Mhakiki: Alfred Lobawoi
Mchapishaji: African Ink Publishers
Kitabu: Safari ya Bahati
Mwandishi: Timothy Omusikoyo
Safari ya Bahati ni hadithi sisimuzi mno inayoelezea safari ya mhusika Bahati ilivyokumbwa na sadfa, bahati nzuri na hata mikosi kwa upande mwingine. Safari yake inatokana na likizo aliyokuwa nayo hivyo basi kumbidi kusafiri kuenda sehemu mbalimbali kama njia mojawapo ya kutumia likizo hiyo yake kujifurahisha na hata kupata nafasi ya kujionea mambo mengi ambayo hakuwahi kuyaona.
Mwandishi wa kazi hii Bw. Timothy Omusikoyo Sumba ambaye ni mzoefu wa kazi ya aina hii hasa kwa kitembo cha watoto ameandaa kwa minajili ya wanafunzi wa gredi ya 3, 4, na 5. Kupitia kwa kazi hii jinsi ilivyofinyangwa mwanafunzi yeyote atakayediriki kusoma atajifunza misamiati aina ainati hasa kuhusu vyombo vya usafiri. Kadiri miaka inavyosonga mambo yanabadilika, vivyo hivyo baadhi ya mambo yaliyobadilika mwandishi ameyaangazia na kumweka msomaji katika usasa. Hii ni mbinu ambayo itamvutia msomaji yeyote yule aliyekuwa katika ukale kutumbukia katika usasa ambao umesombwa na ulimwengu wa kiteknolojia.
Lugha iliyotumiwa katika utunzi wake ni rahisi na wa kueleweka wazi ili kumpa msomaji nafasi ya kuelewa kwa kina ujumbe uliopitishwa. Pia ni njia mojawapo ya kuwakuza wanafunzi wawe na umilisi aula wa lugha wanavyozidi kukwea ngazi ya elimu.
Sifa mmojawapo ya kitabu hiki ni jinsi ambavyo kimejikita kwa usasa na kueleza kinagaubaga jinsi ambavyo athari zake zilivyo. Usasa huu umeletwa na familia ya mhusika Bahati anayejipata katika familia inayojiweza. Mhusika huyu anapendwa na wanafamilia yake hadi ya kupendwa. Kupitia kwa kazi hii, Bahati anapata fursa ya kutembea mahali popote atakapo kwa kuwa familia yake inajiweza kifedha.
Hali hii inageuka kuwashangaza wanakijiji wa Lukongo ambao hawaamini macho yao wanapomwona mtoto mdogo ambaye amepata bahati na mapenzi kutoka kwa familia yake. Ujombani alikoenda alilakiwa na wanakijiji baada ya Inspekta Salome kumbeba kutumia karandinga la kazi. Hii ni baada ya baiskeli aliyokuwa akiendesha kuharibikia njiani. Wanakijiji kabla ya kumlaki walishangaa iwapo Bahati alikuwa amekamatwa na polisi, ila kwa bahati nzuri wakapambazukiwa ilikuwa ni wema wa inspekta huyo mwema.
Isitoshe, kazi hii imeyashughulikia maudhui mbalimbali kama vile teknolojia, wakati ambapo Bahati mwenyewe ana nafasi ya kutumia simu ya mkononi na kutagusana na ulimwengu wa mitandao ambapo utumiaji huo unamponza anapowapigia zimamoto simu kiholela. Pia maudhui ya utabaka unajitokeza wazi baina ya wanajamii wa Lukongo na familia ya Osiang’o. Familia hiyo ina wasomi ambao wanamiliki magari na hata wengine kufanya kazi serikalini. Elimu pia ni maudhui ambayo yamejitokeza pia. Wanàkijiji wa Lukongo kufanya kazi ya udereva, udaktari na hata wengine kuwa rubani yadhihirisha jinsi ambavyo jamii yao ilivyoelimika.
Uwajibikaji pia ni jambo la maana sana ambao unamwokoa Bahati alipozama kwenye mto Shisama. Sewe alimwokoa Bahati kabla ya kukata roho kisha Auma akawapigia madaktari simu wakaja haraka kutumia Ambulensi.
