Benson Bayah
By: Wanjohi. P. Mugambi
Hebu tueleze mengi kukuhusu.
Ugumu wa kitu chochote usiwe chanzo cha kuzima ndoto zako. Huu ndio wosia wangu.
Jina langu ni Benson Bayah. Wengi wananitambua kwa jina la kazi ambalo ni Kaka Benayah. Nilizaliwa katika kijiji cha Sita kilichoko katika kaunti ndogo ya Malindi, Kaunti ya Kilifi. Masomo yangu ya chekechea na msingi niliyapokea katika shule mbalimbali. Nilianza kisomo cha chekechea katika shule ya St Francis iliyoko mji mdogo wa Gede, mji uliokaribiana kitalifa na Gedi Ruins. Nilipotinga darasa la kwanza , nilihamia shule ya msingi ya Chafisi Baptist iliyoko katika mji wa Watamu. Hapa nilisoma madarasa machache tu. Darasa la tatu likanipata katika shule ya msingi ya Gede.
Katika shule ya msingi ya Gede, nilifanikiwa kusoma hadi darasa la tano. Safari yangu ya kutafuta elimu ilikojificha ikanipeleka tena Watamu. Muda huu ilikuwa katika shule ya msingi ya St Dominic. Baada ya miaka kadhaa ya kuwa kama mhamiaji, nilifanikiwa kutulia katika shuke hii na nikafanikiwa kumalzia kisomo changu cha msingi mnamo mwaka wa 2015. Baada ya kutia fora katika mtihani wangu, nilibahatika kupata nafasi katika shule ya upili ya Wavulana ya Mukaa katika kaunti ya Makueni.
Shule ya wavulana ya Mukaa ilinipata nikiwa ndio kwanza naanza kuchangamkia talanta yangu, talanta ya kutunga na kughani mashairi. Naam, naweza kusema kwamba hapa ilikuwa ndio kwanza mkoko ulikuwa unaalika maua. Ni katika shule hii ndipo nilihsi uzao mpya. Ni papa hapa ndipo nilipojitambua na kujifahamu barabara na mshawasha wa mengi mazuri niliyoyatenda ukang’oa nanga. Nikiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, niliweza kutunga mashairi ya arudhi na kuyaghana wakati wa gwaride . Wanafunzi pamwe na walimu walistaajabu uwezo wangu. Hata hivyo, jambo hili kwangu halikuwa geni. Awali nikiwa mwanafunzi wa darasa la tano, katika shule ya msingi ya Gede, nilitunga shairi langu ka kwanza kabisa kwa mada, “Gede Sasa Yasifika.’’ Naweza kusema Shule ya Mukaa ilikuwa tu uwanja wa mimi kutamba na kutaratamba na kuonyesha uwezo niliokuwa nao. Nilijiamini na kuimarika zaidi, aghalabu baada ya kupewa nafasi chungu nzima za kughani mashairi ya mada mbalimbali. Mnamo mwaka wa 2017 nikiwa katika kidato cha pili, shairi langu , “Mukaa Ni Sukari’’liilichapishwa katika gazeti la Mukaa Times.
Kuchapishwa kwa shairi langu katika gazeti hilo kulinichochea zaidi. Nikaanza kusonga hatua baada ya nyingine. Niliongeza mapenzi zaidi katika lugha ya Kiswahili. Hatimaye nilianza kuandika makala mafupi mafupi na hadithi fupi mbalimbali. Niliikumbatia fasihi kwa mikono miwili. Matokeo yake yakawa kuzaliwa kwa chama cha Kiswahili cha Mukaa( CHAKIMU). Nikiwa mwenyekiti nilisaidiana na mlezi wa chama ambaye ni Bw. Deon Musau Muia kumleta hayati Profesa Ken Walibora katika kongamano kubwa shuleni mwetu. Baada ya kongamano hilo, nilifahamu fika taaluma niliyohitaji kusomea punde baada ya kumaliza kisomo cha shule ya upili. Uanahabari. Naam, mapenzi yangu ya lugha yalikuwa yanaegemea sana taaluma hiyo. Nikaamua kuivulia nguo na kuigolea bahari ya uanahabari.
