By Alfred Lobawoi
Worth Noting
“Tuzo hii ni tuzo kubwa zaidi ya Kiswahili Afrika, ambayo sasa imeendelea kutambua mchango wa fasihi ya Kiswahili kwa miaka 10 mtawalia. Hili ni jambo kubwa, si tu kwa zawadi za fedha watoazo, ila kuyachapisha maandishi ya watunzi na kuyatafsiri kwenda lugha nyingine, ni katika kuhakikisha kuwa dunia inapata kusoma fikra za watunzi, ambao wengi ni vijana na chipukizi.
Kubwa ni kujiandaa na kuhakikisha kuwa kazi inakuwa nadhifu na imekidhi vigezo anuwai vilivyowekwa bayana.
Niliandaa uandishi kwa msukumo wa ndani ya moyo, na si kingine. Na hasa huwa ni kujiliwaza na kujipoza, ila faida nyinginezo zikipatikana inakuwa ni ziada tu.
Ushauri mkubwa ni kusoma sana kabla ya kuandika. Na kuandika bila ya kuchoka, bila ya kutarajia kusifiwa au kupata fedha, kusifiwa na fedha kusiwe kusudio kuu, ila kuje kwenyewe kama tija baada ya hadhira kukiri uzuri wa kazi.”
- Tueleze Bashiru Abdallah ni nani kwa kifupi?
Bashiru Abdallah ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto 7 kwa Mama wawili na Baba mmoja. Nilizaliwa Mei 8, 1992 Ujiji – Kigoma. Nimeanza uandishi wangu mwaka wa 2015 kwa siri na kuanza kuandika kwa dhahiri 2018.
- Unahisije baada ya kushinda tuzo ya heshima katika kitengo cha mashairi kwenye tuzo hii?
Ni fakhari na furaha kubwa kuwa kwenye orodha fupi na hatimaye kushika nafasi ya kwanza kwenye tuzo hizi kubwa kabisa za Kiswahili. ‘Bure Ghali’ ndio mkusanyiko wa mashairi ambao niliuandaa na kutuma kwenye mashindano haya; hasa ikiwa ni baada ya majaribio mengi. Baada ya dhiki faraja.
- Je, mashairi ambayo uliyawasilisha yalikuwa vipi?
Mashairi niliyowasilisha ni mashairi ambayo yameandikwa kwa muktadha na hisia tafauti ambazo zinagusa jamii zetu, lakini pia zinazoakisi ukweli wa mambo kimafumbo na kuacha hadhira iamue yenyewe makusudio na tafsiri zake.
- Ulipata vipi msukumo wa kuyatunga mashairi?
Msukumo wa kutunga mashairi kwa ujumla kwangu huja kutokana na fukuto la roho na mambo yanayonipitikia au kuwapitikia wengine. Niliandaa uandishi kwa msukumo wa ndani ya moyo, na si kingine. Na hasa huwa ni kujiliwaza na kujipoza, ila faida nyinginezo zikipatikana inakuwa ni ziada tu.
- Mashairi yako hujikita katika maudhui gani na mbona?
Maudhui ni nyingi, kwa ujumla nadhani mengi katika yanayotuzunguka nimeshayaandikia.
- Huwa unatumia mbinu ipi kuhakikisha kuwa mashairi yako yana mguso kwa hadhira?
Kubwa ni kuuvaa uhusika, na kuteua maneno sahihi ili kugusa hisia za hadhira. Ninachoshukuru ni kuwa nimeweza kupitia kazi za wengi katika wakongwe na chipukizi wenzangu ili kupata mawazo, mbinu, ufundi na kujifunza zaidi na zaidi.
- Katika sanaa hii ya ushairi, ni washairi wepi ambao walikuathiri?
Wako wengi ila wa mwanzo kabisa ambaye ndiye aliyepanda mbegu rohoni mwangu ni Alhaj Osan Omar Ngulangwa, na baadaye nikasoma na ninaendelea kusoma kwa wengi wakongwe na Chipukizi. Siwezi kumtaja mmoja mmoja.
- Tuzo hii ya Safal Cornell ina mchango upi katika makuzi ya Kiswahili?
Tuzo hii ni tuzo kubwa zaidi ya Kiswahili Afrika, ambayo sasa imeendelea kutambua mchango wa fasihi ya Kiswahili kwa miaka 10 mtawalia. Hili ni jambo kubwa, si tu kwa zawadi za fedha watoazo, ila kuyachapisha maandishi ya watunzi na kuyatafsiri kwenda lugha nyingine, ni katika kuhakikisha kuwa dunia inapata kusoma fikra za watunzi, ambao wengi ni vijana na chipukizi.
- Ni changamoto zipi ulikumbana nazo wakati wa kujiandaa kushiriki tuzo hii?
Changamoto ni nyingi, na hazikosekani hata kidogo. Hasa unapojiandaa kuwasilisha muswada. Ila kubwa ni kujiandaa na kuhakikisha kuwa kazi inakuwa nadhifu na imekidhi vigezo anuwai vilivyowekwa bayana. Ingawa, inahitaji kutenga muda mwingi na kutuliza akili kwenye kuusuka muswada lakini pia kuwapatia watu wa karibu kuutazama, jambo ambalo si wote wanaweza kukupa ushauri stahiki.
- Una ushauri upi kwa washairi wachanga ambao wangependa kushiriki kwenye tuzo hizi?
Kwanza nami sijitoi kundini, lakini ushauri mkubwa ni kusoma sana kabla ya kuandika. Na kuandika bila ya kuchoka, bila ya kutarajia kusifiwa au kupata fedha, kusifiwa na fedha kusiwe kusudio kuu, ila kuje kwenyewe kama tija baada ya hadhira kukiri uzuri wa kazi. Lakini tusikate tamaa na wala tusikubali kukatishwa tamaa.
- Una mipango ipi baada ya ushindi huu?
Hakuna mipango mipya, zaidi ni kuendelea kuzisuka kazi nyingine ambazo ziko mkononi. Tunaendelea kuandika madhali tuna neema ya afya na uhai.

