika masomo ya Kiswahili na Jiografia.
Nilihitimu na shahada ya Ualimu mwaka wa 2016. Nimefunza Shule za Upili za Karaus, Meshack Tumkou na Sasa nafunza katika Shule ya Upili ya Noigam, gatuzi la Trans Nzoia.
Ni kipi kilikuchochea na kukufanya ulivyo sasa?
Kwanza ni kipaji cha utunzi. Naamini nina kipaji cha utunzi wa mashairi na kipaji hiki kilichochewa na ari ya kuwa mmoja wa watunzi au Malenga bora. Nilitamani sana kuandika angalau nami nitimize ndoto yangu ya muda mrefu. Kichocheo kingine ni watunzi waliotangulia katika tasnia hii ya uandishi kama vile Shabaan Robert, Ken Walibora, Mwalimu Hassan Mbega, Said A. Mohammed, wallah Bin wallah, Euphrase Kezilahabi na wengine wengi ambao ni kichochea sana kwangu katika tasnia hii ya umalenga na uandishi kwa jumla.
Siku yako ya kawaida huwa vipi?
Baada ya kutekeleza shughuli za siku, huwa napenda angaa kutunga beti hata mbili au tatu za shairi. Nafanya hivi ili nisisahau mada au kile nilichoona na kukiwazia kutunga. Pia huwa napenda kupitia mashairi gazetini nipatapo nakala ya gazeti ya taifa Leo. Na mwisho huwa napitia na kuhariri miswada yangu ya hadithi ninayopania kuchapisha mwakani inshalla.
Ni kipengele kipi unachopenda katika kazi yako?
Napenda fani katika utunzi wa tungo bunifu ninazotunga. Kipengele hiki hukuza na kuifanya kazi iwe ya aina yake kwani huu ndio upekee wa mwandishi katika kazi fulani zake. Hali hii hunifanya kuwa mbunifu zaidi katika kila tungo ili kuzidisha ubora wa kazi na mbinu zilizotumika.
Ni kipi kigumu katika kile unachofanya?
Kigumu sana ni kuyakusanya malighafi ya uandishi na kuyaweka katika kiwango kitakacho kubalika na wengi. Kumbuka uandishi si uandishi tu bali mwandishi anastahili kuandika kazi bora itakayokubalika na wasomaji wake. Unawezakuwa na wazo lakini jinsi ya kuiweka au kuiunda hadi ilete mvuto na mguso wa aina yake ndio balaa wakati mwingine. Hapa ndipo mara nyingi najikuta nikifuma na kufumua utungo au hadithi na kuiweka katika kiwango kubalifu. Si kazi rahisi ila kwa kuwa sisi ni waandishi, inatupasa kufanya hivyo ili kuendana na mahitaji ya hadhira lengwa.
Je,umewahipitia changamoto katika ulifanyalo? Tafadhali tuelezee.
Zipo changamoto tena nyingi. Moja ni tungo kuibiwa hasa tunapopachika kazi zetu mitandaoni. Mtu ataichukua kazi hiyo labda ilimpendeza na kuifanya kuwa yake binafsi. Si ajabu ukute kazi zake zikiwa zimepachikwa jina la mwingine. Pili, Kuna wakati mmoja kazi yangu ya ushairi katika diwani ambalo tulishirikiana na matbaa moja nchini, shairi langu liliandikiwa mwandishi mwingine. Hili halikunifurahisha hata baada ya wahariri kujuzwa. Changamoto nyingine ni hela katika uchapishaji. Uchapishaji ni gharama. Hasa pale matbaa inapokuambia kuwa itahaoisha nakala mia moja. Matbaa haitataka kujua iwapo mfuko wako hauruhusu nakla hizo kuchapishwa. Ingekuwa vyema iwapo matbaa yatasikilizna na waandishi na kukubaliana kuchapisha idadi Fulani ya nakala kulingana na hela alizonazo mwandishi.
Je unajipa shime kivipi ili usonge mbele?
Nilipoingia katika ulingonwa uandishi, nilijua kwamba ndio Sasa safari imeanza. Nilijua Nina mwendo mrefu wa kuandika na kutunga kazi bora Bali si bora kazi. Najipa shime kwa kujiwekea kiwango kila wakati au hata siku. Huwa naandika mashairi angalau siku nne au tano kwenye juma. Hii inanisaidia kuwa mbunifu zaidi na kutambua masuala mtambuko yanayozukankila uchao. Isitoshe, ninan ndoto ya kuchapisha zaidi kabla umri haujakwenda na majukumu kunizonga zaidi. Shime hii hunifanya kujidunga na miradi mbali mbali ya uandishi ninapojumuishwa. Kufikia Sasa nimefanikiwa kuchapisha diwani Tisa za ushairi nilizojumuishwa na Hadithi fupi nane nilizojumuishwa. Binafsi nimechapisha diwani ya hadithi fupi mwaka wa 2023 na naazimia kufyatua nyingine hapo mwakani.
Je huwa tunatangaza kazi zako? Tuambie jinsi ilivyokusaidia.)
Naam huwa natangaza kazi zangu hasa kwenye mtandao wa Facebook kupitia ukurasa wangu wa “Malenga Mtanashati _ Author”. Pia kwenye baruapepe “henrymomanyi083@gmail.com” kwa wale ambao hutakam kutungiwa na kutumiwa mashairi kwa gharama ya kuelewana. Njia hizi zimenisaidia kuuza nakala, kazi zangu kuwafikia wengi hasa kwenye mitandao na pia watunzi wengine hunipata humo na kunihususha kwenye miradi mbali mbali.
Ni wosia gani ungependa kuwapa wanaopania kuwa kama wewe?
Utunzi ni safari. Na kama ilivyo safari, Kuna milima na mabonde. Changamoto hizi ndizo hukupevusha na kukufanya utie bidii zaidi katika ufanyalo. Iwapo una kipaji cha utunzi, kitumie sasa hivi kabla umri kukuenda. Watunzi ni wengi ila cha muhimu ni unachotunga kiwe na mnato wa pekee kwa wale unaowalenga.
Ukipewa fursa, ni athari gani utakayoleta duniani, taifa na kwako binafsi?
Nitabadilisha mtazamo wa watu kuhusu kubaguana katika misingi ya kikabila. Tabia hii imetunyima nafasi na ubora ambao tunastahili kama wanadamu. Pili kujikomboa kutoka kwenye dunia ya “nitafanya” mpaka kwenye dunia ya “ninafanya au ninatenda” Hali hii itatukomboa kutoka kwenye minyororo ya uzembe, kulaza damu na kutamani kufanya ilhali hutekelezi lolote.
Iwapo mtu angependa kufikia kazi zako na kile unachofanya, atakupata kwa njia ipi?
Baadhi ya kazi zangu hupachikwa mitandaoni kama vile Facebook @malenga Mtanashati -Author. Pia barua pepe @henrymomanyi083@gmail.com na mashairi katika gazeti la Taifa Leo.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- After Madrid chaos derby: Mourinho pulls out the printer
- Smart classroom revolution hits Nyeri schools
- Retirement is not a prison sentence: The Uhuru Kenyatta case and the defence of citizenship
- Taufiq Rafat: Voice of Pakistani English Literature
- Nomthandazo Mgcina: A young voice for education, sisterhood and youth empowerment