1.Hebu tueleze mengi kukuhusu
Naitwa Franklin Onyango Omusikoyo. Nimezaliwa katika kijiji cha Ebubule, Mumias. Nimesomea katika shule ya msingi ya Ahong’injo kisha nikajiunga na shule ya upili ya wavulana ya Kaimosi katika kaunti ya Vihiga ambapo nilifanya mtihani wangu wa kitaifa na kufua dafu mnamo mwaka wa 2023.
Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea taaluma ya uanasheria mpaka sasa.Taaluma iliyonipendeza zaidi kufanya baada ya shule ya upili ni ya uanasheria kwa sababu ina mambo mengi yanayonipendeza . Kwa sababu taaluma hiyo huwa na kufanya utafiti na uchunguzi wa hali ya juu ambapo kibinafsi mimi hufurahia kazi hiyo,pia huwezesha utetezi wa haki na kupigania usawa wa kila mmoja ,vilevile,inaleta ubunifu kwa anaye somea kwani kila kesi huhitaji suluhisho mwafaka ili kutatua hivyo basi kukuza uwezo wa kufikiria.Isitoshe,taaluma hiyo huwekeza ujuzi fulani kwa mwanafunzi ambayo humsaidia kutatua kesi zinazochipuka.Hivyo ndivyo vilivyonipendeza na kunifanya kutaka kusomea uanasheria.
Baadhi ya walionichochea pia ni Ami wangu ambaye ni mwanasheria maarufu na mwenye sifa chungu nzima ,ueledi wake katika taaluma hiyo ulinichochea zaidi kutaka kusomea taaluma hiyo.
Pia ,kupitia kutizama vipindi kadhaa kama vile “vioja mahakamani ” katika runinga vilinipa motisha na ari zaidi .Halikadhalika,sifa na umaarufu unaotokana na taaluma hiyo pia ni baadhi ya vitu vilivyonichochea.
Kitu kingine ninachojihusisha nacho ni uandishi wa vitabu kwani ni kitu ninachopenda pia ,wazazi wangu ndio walionichochea kujikita katika uandishi wa vitabu vya hadithi na pia kunikosoa popote ninapo fanya kasoro.Nakumbuka nilipokuwa katika darasa la saba ,Babangu alinielekeza kuhusu uandishi wa vitabu na pia kunipa nafasi ya kuweza kuandika kitabu kimoja cha hadithi almaarufu “Taswira ya Maisha”.
Vilevile,najikita pia na kusomea ujuzi katika tarakilishi kwani teknolojia ya kisasa inahitaji ujuzi wa undani katika tarakilishi haswa katika kuimarisha usalama wa data na Mali za wenyewe.
2.Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Kilichonichochea hasa kujitahidi na kuzama katika tasnia hii ni mvuto na motisha kutoka kwa wanasheria na majaji mbalimbali walioonesha weledi wao katika masuala ya kisheria na kufanikiwa katika nyanja hiyo.
Vilevile, hamu ya kutaka kutetea haki za watu ilinipa motisha. Niliona kuwa watu wengi hawajui haki zao na walihitaji kujanjarushwa kuhusu mkondosheria faafu. Isitoshe, hamu na hamumu ya kupenda kutatua shida pindi zinapotokea ilinitawala. Niliamini fika kuwa uanasheria utanipa fursa mwafaka ya kutimiza ndoto yangu. Basi nikajitolea mhanga na kutia fora masomoni kwa kufahamu fika kuwa mtaka cha mvunguni sharti ainame.
3.Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Aghalabu, siku yangu huwa na shughuli dabali pindi kunapokucha ikizingatiwa kwamba mimi ni mwanafunzi anayesomea uanasheria. Taaluma ya uanasheria ni pana kama uwanja wa ahera na inavyo vitengo vingi mno kuliko watu wanavyodhani. Kimsingi, mimi huanza kwa kupiga jaramba kisha mazoezi ya viungo vya mwili kabla ya kuzingatia shajara yangu ya siku. Baada ya kustaftahi huwa nabukua makala mbalimbali yaliyoshiba elimu ya sheria ili kujichotea maarifa. Katika uzi uo huo sikosi kuhudhuria mihadhara chuoni na kufanya utafiti katika nyanja za kisheria.
4.Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Kinachonipendeza mno katika taaluma yangu ni kupata fursa ya kuhudhuria vikao vya mashtaka kortini. Jambo hilo hunivutia sana na hunifanya nifahamu fika kuwa sheria ni hai. Je, ni nani asiyejua kuwa sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma? Halikadhalika, napenda kutangamana na majaji wa mahakamani ili kupukuchua hekima na busara zao. Katika muktadha uo huo natagusana na wanasheria waliobobea na kubobeana ili kuambukizwa utaalamu aula. Mtagusano huo hunipendeza maadamu hunisaidia kukuza ubunifu na umaarufu katika taaluma ya sheria. Ama kweli chuma hunoa chuma.
5.Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Changamoto kubwa ni uchechefu wa fedha, ukosefu wa wakati wa kutosha na makala mengi ya kusomea ya kisheria. Fedha zimeadimika kama maziwa ya kuku. Wakati nao una mbawa na huyoyoma bila subira. Uhaba wa wakati huathiri shughuli za utafiti. Aidha, taaluma hii inatarajia bidii kutoka kwa mwanafunzi ili kusoma kwa kina kufahamu makala na kesi mbalimbali katika nyanja ya kisheria ambayo ni pana mithili ya bahari.
6.Umewahi kupata changamoto katika kazi yako?Tuambie kuihusu.
Changamoto ni tele Kuanzia kwa uhaba wa pesa za utafiti, kazi nzito ya kusoma na kutatua kesi mbalimbali kulingana na katiba ya nchi ambayo huchosha. Halikadhalika, kutamaushwa na wasemao kuwa taaluma hii inachukua miaka na mikaka kusomea kabla ya kuingia katika soko la ajira. Hata hivyo mimi naamini fika kuwa subira huvuta heri.
7.Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Bidii zangu ndizo nguzo muhimu katika kudhibiti changamoto zinazoniandama.
Pia, uwajibikaji, nidhamu, maombi, kujifunza kutokana na wosia bila kusahau uvumilivu kwa kuwa mvumilivu hula mbivu.
8.Huwa unatangaza kazi yako?Tuambie hatua hiyo inakusaidia vipi?
Mara kwa Mara huwa natangaza kazi zangu katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa kuwa teknolojia imerahihisha mambo. Bila shaka mitandao hiyo ya kijamii inao utitiri wa wateja watarajiwa. Nashukuru utandawazi kwa kuweka mambo wazi. Nimepambazukiwa kuwa mitandao ya jamii huukuza umaarufu wangu na kunifanya kujulikana kama pesa. Umaarufu huo unaweza kunitongozea waajiri na wateja chungu nzima.
Sitaki kusahau kusisitiza kuwa kupitia mahudhurio ya vipindi vya mashataka kortini ambavyo hupeperushwa mubashara katika runinga, sijizolei tu umaarufu bali pia najfunza mengi kuhusu sheria. Ushauri wangu kwa wanaopenda kuwa wanasheria kama mimi ni kuwa wakumbatie bidii masomoni hususan katika lugha zote mbili, Historia na somo la Dini. Ikumbukwe kuwa mbele ya Mwenyezi Mungu yote yawezekana.

