Judy Njeri
By Alfred Lobawoi
Worth Noting
“Kile kilichonifanya kuwa mtu niliye leo ni hamu yangu ya kubadilisha mtazamo kwamba ni wanaume pekee wanaoweza kufanikiwa katika uzalishaji wa filamu. Natamani kuwahamasisha watu; hasa wasichana—waamini katika uwezo wao na kujithamini.
Nia na bidii hunisukuma kuendelea hata wakati mambo ni magumu. Pia, kushirikiana kama kundi moja na wenzangu kunaleta nguvu mpya—tunasaidiana, tunahamasishana, na tunashirikiana kwa lengo moja.
Kukabiliana na watu hawa wanaojivuta au waliokata tamaa ni changamoto, hasa unapojaribu kujenga jina na kutafuta nafasi ya kazi kutambulika.”
- Kwa kifupi utueleze wewe ni nani?
Njeri Ngotho ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo cha Kiufundi cha NIBS, akisomea kozi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano. Ni mwandishi mahiri wa hadithi, anayezibadilisha kuwa filamu na maigizo ya jukwaani. Kama mwandishi wa miswada na mkurugenzi wa filamu, anachukua jukumu muhimu katika kikundi cha ubunifu cha TRY ANGLE PRODUCTION, ambacho hivi karibuni kilizalisha filamu Kwa Jina la Njaa inayopatikana kwenye mtandao wa YouTube.
Zaidi ya kujihusisha na filamu, Njeri pia ni mtayarishaji na mtangazaji wa redio mwenye ujuzi. Katika runinga, anahudumu kama mtayarishaji na mwendeshaji wa kipindi cha The Golden Transition, ambacho pia anakisimamia kama mkurugenzi. Uzoefu wake mpana katika majukwaa tofauti ya vyombo vya habari unaonyesha kipaji chake, ubunifu na dhamira yake ya kusimulia hadithi zenye athari.
- Ni kitu kipi kilikuchochea uwe jinsi ulivyo?

Kile kilichonifanya kuwa mtu niliye leo ni hamu yangu ya kubadilisha mtazamo kwamba ni wanaume pekee wanaoweza kufanikiwa katika uzalishaji wa filamu. Natamani kuwahamasisha watu; hasa wasichana—waamini katika uwezo wao na kujithamini.
Pia, nafanya kazi kwa bidii kila siku kuhakikisha maisha yangu ya baadaye yatakuwa bora, niishi maisha ninayoyaota na kuwahimiza wanawake wengine wafanye kazi kwa bidii na kufuatilia malengo yao bila woga.
- Wewe hupanga vipi siku yako kunapokucha?
Kwa kawaida mimi huamka saa 4:00 Alfajiri kwa ajili ya kutafakari (meditation) kisha baada ya halo ninapata kifungua kinywa kabla ya kuzungumza na waigizaji pamoja na timu ya uzalishaji wa filamu. Mazungumzo yakikamilika Mimi huhakikisha nimetuma mswada ambao upo tayari ndipo nijiandae rasmi kupambana na siku na kuingia darasani.
Isitoshe, mafunzo ya darasani yakikamilika Mimi pamoja na kikosi changu huanza kurekodi kipindi bila mapumziko ya chakula cha mchana. Kugawana kazi na kuchambua sehemu za filamu pamoja na Guandaru wa Ngure na Mbugua wa Chege ambao ni waasisi wenza wa Try Angle Production hufuatia.
Kwa upande mwingine siku yangu hukamilika kwa kutazama filamu za Kenya na kupumzika kabla ya kufunga siku rasmi kwa dua saa 5:00 ndipo nilale.
- Ni kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Kile kinachonifanya nipende kile ninachofanya ni nafasi ya kuingiliana na watu mbalimbali na kujifunza kutoka kwao. Kupitia kazi yangu, ninapata fursa ya kukuza vipaji na kusaidia wengine kugundua uwezo wao, hasa vijana. Ninapenda kusimulia hadithi za kweli ambazo zinaigusa jamii kupitia filamu na sinema, kama vile Kwa Jina la Njaa. Kupitia uandishi na utayarishaji wa maudhui, ninaweza kuelimisha, kutoa taarifa na kuburudisha watu kwa njia yenye maana. Furaha yangu huongezeka ninapoona watu wakikubali na kupenda kazi tunayofanya kama Try Angle Production. Zaidi ya yote, napenda kuona mawazo yangu yakigeuka kuwa picha halisi ambazo watu wanaweza kuangalia na kuzihusisha na maisha yao.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi zako? Tueleze.
