Former BBC, Journalist Charles Hillary
By Alfred Lobawoi
Worth Noting
“Awali nilipenda kumsikiliza sana bw. Charles Hillary hasa wakati ambapo nilipata video yake akitangaza taarifa ya habari. Ulumbi wake kwa lugha ya Kiswahili uliniteka bakunja. Kando na bw. Charles Hillary Nkwanga kuwa mtangazaji hodari wa taarifa pia alikuwa mweledi katika utangazaji wa kabumbu. Umilisi huu wa kuwa na vipaji viwili na vyenyewe kumkaa pia kuliwavutia wengi na kuwapendeza. Hilo ni jambo jingine ambalo atakumbukiwa kwayo.”
Naandika makala haya nikiwa na masikitio makubwa sana kuhusu kifo cha gwiji Charles Hillary Nkwanga ambaye alitangulia mbele za haki mnamo Jumapili 11 katika Hospitali ya Mloganzila alikokuwa akipokea matibabu.
Habari hizi nilizipokea kwa uzito sana nilipokuwa katika harakati za kutafuta taarifa za hapa na pale kama kawaida ya uanahabari. Japo nilichukua mda kuelewa kama kweli ni Charles mmoja nimjuaye au ni mwingine. Baadaye nilielewa fika ni ukweli. Kuro haisemi uongo kumbe. Habari hizi hazikuwa kwenye mitandao ya kijamii pekee bali pia kwenye ukurasa wa wakereketwa wengi wa Kiswahili. Ukweli ni kuwa chema hakidumu.
Awali nilipenda kumsikiliza sana bw. Charles Hillary hasa wakati ambapo nilipata video yake akitangaza taarifa ya habari. Ulumbi wake kwa lugha ya Kiswahili uliniteka bakunja. Si hayo tu, yeye ni miongoni mwa wanahabari ambao utapenda mno kuwasikiliza mara kwa mara kutokana na mtiririko wao aula katika utangazaji na muwala ambao ni wa kuvutia. Isitoshe, licha ya yeye kuwa mwanahabari kutoka taifa la Zanzibar, kinachovutia na kutia moyo ni jinsi ambavyo watu kutoka mataifa ya nje wanavyomfahamu Hillary kwa ujuzi wake na tajiriba pana katika ulingo wa utangazaji. Tangu enzi zile akiwa katika mashirika kama vile shirika la Utangazaji BBC, Radio One na DW ambapo alitengeneza msingi mzuri katika tasnia ya uanahabari na kuacha alama ambayo itadumu daima dawamu.
Hillary ambaye amefariki akiwa bado ni Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano kwenye ikulu ya Zanzibar na Msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakumbukwa pakubwa na waandishi wa habari waliotangamana naye kama mtu mnyenyekevu, mcheshi, muungwana na mwenye kipaji cha kipekee. Mti mkuu ukigwa wana wa nyuni huyumba eti.
Vyombo vya habari vya Zanzibar, Tanzania na hata mataifa mengine kwa kweli kimempoteza mhimili muhimu katika ulingo wa uanahabari. Sauti yake na ucheshi wake ulivyotaanisi kwenye masikio na macho ya watazamaji na wasikilizaji, itasalia kuwa kumbukumbu nzuri sana katika taifa la Zanzibar. Si hayo tu, pia wengi ambao walipata nafasi ya kushikwa mkono naye wanamzungumzia kama mtu ambaye alipenda kuvikuza vipaji changa hasa katika ulingo wa utangazaji jambo ambalo limewafanya wengi kuinukia na kuwa mfano bora.
Kando na bw. Charles Hillary Nkwanga kuwa mtangazaji hodari wa taarifa pia alikuwa mweledi katika utangazaji wa kabumbu. Umilisi huu wa kuwa na vipaji viwili na vyenyewe kumkaa pia kuliwavutia wengi na kuwapendeza. Hilo ni jambo jingine ambalo atakumbukiwa kwayo. Katika safu hiyo hiyo kifo chake pia kinafufua kumbukumbu ya mwendazake Leonard Mambo Mbotela ambaye alitangulia mbele za haki mwaka huu, naye alikuwa mtangazaji mzuri wa taarifa pamoja na kabumbu.
Waandishi na watangazaji katika taifa hili letu pia watamkumbuka Charles Hillary alipoalikwa kwenye kongamano la Kiswahili WASTA kama mgeni mashuhuri na hata kutuzwa kutokana na mchango wake adhimu wa kukikuza Kiswahili.
Pamoja na hayo nilipata nafasi adhimu mno kama njia mojawapo ya kukusanya maoni ya kuandaa makala haya kuhusu kumbukumbu ya wakereketwa wamjuao Charles Hillary ambao walizungumza yaliyowakaa moyoni; “Mimi ninamkumbuka nguli, Charles Hillary Nkwanga kama mlumbi hodari na aliyekitetea Kiswahili Sanifu. Kimefiwa Kiswahili. Kiswahili Kimefiwa.” akasema bw. Bitugi Matundura ambaye ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo kikuu cha Chuka.
Ingawa ndiyo njia yetu sote kwenda hatuna la kuamba ila kumtakia mwendazake Charles Hillary alazwe penye wema peponi na Mwenyezi Mungu amuepushe na adhabu ya kaburi Inshallah. Makiwa sana kwa ndugu jamaa na marafiki wa mwendazake pamoja na Tasnia ya Uanahabari pamoja na Kiswahili kwa jumla.