Alfred Lobawoi
By: Wanjohi. P. Mugambi
Hebu Tueleze Mengi kukuhusu

Alfred Lobawoi ni mzawa wa kaunti ya Laikipia. Masomo yake yalianzia katika shule ya msingi ya Oljogi na baadaye alijiunga na shule ya upili ya St. Joseph Tigithi Boys. Ari yangu ya kukipenda Kiswahili ilianzia chekechea. Ilhamu yangu ikakuzwa zaidi na Bi. Halima Hussein katika shule ya msingi aliyeona mshawasha wangu wa kukienzi Kiswahili zaidi. Walimu wengine walionichochea ni Bw. Francio Obadiah, Victor Chimasia na Bw. Kabue hadi nikawa jinsi nilivyo. Nawathamini sana.Bidii hizo zimenifaulisha katika nyanja za uandishi na kuanza kutunga mashairi, hadithi fupi na hata kualikwa redioni na runingani kukiendeleza Kiswahili. Kazi ya kwanza kuchangia ilikuwa diwani ya Malenga wa Afrika ya mashairi na baadaye nikachangia katika mkusanyiko wa Gilasi Iliyovunjika na hadithi nyingine. Msururu wa kazi zingine zilifuatia kama vile Lulu za Ushairi, Dagaa na Mashairi mengine, Utando wa Ushairi, Wosia na mashairi mengine, Njia ya Mwongo na hadithi nyingine miongoni mwa kazi zingine.
Isitoshe, kwa sasa nipo katika taasisi ya Mafunzo ya NIBS ambapo nasomea shahada ya Uanahabari huku nikiendesha vipindi vya Kiswahili. Si hayo tu, pia nachangia sana kwenye Gazeti la Taifa Leo na Daily Nation kuandika mashairi, mijadala na barua kwa mhariri ambayo inanipa nafasi ya kuonyesha ueledi wangu uandishini na umilisi wa taaluma ya uanahabari.
Nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Kilichonichochea niwe jinsi nilivyo ni kwa sababu vijana wengi hawajiamini kwa kile ambacho wanachokifanya. Nafasi hii ambayo nipo itawapa msukumo wa kutia fora na kujisabilia zaidi bila woga kufanikisha malengo yao. Kusoma vitabu vya Kiswahili kumenisaidia. Waandishi wa fasihi kama Said A. Mohammed, Ken Walibora, K. Wamitila na Timothy Sumba vimenilea katika uandishi. Pia kuwasikiliza wanahabari ninaowaenzi tangu kama vile; Leonard Mambo Mbotela, Jack Oyoo Sylivester, Mathias Momanyi, Wambugu Yusuf na Rashid Abdallah kumenijenga sana. Wanazungumza Kiswahili fasaha na cha kuvutia.
Siku yako huwa vipi kunapokucha
Siku ambayo ilikuwa bora katika safari yangu ni wakati ambapo niliandika shairi langu la kwanza na likachapishwa kwenye gazeti la Taifa leo. Hatua hiyo ilinijenga sana na kunifanya nijiamini zaidi kupiga makasia popote pale. Mbali na hayo nilialikwa kwenye kituo cha TV47 kwenye kipindi cha Ulingo wa Mwandishi na hata Radio 47 kwenye kipindi cha bahari ya Elimu jambo ambalo nalionea fahari sana kila leo. Kushirikishwa pia kwenye uhariri wa vitabu kama vile Tasnia ya Ushairi, Utando wa Mashairi na Taswira ya Maisha kumenitanua wigo sana.
Je, unaandika kuhusu nini hasa
Kazi ambayo napenda kufanya kwa dhati ya moyo wangu ni kuandika hadithi na kutunga mashairi kwa minajili ya kuifaa jamii. Napenda kufunza, kuelekeza na kutoa hisia zangu kupitia kazi za fasihi mno, ili kuwafikia watu wengi.
Umepata ugumu upi katika kuandika
Ugumu ambao nimewahi kuupata ni kuchangia diwani ambayo ilinihitaji kulipa kiasi fulani cha hela. Wakati huo ulikuwa mgumu sana kwangu hata nikasitisha kutuma miswada yangu kwenye mashirika ya Uchapishaji.
Je, umekutana na changamoto zipi?
