Ulifunge lako domo, uwache kubwatabwata
Maneno yawe hayamo, Usisambaze sakata
Fitina weka kikomo, kubwabwaja sasa kata
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Usijifanye redio, kutangaza ya wengine
Baya lako kusudio, kila siku na mengine
Watujuza kwa rudio, mara nyingi sio nne
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Hata kama umeona, punguza kubwatabwata
Labuda chozi latona, na maini yanakata
Ukitangaza wadona, roho zetu kwa utata
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Nawe kweli msemaji, mbona yako wayaficha
Kutangaza hutaraji, wanyamaza kutwa kucha
Kimya wakivika taji, ya wengine unachacha
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Ya wenzako wayasema, Kila pande watangaza
Domo lako latetema, ndipo unanishangaza
Wasema bila kuhema, bila kitu kubakiza
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Unasema kwa kelele, vijijini na mijini
Domo lako ni kengele, yasikika na njiani
Wazitoa siri tele, waziweka hadharani
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Unaupoteza muda, ya wengine kubwabwaja
Unatoa ushuhuda, bila shaka watutaja
Waisambaza husuda, Domo lako lina chaja
Domo lako bwaku bwaku, ebu wacha kubwabwaja!
Mtunzi: Omar Duncan
Mahali: Lungalunga