Mwalimu Duncan Mulu
- Hebu tueleze mengi kukuhusu.

Ninaitwa Mwalimu Duncan Mulu. Mimi ni mwalimu wa Kiswahili na somo la dini. Aidha, ni mtunzi wa mashairi na hadithi za Kiswahili. Nimezaliwa kaunti ya Kwale, Pwani ya Kenya. Nilisomea shule ya Msingi ya Mahuruni, iliyopo Kaunti ndogo ya Lungalunga, Kwale. Nilifaulu vyema mtihani wa KCPE, na kujiunga na shule ya upili ya kitaifa ya Nairobi School, ambako, moto wa ndoto yangu ulitiwa mafuta, ukaongezeka si haba. Baada ya hapo, nilifaulu kujiunga na chuo kikuu cha Pwani, nilikosomea ualimu.
Awali, nilipenda sana kusomea unahabari, japokuwa taaluma zote mbili nilizipenda sana. Nilipenda niwe mtangazaji gwiji wa Kiswahili, si msomaji habari, si mhariri, si mtangazaji wa vipindi vya injili, Taarab na Kiswahili. Hata hivyo, Kiswahili kilinifanya nipende ualimu. Kilinipa njia mbadala, nikataka niwe Mwalimu wa lugha, njia ambayo naamini ipo siku itanifikisha kuwa Profesa wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili. Mungu alipofungua mlango huu, sikuwa na budi kuuchangamkia. Nafurahia sana kuwatunza na kuwafunza wanafunzi.
Katika himaya ya uandishi, nimeandika hadithi fupi kama vile Moto Wa Ndoto, katika mkusanyiko wa hadithi fupi wa Simu Ya Ajabu na hadithi nyingine, na Povu La Uovu katika diwani ya Nahofia Kesho yangu. Aidha, nimechapisha mashairi katika Wasifu wa Omosikoyo Sumba, na Sauti za Washairi.
- Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Kilichonichochea kuipenda tasnia hii ya Kiswahili ni karama tu kutoka kwa Mungu. Katika makuzi yangu, nilijipata tu nikipenda vipindi vya redio za Kiswahili, mziki, michezo ya kuigiza, fasihi na masomo ya Kiswahili. Chochote kinachokihusu Kiswahili, hunisisimua na kuniteka bakunja.
- Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Ninapoamka tu, cha kwanza dua. Kisha, bongo langu hupata muda wa kufikiri beti mbalimbali za Kiswahili, na nafasi niliyo nayo katika kupiga makasia katika bahari hii kubwa ya Kiswahili.
- Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Mimi hupendezwa sana na namna Kiswahili hunisaidia kupitisha maadili kwa wanafunzi wangu na hata wasomaji wa kazi zangu. Vilevile, Kiswahili kimenipa marafiki si haba. Kwa ajili ya tasnia hii, najipatia kipato vilevile.
- Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Kwa hakika, namshukuru Mungu sana kwani amenifanyia wepesi. Sioni ugumu wowote katika tasnia hii. Sing’ang’ani sana. Mungu amenipa uwezo unaonisaidia kupambana na kila kazi. Inshaallah, nitapiga hatua nyingi zaidi.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.
Naam! Changamoto hazikosi popote penye riziki. Kama waandishi chipukizi wengine wengi, changamoto kubwa ni kupata soko la kazi zetu. Aidha, mchakato mzima wa kupata matbaa za uchapishaji kwa uwezo wetu mdogo wa kiuchumi huwa changamoto kubwa.
- Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Hupata mshawasha mkubwa kutoka kwa wanaoelewa uwezo wangu kuwa nisichoke kupambana ili nipige hatua. Hili, hunipa moyo na kunisaidia kupiga hatua.
- Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia.
Naam. Huitumia sana mitandao ya kijamii kutangaza kazi zangu. Hii husaidia sana kuwafikia rafiki zangu, hasa wale niliosoma nao.
- Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe.
Kwa yeyote mwenye hazma na hamu ya kutaka kuwa Mtaalamu wa Kiswahili, kwa kupitia ualimu, utangazaji, uandishi ama kwa njia nyingine yoyote ile, anafaa mchapakazi, mnyenyekevu na mwenye kufuata ushauri. Ajitume kielimu apande vidato vya kiakademia kwa ujasiri, huku akishabikia kuzisoma kazi za Kiswahili pamwe na kusikiliza vipindi vya lugha ili kujinoa makali.
- Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?
Ningeipata fursa hii, ningehakikisha Kiswahili kinakuwa somo la lazima katika viwango vyote vya kiakademia. Aidha, ningelibuni baraza la Kiswahili nchini Kenya, ili kuendeleza lugha hii kwa kuwaleta wadau wote wa Kiswahili; wasomi na wapenzi wote wa lugha hii.
- Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?
Kwa kutembelea mtandao wangu wa Facebook, *Dunco Dunco* utapata mashairi yangu niliyoyaangika humo. Halikadhalika, YouTube, utanipata kwa chaneli yangu ya Duncan Mulu. Kwa vitabu nilivyochapisha, wasiliana na Matbaa ya Best Editors Publishers ama unitumie ujumbe kwa mtandao wangu wa Facebook nikuelekeze namna ya Kuvipata.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Reprieve for over 200 MKU students as Court quashes CS order to stop Oral Health degrees
- Kamuri calls for unity, safety amid market fire, school tragedy and Ebola facility debate
- Hundreds benefit from free specialized medical services at Othaya health camp
- Mudavadi in Seoul ahead of the South Korea, African Foreign Ministers Summit
- Madaraka day message from Supreme Global President of Peace and Universal Leader