Alfred Lobawoi
Alfred Lobawoi ni mshairi ambaye amechangia diwani mbalimbali ya mashairi ikiwemo, Dagaa na Mashairi mengine, Utando wa Ushairi, Tasnia ya Ushairi, Wosia na Mashairi Mengine, Lulu za Ushairi, Malenga wa Kenya, Malenga Wa Afrika miongoni mwa kazi zingine za ushairi. Pia amechangia sana katika uandishi wa Hadithi fupi za Kiswahili kwa wanafunzi wa shule ya msingi na shule ya upili kupitia kwa kazi kama vile Gilasi iliyovunjika na Hadithi Nyingine, Mtoto wa Dhahabu na Hadithi Nyingine na Njia ya Mwongo na Hadithi Nyingine.
Kwa sasa ni mwanahabari ambaye amejikita sana kwenye masuala ya Elimu kwa kuviendesha vipindi vya Kiswahili na kuandika makala ya Kiswahili kwenye magazeti. Isitoshe, huchangia kuandika tahakiki kwenye gazeti la Mt. Kenya Times na kuwakuza waandishi chipukizi.
Ari na ilhamu yake ni kujenga mustakabali mwema ambao utakuwa wa manufaa makubwa katika ulimwengu wa sasa na hata kuvichochea vizazi hadi vizazi, kushaliki ima fa ima kukuza na kuitetea lugha ashirafu ya Kiswahili.
Huu Mwaka
Yarabi uniwezeshe, hili dua ninatia,
Pa mawi uniepushe, nisije nikajutia,
Mola unineemeshe, waja wakitoa tia,
Huu mwaka ninasema, si wa kujaribu kwangu.
Wallahi ninayo nia, lazima niitimize,
Hata nisipofikia, pambanoni nijitoze,
Hatua siyo hatia, kawaida nijikaze,
Huu mwaka ninasema, ni kusema na kutenda.
Si vyema nijipumbaze, nikamvizie kobe,
Ni sawa nijiulize, mbona mchezo wa kibe,
Heri nikambamize, akawa zao la shibe,
Huu mwaka ninasema, hakuna kumvizia.
Naapa hii si debe, kama ya uongozini,
Ya kuonyesha ubabe, nikatambe siasani,
Wala si kufanya gube, hata ajua Manani,
Huu mwaka ninasema, kushindwa si mambo yangu.
Ala zipo mikononi, timazi pia utepe,
Nizidishe umakini, nikwepe kuwa mapepe,
Jambo zuri natamani, mwishowe likanilipe,
Huu mwaka ninasema, uwe wenye heri tele.
Hata mgongo wanipe, wasena wangu wa kweli,
Waseme nipe nikupe, kwangu igeuke kali,
Afadhali nikatape, bila hata kuwajali,
Huu mwaka ninasema, Mungu mbele siku zote.
Yale ninayoyakuli, ya Allah uyabariki,
Yajapo hata maswali, majibu yakaafiki,
Katu mimi nisifeli, kwa kujifanya kisiki,
Huu mwaka ninasema, siondoki kapa kamwe.
Ninaomba nishaliki, nisizame baharini,
Nielee ja samaki, asiyeishiwa kani,
Sitaivumbika chuki, daima nitaauni,
Huu mwaka ninasema, naishi katika ndoto.
Mtunzi: Alfred Lobawoi
Lakabu: Mweledi Chipukizi
Mahali: Ruiru.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER October 3, 2026
- Ruto puts Coast landlords on notice over squatter harassment
- Nairobi lights candles for Raila in Uhuru Park tribute
- Jambojet returns to Entebbe with daily flights and fares from KSh22,950
- From Lamu to the region: What the Dangote Refinery could mean for Kenya’s energy economy