Gakurya Mwinyi
Mola amesema “Enyi, waja wenye na imani” .
Hajasema “Ewe Mwinyi”, mshangae nina nini!
Yani ni mimi na nyinyi, tusiwaze kina nani.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Imefaradhishwa kwenu, swaumu ya Ramadhani.
Sawa na wa nyuma yenu, walokuwa duniani.
Funga si tu zama zenu, ipapo tangu zamani.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Siku za kuhesabika, ndio funga ya wajibu.
Zifungwe kukamilika, kwa sharuti na kusibu.
Kuna sunna ukitaka, kwa kuongeza thawabu.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Awaye yu safarini, au anayo maradhi.
Hatafunga Ramadhani, na siku azihifadhi.
Atakapotamakani, badalaye atakidhi.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu
Na kwa wale wawezao, wawalishe masikini.
Wawape chakula chao, wasidai hata peni.
Hilo ni jukumu lao, wenye kuifata dini.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Tujue pia ni mwezi, uloshuka Quruani.
Hio yaonesha wazi, wakati tuupangeni.
Tuondoeni ajizi, kitabu tukisomeni.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Aliamuru Mwenyezi, kwenye kuanza swaumu.
Anayeuona mwezi, kufunga yamlazimu.
Ama ambaye hawezi, imeshatajwa hukumu.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Naomba mausitadhi, watunzi wa mashairi.
Waendeleze waadhi, ufahamu ukithiri.
Suala nawakabidhi, zikunjueni suduri.
Tufungeni Ramadhani, ili tumcheni Mungu.
Mtunzi: Gakurya Mwinyi
Mahali: Beirut, Lebanon