Raphael Mugi
Hebu tueleze mengi kukuhusu.
Jina langu ni Raphael Mugi lakabu ni Tuju mzaliwa wa Nyeri. Nilipokezwa malezi yangu na wazazi wangu wapendwa Joseph Mahinda na Rose Wanjohi katia eneo la Ngobit Laikipia Mashariki nyumbani tulikohamia tangu nilipotimiza miaka miwili karibu na mbuga la wanyamapori Olpajeta. Mimi ni mshairi chipukizi anayejaribu kupiga makasia kila kuchao. Ndoto yangu ya kupenda mashairi na kuyatumbuiza ilitokea mwaka 2012 nilipokuwa darasa la 3 na mwalimu wangu mkuu Bi. Pauline.N. Mumbiko. Alinifunza jinsi ya kuyakariri hata kwenye tamasha za muziki ambapo nilijizolea ushindi. Nilijiunga na shule ya upili ya kitaifa ya wavulana ya Nanyuki iliyopo Laikipia. Sikushiriki sana kipindi kile ingawa utahini wa mashairi na walimu wangu Bwana Kamweti, Bwana Musyoki, Bwana Murimi, Bwana Kabati na Bi. Waihenya ulinipa mshawasha wa kuyapenda mashairi. Nawashukuru sana mwalimu mkuu Bwana Minishi Oliver na naibu naibu wake wa maswala ya kiakademia Bwana Gitonga waliohakikisha Kiswahili kimekumbatiwa katika sekta zote, drama na muziki na pia ufunzaji darasani. Nilijiunga na chuo kikuu cha Kiteknolojia Cha Murang’a ninapoendelea kufanya shahada ya ualimu katika Kiswahili na Historia tangu mwaka 2022. Hapa ndipo niliamua kuendeleza uandishi wa mashairi na hata kupata fursa kuyakariri shuleni katika hafla ya kufuzu kwa wanafunzi sherehe ambazo zilikuwa mubashara runinga za KTN 2023 na NTV 2024 mtawalia. Kwa kudura za Mwenyezi Mungu nimeweza kuchangia miradi miwili ya diwani za mashairi. Mmoja ni Halua ya ushairi na Wasifu wa Hassan Muchai. Mashairi yangu pia yamekuwa yakichapishwa kwenye gazeti la Taifa Leo Jumamosi tangu mwanzo wa 2023. Nawavulia chepeo wahadhiri wangu Dkt Jane Maithya, Dkt Miricho na Dkt Rose Kawira ambao wamenishika mkono, wakanielekeza na kuwa kielelezo bora kwangu. Namshukuru pia ndugu yangu mkubwa Martin Mugi ambaye kila wakati hunitia matumaini kuwa kesho itakuwa bora kuliko leo kupitia juhudi zangu za kujiboresha.
Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Mwalimu wangu mkuu Bi. Pauline N. Mumbiko ndiye alinipa mshawasha huu nilipokuwa darasa la tatu 2012. Aliandika mashairi kisha akanipa na kunifunza kuyakariri ambapo niliyatumbuiza katika hafla ya kumuenzi Padri Luigi Cabiuroto wa parokia yangu ya Sirima. Pia niliyakariria viongozi wetu walipozuru shuleni kama gavana Joshua Irungu, mbunge Anthony Kimaru na diwani hayati Kamakia. Pia ndugu yangu mkubwa ya kufa kupona Dennis Ngatia wa Karatina alinivutia sana nilipomsoma kwenye gazeti na kumsikia redioni. Dadangu mkubwa Esther Wairimu pia alinichochea sana kupenda ushairi sababu ndiye alikuwa mwalimu wangu aliponifanyisha mazoezi ya kukariri ili niweze kuibuka kidedea.
Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Siku yangu huwa shwari mara nyingi kunapokucha ila wakati mwingine najipa moyo tuh hasa ninapomuwaza mama ambaye sijui alipo.
Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Mimi hupendezwa na mashairi hasa ya mahaba au ya kunitia moyo. Mashairi kuhusu hali halisia ya inayokumba nchi yangu Kenya.
Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Ugumu huwepo katika kuishi maisha ya chuo lakini kujituma siku zote ni muhimu. Watu wengine pia hunidhihaki pia wanapouliza hiki Kiswahili ninachotetea kila wakati kitanisaidia wapi. Mimi huwajibu kuwa “IPO SIKU” watajionea wenyewe.
Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.
Nimepata changamoto ya uuzaji vitabu vyangu vya mashairi. Watu wengi hawapendi vitabu vya Kiswahili kwa ujumla na pia kusoma au kununua kazi hizo ni nadra sana.
Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Mhadhiri wangu Dkt Maithya hunisaidia kupambana na changamoto hii hasa anapoamua darasa letu litashughulikia ushairi na tutachambua diwani yangu. Wanafunzi kadhaa huwezi kunifuata ili kufahamu zaidi kuhusu mashairi. Kutokufa moyo pia hunisaidia kuwa na matumaini makubwa.
Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia.
Huwa natangaza kazi yangu mtandaoni kupitia makundi whatsap, sasisho langu na video katika ukurasa wangu wa tiktok@Tuju Raph.
Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe.
Anayetaka kuwa malenga, mimi nampa moyo aanze manake safari ndefu huanza kwa hatua moja. Lazima ajiamini anaweza sababu usipojiamini hakuna atakayekuamini unaweza.
Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?
Nikipatiwa nafasi ya kubadisha ulimwengu nitakipigania Kiswahili kwa udi na uvumba hadi kipate utambulisho kama lugha ya kuwaunganisha watu wote ulimwenguni . Kwa vile binadamu ni kiumbe dhaifu, nitajirekebisha nilipofanya dosari na kujiboresha kila siku.
Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?
Yeyote anataka kuona kazi zangu anitafute kwa nambari ya simu 0742343449 katika whatsap, katika ukurasa wangu wa tiktok @Tuju Raph na pia katika facebook. Kiswahili kitukuzwe hadi kitukuke, viswahili vifukuzwe. Ahsante sana
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Gunners end Villa’s winning streak
- Loyalty in Hollywood: Does It Really Exist?
- Fernandes rewrites the record books as United cruise past Brighton
- Senegal’s Revolution Eats Its Own: President Faye Sacks Prime Minister Sonko as Debt Crisis Deepens
- Government scholarships are out there — you just need to know how to find them!