Changamoto kubwa ninayokumbana nayo ni kusawazisha kati ya masomo na kazi ya upigaji filamu. Wakati wa masomo una ratiba maalum, lakini upande wa utayarishaji wa filamu hauna muda rasmi—unahitaji muda mwingi na mara nyingi kurekodi huendelea hadi usiku au siku zisizopangwa. Hii huleta ugumu katika kupanga muda wa kutosha kwa kila jukumu.
Pia, wakati wa kufanya masoko ya kazi zetu, hukutana na watu wasiotaka kushirikiana au wasioamini kazi unayowasilisha. Kukabiliana na watu hawa wanaojivuta au waliokata tamaa ni changamoto, hasa unapojaribu kujenga jina na kutafuta nafasi ya kazi kutambulika. Inahitaji uvumilivu, ustahimilivu na ujasiri mkubwa ili kuendelea kusonga mbele licha ya vizingiti hivi.
- Ni nini kinachokusaidia kuepuka changamoto hizi?
Kile kinachonisaidia kushinda changamoto ni azimio langu la dhati la kufanikisha ndoto zangu. Nia na bidii hunisukuma kuendelea hata wakati mambo ni magumu. Pia, kushirikiana kama kundi moja na wenzangu kunaleta nguvu mpya—tunasaidiana, tunahamasishana, na tunashirikiana kwa lengo moja. Kuwa na hadhira inayotutia moyo pia hunipa msukumo mkubwa; kuona watu wakithamini na kupenda kazi yetu huniweka hai kiakili na kihisia. Zaidi ya yote, kukumbuka malengo yangu ya maisha hunikumbusha kwa nini nilianza safari hii, na hunifanya nisikate tamaa hata mbele ya changamoto kubwa.
- Ni ushauri upi ambao ungependa kumpa yule anayetaka kuwa kama wewe?
Kwa mtu yeyote anayetaka kufanana nami, kuna mambo muhimu ya kuzingatia: Kwanza, kuwa na azimio la dhati na usikate tamaa kirahisi. Pili, zingatia malengo yako kwa umakini na usiruhusu mambo ya pembeni kuyakurupusha. Pia, tafuta watu ambao wataweza kukusaidia na kukuunga mkono katika safari yako—kama marafiki, familia, au viongozi wa kitalii. Mwisho, kumbuka kwamba mafanikio hayaendi kwa haraka; lazima uwe na uvumilivu na uthabiti hadi utakapofikia kile unachotamani.
- Ukipewa nafasi ulete mabadiliko ulimwenguni na kwako pia utafanyaje?
Kama ningepata nafasi ya kubadilisha jambo lolote, ningehakikisha tunapata vifaa vyote ambavyo sisi kama Try Angle Production tunavitamani, kwani kwa sasa tunakosa vifaa hivyo na inakuwa vigumu kufanya kazi kwa ufanisi. Pia, ningependekeza kila nchi iwe na Katibu wa Wizara wa Filamu (Film Cabinet Secretary) anayesimamia sekta hii kwa umakini zaidi.
Ningependa kuona kila mtu akipenda filamu na kuielewa umuhimu yake kama sanaa na biashara. Vivyo hivyo, kama kuna fedha za ujenzi wa barabara na ukarabati wa ofisi za serikali, ningependa pia kuwe na mfuko maalum wa kusaidia filamu, ili kuwekeza na kukuza sekta hii muhimu kwa maendeleo ya kitaifa na kukuza vipaji vya vijana.
- Anayetaka kuona kazi zako atazipataje?
Kupata kazi zangu, unaweza kutembelea Try Angle Production kwenye mitandao ya kijamii. Tunatengeneza mfululizo wa filamu fupi na sinema ambazo zinapatikana kwenye kituo chetu cha YouTube. Try Angle Production ilianzishwa na sisi watatu: Guandaru wa Ngure, Mbugua wa Chege, na mimi mwenyewe, Njeri wa Ngotho. Tumetoa kazi mbalimbali kwenye kituo chetu cha YouTube, ikiwa ni pamoja na mfululizo unaoendelea Kwa Jina la Njaa.
Pia, unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii:
Facebook: Njeri WA Ngotho
TikTok: njeri WA ngotho
YouTube: Njeri WA Ngotho
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER August 13, 2026
- The deputy’s dilemma: Gachagua warns Kindiki he is next
- KEMSA chief outlines supply chain reforms ahead of health summit
- Why Audi’s smaller models are often more desirable than their bigger brothers
- The politics of tomorrow: Why Kenya keeps replacing the future with the next election