Fatma Ali Mohamed
Yangaambwa mengi mambo, kwa nguvu na jitihada
Ya wazi na ya mafumbo, yakaongezwa na shada
Halivuki langu umbo, bure mnajipa shida
Yalishaambwa zamani, toka tumboni mwa ummi
Yalisemwa hadharani, Kisha yakawa uvumi
Heyebadili kanuni, ugali ukawa lami
Bure mwajipa adhabu, kushinda vibarazani
Mwajijazia dhunubu, ijapo hambaini
Harakieni kutubu, hatudumu duniani
Vile hamkati cheti, mnayotaka Ambani
Mimi niko madhubuti, subira iko moyoni
Nahisi sipandi chati, kuwajibu majununi
Ingalikuwa maneno, yaondosha utu wangu,
ningefanya mapambano, tusi lenu tusi langu
Na ningejikaza mno, ushindi ukawa wangu
Ila maneno si mtu, hayawezi niadhibu
Sitoifanya papatu, kugombana na kidhabu
Nitabakia sukutu, Mola atawaadhibu
Pia maneno si nyuki, kwamba yatanitafuna
Semeni na sishituki, usiku pia mchana
Sitowafanyia chuki, sababu habari sina
Nakuomba ya Manani, mjao nipe subira
Sishindane na wahuni, ikanivuka Sitara
Yote nawasameheni, kwa Mungu hili ni bora
Mtunzi: Fatma Ali Mohamed
Mahali: Pemba – Zanzibar