TAHAKIKI
Anwani: Mosi Na Pili
Mwandishi: Timothy Omusikoyo Sumba
Mhakiki: Alfred Lobawoi
Hiki kitabu kimeandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa gredi ya chini au niseme chekechea. Mtaala wa sasa wa elimu umekumbatia mfumo wa kuandaa hadithi nyingi bunilizi ili kuwaandaa watoto wadogo wawe na umilisi wa lugha; au Kiswahili ama Kiingereza. Kupitia mfumo huu ndipo unapata kwamba wanafunzi wa chekechea tayari wamejua mzo wa mambo na wanakuwa wepesi wa kuyaelewa mambo ambayo wanafundishwa darasani.
Mosi na Pili ni kitabu kilichoandikwa na Timothy Omusikoyo Sumba ambacho kimeshughulikia masuala yanayohitajika na mtaala wa umilisi nchini Kenya. Mwandishi huyu ni nguli wa fasihi ya watoto ambaye ameandika matopa ya vitabu kwa ajili ya kitembo hiki cha chekechea. Hata hivyo, kazi zake nyingi huibua mafunzo belele miongoni mwa wasomaji wake. Mosi na Pili ni kitabu ambacho kinatoa mafunzo kwa wanafunzi kuelewa Siku za Wiki au siku za Juma. Ni wengi mpaka sasa hawana ufahamu ni siku gani hasa hutanguliza siku za Wiki. Wengine hushikilia Jumatatu kwa kuwa wanasema kwamba wiki huanza siku hiyo. Wengine husema ni Jumapili. Wengine wakaishia kusema ni Jumamosi. Ingawa wengine husema kwa kuwa wiki ina siku saba basi inawezekana Jumatatu ikaanzia orodha. Mategu hayo yote yameteguliwa na mwandishi wa kitabu hiki.
Mwandishi ametumia majina ya wahusika kama vile ‘Mosi’ kwa maana ya Jumamosi, Pili kwa maana ya Jumapili na Tatu kwa maana ya Jumatatu. Majina haya ya wanafunzi watatu ambao ni marafiki yatamrahisishia mtoto wa gredi ya chini kusoma na kuwaelewa wahusika kwa wepesi mno. Kitabu chenyewe kinaelezea usuli wa wanafunzi hao kutaka kujua siku za wiki wanapopatana bustanini. Mosi anasema alizaliwa Jumamosi naye Pili anasema alizaliwa Jumapili. Tatu anaongeza alizaliwa Jumatatu. Baada ya wote kujua siku ambayo walizaliwa wanaanza kuangalia kalendani ni nani mkubwa. Mosi anasema yeye ni mkubwa naye Pili na Tatu wanakataa katakata. Pili anawaambia wenzake yeye ndiye mkubwa kwa kuwa Wiki huanza Jumapili. Mosi anakataa na kusema ndiye mkubwa kwa kuwa Wiki huanza Jumamosi.
Mjadala huo wao wa kutambua siku za wiki unakwama baada ya kukosa kuafikiana ni ipi siku ya kwanza ya wiki. Mhusika kwa jina Tatu anaapa kumuuliza mwalimu wao Somi. Siku moja Jumatatu ndipo mwalimu wao alipowafunza siku za wiki baada ya kuwa gizani kwa mda. Mosi, Pili na Tatu walifurahia kuwa watajua siku za Juma. Hapo ndipo walipotanabahi kuwa wiki ina siku saba na siku ya kwanza ya wiki ni Jumamosi.
Ukweli ni kwamba kazi hii imefanikiwa kugusia masuala ibuka katika mtaala wa umilisi na kulete mwanga ambao haukuwepo awali. Aidha, hii ni tunu kwa wanafunzi wa kitembo cha Chekechea kutagusana na misamiati faafu na ile ambayo ni nyepesi mno kwao kuelewa. Isitoshe, lugha ya hadithi hii ni sahili na ya kuvutia mno. Yeyote yule akisoma anavutiwa ajabu na jinsi ambavyo mwandishi alivyosuka maandishi yake.
Kwa mintarafu hiyo pia picha ambayo imetumika kwenye kitabu hiki ni picha nzuri nzuri yenye mvuto wa aina yake. Kabla mwanafunzi atagusane na maandishi picha itamwelekeza zaidi ya kile ambacho kimeandikwa. Hatua hii itamsaidia sana mwanafunzi wa chekechea kuelewa hadithi zaidi na hata kumjengea taswira akilini. Halikadhalika, maudhui kama vile dini, Usawa wa kijinsia na Elimu yameshughulikiwa vyema kwenye hadithi hii kiustadi. Vyote hivyo vimemsaidia mwandishi mwenyewe kusuka kazi hii na kuibuka na hadithi nzuri na ya kuvutia.
Kimsingi niseme kwamba hii ni mojawapo ya kazi ambayo ni ya kipekee mno. Inavutia kuanzia jaladani, maandishini na hata mahali ambapo picha zimetumika. Itamkuza vyema mtoto wa chekechea na kuwa nguzo katika umilisi wake wa lugha ashirafu ya Kiswahili. Mwishoni mwa kazi hii pia kuna Sherehe mahali ambapo kuna misamiati iliyotumika na maana yake. Hapa msomaji atajifunza misamiati aliyotumia mwandishi pamoja pia na maswali mepesi ya kumchangamsha. Ikumbukwe kuwa mtu huanza mahali.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Spain are world champions again as Torres shatters Messi’s farewell dream
- When the songs fade, the wounds remain: The human cost of Ol Kalou’s by-election
- From Sleepless Nights to New Beginnings: How Community Kindness Restores Hope and Dignity to Widows
- A voice of compassion, service, and hope
- New York’s mayor mulls Netanyahu arrest as UN summit looms — and the world holds its breath