Alfred Lobawoi
Nikitunga tungo moja, lenye vina na mizani,
Nikazitimiza haja, kugusa waja moyoni,
Hufinyanga yangu hoja, juu lama huko chini,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Hutunga nyingi bahari, nikiwa nayo malengo,
Ukitazama urari, wa vina kila ukingo,
Utaingiwa na ari, uimbe kama mtungo,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Napenda nitunge sana, tungo mia na zaidi,
Katu nisipige kona, lengo langu kukaidi,
Hata kama sitavuna, kutunga nitashitadi,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Nikilala kitandani, mawazo huniandama,
Ikanisuta kwa nini, kuandika ninakoma,
Hapo huketi kitini, utunzini kujitoma,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Usione najidai, hiyo si laiki yangu,
Ukisikia madai, hayo ni ya walimwengu,
Abadi ukiwa hai, utayaona mizungu,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Ingekuwa heko nyingi, nizipatazo kwa watu,
Ije inipake rangi, nivutie kila kitu,
Singefanya mambo mengi, kwa kuona mimi jitu,
Mashairi nayaenzi, ukomo wa kuyaenzi.
Na kama unayaenzi, onyesha wazi wazi,
Hata mwana wa mhunzi, huvuvia kwa mzazi,
Jimudu kwayo utunzi, tuelekeze vizazi,
Mashairi nayaenzi, mimi hapa Lobawoi
Mtunzi: Alfred Lobawoi
Mahali: Ruiru.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Ruto tells UN: Africa’s crisis is rigged rules, not empty coffers
- Njogu’s diaspora agenda gains fresh impetus as Kenya launches investment platform
- Eldoret to host 2026 UN Tourism Week: Can the North Rift redefine Kenya’s tourism story?
- After Madrid chaos derby: Mourinho pulls out the printer
- Smart classroom revolution hits Nyeri schools