Halikadhalika, ushirikiano pia unajitokeza pindi ambapo baiskeli ya Bahati inapoharibika. Usaidizi kutoka kwa marafiki zake kumbebea baiskeli yake kwa mkokoteni kisha Inspekta Salome kutumia karandinga la kazi kumbeba hadi ujombani, unadhihirisha ushirikiano. Isitoshe, pia familia ya mzee Osiang’o inashirikiana kuandaa sherehe ya Krisimasi kwa ajili ya kusherehekea pamoja na familia yake. Hali hii inaonyesha jinsi ambavyo upendo wao umekithiri kwa kutambua kuwa umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
Mbali na hayo kazi hii pia ni kichocheo cha wanafunzi kujifunza vyombo vya kila aina vya usafiri ambavyo vinatumika. Kando na wengi kujua baiskeli, gari na treni. Pia helikopta aina ya chombo cha usafiri ambacho hakijajulikana na wengi. Wengine pia hutumia wanyama kama vile farasi na punda kama njia mmojawapo ya kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine. Wanafunzi wengi watapambazukiwa kuwa vyombo vya usafiri ni vingi na hutegemea pa kusafiri; iwe ardhini, angani au majini. Zaidi ya hayo, nimependezwa sana na matembezi ya Bahati ambayo yanamfanya kutagusana na vyombo vingi vya usafiri na kumfanya kujua mengi. Ikumbukwe kuwa ni wengi ambao wangetamani sana kujua baadhi ya vyombo vya usafiri kama vile Helikopta, tuktuk pamoja na garimoshi ila hawajawahi pata nafasi hiyo. Kutalii kwa Bahati, kutawabadilisha wengi mtazamo na kuwatia bidii ili nao waabiri vyombo hivyo siku moja.
Mafunzo mengine yanayotolewa na kazi hii ni kuwafunza wanafunzi uzuri na ubaya wa vyombo vya usafiri. Jambo la kwanza, gari hutumia petroli ambayo huwa gharama kwa wakati mwingine kutokana na bei ya mafuta kuwa juu. Kadhalika, gharama ya kutengeneza inapoharibika huwa juu tofauti na yule anayemiliki baiskeli. Baiskeli pia imezungumziwa kuwa vyombo vya habari ambavyo husaidia kuimarisha afya mwilini. Wengi hutumia kufanya mazoezi. Mafunzo mengine yanajikita katika utiifu, ambapo mhusika Bahati anatii ushauri wa walimu na wazazi wake kutokubali msaada wa watu wasiowajua. Watu wa aina hii huweza kusababisha hasara katika jamii na hata kuleta majuto. Ujasiri wa Bahati unamwokoa kutokana na mambo madogo madogo anayokutana nayo katika safari yake.
Sadfa ni mbinu nyingine ambayo imeipa kazi hii mashiko baada ya mhusika mkuu Bahati kusadifiana na baadhi ya mambo. Kupitia kwa kazi hii imesadifu kuwa mhusika bahati anaitwa Bahati ambayo inamtendekea pindi anapofika ujombani; mjomba wake anafika, halati wake, wakoi wake na wenyeji. Hilo ni jambo ambalo hakulitarajia.
Kwa mtazamo wangu nimependezwa mno na mtiririko wa vitushi katika kazi hii. Sina shaka itamtia msomaji ilhamu ya kujifunza lugha ashirafu ya Kiswahili, misamiati na hata kuwa njia ya kumfanya akienzi lugha hii. Nakipigia upatu sana pia kwa wanafunzi wa kitembo cha gredi ya 3, 4 na 5 wakichangamkie kwa hali na mali. Mwanafunzi yeyote anayetaka kuwa na umilisi mzuri wa lugha na awe mwandishi mzuri wa lugha hutegemea jinsi anavyotumia mda wake kuzisoma kazi za fasihi. Hakuna mwandishi mzuri ambaye huibuka ghafla bila ya kusomasoma kazi ya kila aina.
Mwisho kabisa mafunzo yake ni mazuri mno. Mwandishi ana uwezo wa kuteka msomaji. Mfano kumsafirisha kuanzia eneo moja hadi eneo lingine jambo ambalo litamfurahisha msomaji. Pia yatahadharisha sana jamii hasa wazazi wawe wawajibikaji kwa watoto wao pindi wanapowalea ili wasije wakawa balaa katika jamii.