Mathenge Ngatia
By Alfred Lobawoi
Worth Noting
“Niliumbwa niwe mwanahabari niwasilishe, nijulishe na nielimishe pamoja na kuleta suluhu katika matatizo ambayo yanafanyika katika jamii kila uchao na baadhi ya watu ambao wanafaa kuyatatua nao wameyafumbia macho.
Kuishi na watu ambao wanataka wakupange na wakueleze jinsi utakavyokaa huwa ni vigumu sana. Inanipa taabu manake huwezi ukaishi kulingana na matakwa ya jirani yako la hasha, mda fulani inabidi uzime mazungumzo naye kama huna unyenyekevu ndivyo hivyo, hata vita mtapigana sasa kuishi na watu kweli ni mtihani.”
- Kwa kifupi utueleze wewe ni nani?
Jina langu ni Mathenge Ngatia, jina ambalo ni mkusanyiko wa langu na la Babangu, ninalo pia la Kiingereza ambalo ni David. Sipendi kulitumia japo namshukuru Mamangu kwa kuniita Jina la kifalme. Mimi ni mwanafunzi ambaye nipo katika tasnia ya uanahabari na ninapenda sana kujishughulisha na mambo ya kutenda mema na ucheshi na kwa jumla kuonyesha wengine upendo.
- Ni kitu kipi kilikuchochea uwe jinsi ulivyo?
Ni vitu vingi sana ambavyo vimenishinikiza kuwa jinsi nilivyo, nikitangulia kwa uanahabari niseme niseme? Niliumbwa niwe mwanahabari niwasilishe, nijulishe na nielimishe pamoja na kuleta suluhu katika matatizo ambayo yanafanyika katika jamii kila uchao na baadhi ya watu ambao wanafaa kuyatatua nao wameyafumbia macho. Sasa hili ni jambo ambalo limenichochea tangu nilipokuwa mchanga, kisha Mamangu mpendwa Bi. Pouline Ngatia alikuwa anafanya matendo ya kuponya roho za wengine wakati umeishiwa na tamaa angekufariji na kukupa tumaini la kesho, akifanya haya yote nilikuwa mgongoni mwake na ningetofautisha wakati tuliingia na wakati tukitoka jinsi mambo yalivyo. Mama angebadilisha taswira yako katika jamii kama ulikuwa mbaya unasamehewa kutokana na hotuba yake. Hili lilinitia nguvu sana na nikataka kuwa kama yeye au bora zaidi kisha alikuwa na Kiswahili halua. Haya nikatamani sana niwe kama yeye na niheshimiwe kama yeye. Sasa yote ninayomega ni kwa sababu ya Mamangu mpendwa msukumo wake ambao umenifanya nilivyo leo.
- Wewe hupanga vipi siku yako kunapokucha?
Mimi huamka saa kumi unusu kila siku ima nimefanya mambo ya kawaida au kinyume cha kawaida, nikiamka namshukuru Mungu kwa kuniamsha na kunipa nafasi ya kupambana tena na dunia. Kabla sijalala ndio wakati na panga siku yangu lakini wakati ninapoamka sasa nawaza dhahiri kile nitakachotaka kifaulu siku husika, hasa naandika mahali; yaweza kuwa kwenye simu au kwenye shajara ya mambo yangu ya kila siku kisha nafuata hadi siku inapokwisha yale natimiza nasema Alhamdulilah yale sijatimiza nasema Alhamdulilah na naweka imani Mungu atanipa nafasi tena.
- Ni sehemu ipi ngumu kwa kile unachokifanya?
Sehemu ni nyingi sana ngumu lakini kuna pale ndipo upasuluhishe inachukua mda mwingi sana. Kuishi na watu ambao wanataka wakupange na wakueleze jinsi utakavyokaa huwa ni vigumu sana. Inanipa taabu manake huwezi ukaishi kulingana na matakwa ya jirani yako la hasha, mda fulani inabidi uzime mazungumzo naye kama huna unyenyekevu ndivyo hivyo, hata vita mtapigana sasa kuishi na watu kweli ni mtihani.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi zako? Tueleze.
Changamoto ni nyingi na kama hupatani na changamoto ina maana hujajaribu ya kutosha. Mimi hupatana nazo chungu nzima, kazi ya uanahabari unapokea matusi kila uchao mara hukufaa kusema hivi mara unachochea vurugu manake watu watapokea taarifa yako aidha kinyume au waipokee sawa na wajue katika taarifa hapana msimamo wangu hata kidogo, Tena pia kuna changamoto wakati unatafuta taarifa; watu wamenyamaa hawataki kutoa siri inakuwa vigumu sana kwangu lakini nikipiga dua moyo unatulia napata nguvu ya kuendelea na maisha.
- Ni nini kinachokusaidia kuepuka changamoto hizi?
Changamoto utaziepuka ya kwanza ukifeli halafu ukajifunza hilo likifanyika. Tena utalitatua kwa haraka, pili kuwa makini na kuona mambo kitaswira kabla hujayaanza yaani unapanga kwanza kisha unavuta taswira jinsi watu watasema kuhusu kitu fulani kisha fanya vile utaepukana na changamoto nyingi sana. Tatu ni kujijua unajifahamu ufinyu wako ni upi nini haiendi vizuri na wewe halafu ukaipuuza itakuwa sawa. Nne, pigana vita vyako achana na vya wengine ukifanye hivi nguvu yako itatumika vile inafaa, kisha tano mpe Mungu nafasi hizo changamoto atakuletea zikufunze na zikufanye mja bora katika jamiii.
- Ukipewa nafasi ulete mabadiliko ulimwenguni na kwako pia utafanyaje?
Kuleta mabadiliko sio jambo rahisi kama wewe ni mtu wa kuona matatizo pekee, na pia kuleta mabadiliko sio jambo la usiku mmoja. Ni jambo linachukua mda mwingi sana ili lifanyike. Mie ningepata nafasi ya kuleta mabadiliko naweza pigana kitu kimoja tu kwa mwanadamu. Upendo je, tunapendana kweli au ni midomo tu inasaga maneno. Upendo ni nini? Sio swala la kuchezea kama Mungu hatupendi abadan katan tusingekuwa na huu ulimwengu uliojaa mandhari aina ainati mimea wanyama misitu mashine na wanadamu kamwe hangetupa, lakini Mungu anatupenda ndiposa tunafurahia upendo wake. Swali ni je na sisi tungependana kiasi kile dunia ingekuwaje? si tungekuwa tunasameheana? Hakungekuwa na mauaji, mapendeleo, ubinafsi, wivu na vita visivyo na mbele wala nyuma… Ningepigania upendo miongoni mwa watu mimi ni mfano bora.
- Anayetaka kuona kazi zako atazipataje?
Kazi zangu ni nyingi mimi ni mkulima wa mifugo kama Ng’ombe na kuku. Pia mimi ni mwanahabari kazi ambayo naipenda, mimi pia ni CEO wa Ngatia TV ambayo inavuma sana katika mitandao. Mbali na hayo ninafanya kazi Redio 47 hasa katika kitengo cha Lugha Gongana ndani ya kipindi cha Bahari ya Elimu kila Jumamosi. Naendesha kipindi ndani ya NIBS Fm kinachoitwa Chemko la Jamii. Hata hivyo, mimi pia ni ripota wa haiba; haya yote ukitaka kuyaona mitandaoni hata chat GPT ukitandika tu mathenge Ngatia kazi yote utapata na Mungu atakubariki, sote tupendane