Katika maisha hapakosekani changamoto kwa kuwa hiyo ndiyo njia mojawapo ya kunifanya niwe imara na kuniandaa kwa ajili ya maisha ya kesho. Mda wa kuandaa kazi zangu imekuwa changamoto kubwa, kupata nafasi ya kutafiti, mazingira ambayo nafanyia kazi husika na pia kutimiza makataa yanayotolewa na baadhi ya mashirika ya uchapishaji.
Nini kimekusaidia kuziepuka changamoto hizi
Kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwa kila jambo kumenifanyizia wepesi wa kupiga mbizi kwenye tasnia ya uandishi. Isitohe, kuwa na mikabala mizuri na waandishi tofauti kumenifanya nikajifunza mambo mengi ambayo kwayo yamenijenga.
Katika uzi huo huo pia kujifunza kutokana na kazi walizoziandika waandishi waliobobea kwenye tasnia ya uandishi na kujirekebisha kila leo ninapokosa, hunipa sura mpya ya ukuaji. Huwa napendezwa zaidi na jinsi marafiki zangu wanavyoniamini niwasaidie kutenda mambo tofauti yanayohusu uandishi. Kwa hakika wamekuwa nguzo kuu. Hilo ndilo jukwaa langu la kutanua wigo hasa.
Je, wewe hutangaza kazi yako? Tueleze kuihusu
Ndiyo natangaza. Huwa natumia mitandao ya kijamii sana kuzitangaza na kupakia baadhi ya kazi ambazo mimi hufanya. Kupitia njia hiyo ndipo mimi hutagusana na watu wa kila nui ambao hupendezwa na kazi hizo na hata kununua vitabu ambavyo nimevichangia.
Nashukuru ukomo wa kushukuru kuwa njia hiyo imeniwezesha pia kupata kazi zaidi ya kuandika kazi ya kiada ambayo ipo katika hatua ya kutathminiwa na Shirika la Uundaji wa Mitaala KICD.
Wape ushauri wale wanataka kuwa kama wewe
Ushauri wangu kwa yule ambaye angetamani kupiga hatua nilizopiga ni kuwa ajiamini. Kujiamini na kuzithamini kazi zozote ambazo atakazozifanya hata iwe ni kidogo ni kuzuri. Hakuna yule ambaye huibuka ghafla na kuwa bora na mzuri wa kuigwa bila ya kupitia mahali. Duniani kuna watu wa kila aina, kunao watakaokuwa tayari kukusaidia na kunao watakaokosa kukusaidia. Usikate tamaa wala kujiona kuwa haufai. Jijasirishe na uanze hapo ulipo ukiamini utaweza. Hakuna jambo gumu.
Isitoshe, kupenda kujifunza kila siku ni kuzuri. Hulka hiyo humwongezea mtu maarifa tele na kumfanya awe na upekee ambao kila mtu atataka kuiga. Jambo jingine ni kupunguza papara na kukubali kukosolewa kwa ajili ya kujiandalia jukwaa la kujikuza.
Je, unanuia kuleta mabadiliko gani katika ulimwengu
Kubadilisha mtazamo hasi kwa wengi ambao hudhania kuwa uandishi wa Kiswahili ni mgumu. Huwa nasikitishwa sana na kauli hiyo ambayo nilipo sasa mimi huwaathiri marafiki zangu kukipenda na kukipigania Kiswahili.
Baadhi ya marafiki ambao huwa tunafanya shughuli hiyo ni Cornelius Nasong’o, Maureen Gakii na Byril Otieno ambao wamejikita katika uandishi wa makala ya Kiswahili gazetini. Mtazamo huo wa kujifunza na kuchangia bila woga kumewatengenezea wengi nafasi ya kung’aa. Natazamia siku zijazo nitwikwe jukumu la kuwa balozi ambaye atashughulikia lugha Afrika Mashariki na hata Ughaibuni ili niwabadilishe wanafunzi, walimu na wahadhiri, mwishowe dunia ipate mtazamo mpya.
Je upo katika mitandao, watu wanaweza kupata wapi?
Kazi zangu zinapatikana kwenye mitandao mbalimbali. Mfano: Mtandao wa Facebook – Alfred Lobawoi, ambapo mimi hupakia kazi zangu za uandishi, mashairi nk. Youtube (Lobawoi TV) au hata kupitia baruapepe lobaalfred757@gmail.com tunaweza kuwasiliana jinsi ambavyo unaweza kupata kazi zangu.