Baada ya kumaliza shule ya upili, nilijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea taaluma pendwa, Uanahabari na utangazaji. Nikiwa chuoni Nairobi, nilipata nafasi ya kutagusana na watangazaji wenye tajriba kubwa wakiwemo Hassan Ali, Ann Njogu bila kumsahau mwandishi tajika Wallah Bin Wallah. Nikiwa mwaka wa kwanza, nilifanikiwa kuchapisha mashairi yangu katika diwani ya mashairi ya “ Malenga wa Kenya’’. Hii ilikuwa diwani shirikishwa iliyojumuisha watunzi wengine wakiwemo Kaka Fred na ndugu Alfred Lobawoi. Nichukue nafasi hii kumshukuru zaidi huyu ndungu mstaarabu Alfred Lobawoi. Nimeshirikiana na ndugu huyu mweledi wa lugha kutenda mengi. Huyu ni roho safi na mapenzi yake ya lugha ni ya kupigiwa mfano.
Hadi sasa hivi nimeweza kuchapisha hadithi zangu kadhaa katika Antholojia mbalimbali. Hadithi hizo ni kama Utamaushi katika Harufu ya Jehanamu na Hadithi nyingine, Sabasaba ya Kumbukumbu katika Simu Una nini na hadithi nyingine pamoja na hadithi nyingine ambazo bado sijazichapisha. Vile vile, nimeandika diwani yangu ya mashairi ambayo napania kuichapisha mwakani majaliwa.
Pia ,ninao wavuti ambao huutumia katika taaluma yangu ya uandishi wa habari. Hapa kunavyo vitengo kadha wa kadha kama vile kandanda, siasa, biashara, maisha na elimu. Mimi huandika makala na habari kuhusu vitengo hivi. Natazamia kufungua kampuni ya habari nitakayoiita : “ Benayah Times ‘’. Kwa sasa hivi, natafuta waandishi wenza wa habari tutakaoshirikiana kuandika habari na kuandika makala mbalimbali. Kiungo cha tovuti hiyo ni: www.benayahtimes.com .
Uandishi ni bahari. Kwa bidii na mapenzi makubwa ya kazi yangu, ninayo imani kuwa nitaendelea kukua na kuitendea haki taaluma hii.
Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Mapenzi yangu ya fasihi yalichochea pakubwa katika tasnia yangu. Mkufunzi wangu Bw. Deon Muia ambaye pia ni mwandishi alinisaidia pakubwa kukua nilipokuwa katika shule ya upili ya Mukaa. Nilipojiunga na chuo, watunzi wenza na waandishi kadhaa wa kazi bunilizi pia walihusika sana katika makuzi yangu. Naomba kuwajivunia na kuwataja baadhi yao: Alfred Lobawoi, Timothy Sumba, Brian Oigara, Kaka Fred, Salim Kipkoech, Miriam Biketi, Boaz Aseli pamoja na Dokta Ziro. Nitazidi kuwavulia kofia kwa michango yao ima kwa mawazo ama kwa kushirikiana nao moja kwa moja. Vil vile, matembezi yangu katika kituo cha Kiswahili cha Wasta kinachomilikiwa na Wallah Bin Wallah yalinipa mshawasha zaidi wa kuipambania tasnia yangu barabara.
Uwewahi kupata changamoto katika kazi yako?
Naam, changamoto zipo. Nigusie kidogo taaluma ya utunzi wa mashairi. Changamoto kubwa zaidi ni uchache wa wapenzi wa mashairi. Waja wengi siku hizi wana mapenzi finyu katika ulingo huu ikilinganishwa na fani nyingine za kifasihi. Tuchukulie mfano hai kwamba unauza bidhaa zisizokuwa na wateja. Unaweza kukisia na kukadiria hasara yazo. Nimeshuhudia changamoto ya waandishi wachanga kutopewa nafasi ama kipaumbele. Vyombo vikuu vya habari na kampuni za uchapishaji zinasaka wanahabari na waandishi wenye majina mtawalia. Ni yale yale ya matangazo ya nafasi za kazi, kwamba wanataka mtu mwenye tajriba ya miaka kadhaa. Kama ndio kwanza unaona mwanga katika tasnia yako, unaweza kula mwande kipindi kirefu hadi utakapookoka.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Spain are world champions again as Torres shatters Messi’s farewell dream
- When the songs fade, the wounds remain: The human cost of Ol Kalou’s by-election
- From Sleepless Nights to New Beginnings: How Community Kindness Restores Hope and Dignity to Widows
- A voice of compassion, service, and hope
- New York’s mayor mulls Netanyahu arrest as UN summit looms — and the world holds its breath