Wanjohi. P. Mugambi
Machozi kwangu ni tele, nikiiwaza tanzia
Na za simanzi kelele, kote ninazisikia
Imeingia chelele, nafsi imemrudia
Amelala Kisavuli, guru wa wanahabari
Aliianza kikale, miaka ya themanini
Akapaa polepole,ย kufikia kileleni
Leo ame’nda milele, sitamani kuamini
Amelala Kisavuli, guru wa wanahabari
Alishamiri kongole, kotekote duniani
Walomsikia kule, walituzuru nchini
Wamwona wa kike mwale, anotamba runingani
Amelala Kisavuli, guru wa Wanahabari
Imetupokonya ndwele, hii nduli saratani
Nasi machozi ni tele, Kisavuli hatwamini
Mbona twalia uwele, mbona atufie yani?
Amelala Kisavuli,ย Guru wa wanahabari
Tutaupeza upole, kwake ulioshamiri
Na upendo mteule, moyoni aliyokiri
Na mazuri yake yale, uliyotenda kwa heri
Amelala Kisavuli,ย guru wa wanahabari
Kaditamati tungole, kwangu naimalizia
Nilie mato yaole, kwa Jalali metulia
Kwani ilokuwa ndwele, kwangu ndo hiyo sawia
Amelala Kisavuli, guru wa wanahabari
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni