Momanyi Henry
Tanzia imetufikia, gwiji ametuondokea,
Taifa nzima linalia, buriani katupungia,
Na kiza kimetuingia, majonzi yametuvamia,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
1.
Myongo mitano amedumu, kwenye tasnia ya habari,
Ana tajriba ilodumu, yenye kuonewa fahari,
Alikuwa nguzo muhimu, katika uanahabari,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
2.
Na “je,huu ni uungwana,”daima tutaikumbuka,
Binafsi nakumbuka sana, redioni kutobanduka,
Alitutia uungwana, hata sasa tulikofika,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
3.
Mengi ameyashuhudia, jaribio la mapinduzi,
Anajua yalotujia, ilipotokea ajizi,
Yeye alitutangazia, ilivyokuwa yake kazi,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
4.
Yajapo tumeyapokea, ijapo tumenyong’onyea,
Ziraili amenyakua, uchungu umetuzidia,
Kifo utakuja jutia, ukingoni ukifikia,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
5.
Nchi nzima ilitambua, busara na mchango wake,
Sote twamuombea dua, aendapo safari yake,
Mbele za haki ametua, na sisi tumo nyuma yake,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
6.
Beti saba ninakomea, taabili kukutungia,
Umetuacha tunalia, kumbukumbu zimesalia,
Mola atatuepushia, kwenye wema ukitulia,
Ametupungia kwaheri, sogora MAMBO MBOTELA,
7.
JINA: Momanyi Henry
LAKABU: Malenga Mtanashati
ENEO: Kesogon.
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- KEMSA chief outlines supply chain reforms ahead of health summit
- Why Audi’s smaller models are often more desirable than their bigger brothers
- The politics of tomorrow: Why Kenya keeps replacing the future with the next election
- Linda Mwananchi movement warns of plot to disrupt Homa Bay rally
- When equality stops asking questions: Why Kenya must recalibrate its gender agenda