Japheth Maundu Nzomo
1.Hebu tueleze mengi kukuhusu?
Naam,jina langu ni Japheth Maundu Nzomo maarufu kama Zao La Hekima.Nilizaliwa tarehe 17/05/2003 kijiji cha Mataka katika wadi ya Kyuso,katika kaunti ya Kitui! Mimi ni mtoto wa tatu katika familia ya wana watano.Nilijiunga na shule ya msingi ya Mataka mnamo 2009 nikiwa na umri wa miaka sita! Shule hii ambayo ilikuwa ya kutwa ndiyo iliyonifanya nikajigundua kidogo maana niliibukia kuwa bingwa katika mitihani yangu, haswa Kiingereza ambacho kilikuwa somo nililolipenda zaidi. Nilifanya mtihani wa kitaifa wa kuhitimisha masomo yangu ya shule ya 2017. Nilipata alama 319 na kuibukia mwanafunzi wa pili katika shule yetu jambo ambalo lilinipa motisha zaidi wa kutia bidii masomoni! Alama hizi zilinipa mshawasha kwamba nitaishia shule ya bweni ya pale nyumbani. Shule Ya Wavulana ya Kyuso ambayo ndiyo iliyokuwa kileleni wakati huo! Hayo yote yalikuwa matamanio ila hayakutimia badala yake nilijipata katika shule ya kutwa ya Kilalai iliyoko Maua,Meru! Jambo hili halikunifurahisha na katika kilele cha utoto wangu nililegeza bongo na kuwa wa kufeli! Nikaamua nitakapotoshea labda kwa uanajeshi na alama ya D+ ilinifaa zaidi katika shule ya upili hadi pale nilipofika kidato cha tatu mwaka wa 2020,korona ikaja.nikaenda nyumbani nikakaa pale mwaka huo wote! Muda huu akili yangu naweza nikasema ilikuwa na upevu kiasi fulani kwani,niliweza kuona matatizo yaliyotukumba, yaliyonikumba mimi binafsi,na nikajiuliza je, ni vipi naweza nikasuluhisha haya? Jibu halikunijia.Janga la korona lilipoisha na tukaruhusiwa kurudi shuleni mwaka wa 2021 nilijituma vitabuni,nikijua ya kwamba elimu ndiyo itakayoniinua! Ila haikuwa rahisi kwangu! Nikifanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne(KCSE) Aprili 2022,nilifeli,na nikarudia kidato cha na kufanya mtihani tena Disemba 2022 ambapo nilipata alama ya B-.Nilifurahi maana nilijua sasa ndoto ya kuingia chuo kikuu imetimia! Hatimaye 2023 nilijiunga na Chuo Kikuu Cha Kiteknolojia Cha Murang’a, kusomea ualimu wa somo la Kiswahili na Historia! Nikipojiunga,sikuwa bado najijua nina nini kama talanta nilichojua ni kuwa Nina talanta kadhaa! Kwa sababu ya kuchanganyikiwa, nilijiunga na vikundi mbalimbali ikiwemo,MUT debate club, murang’a university kamba association, murang’a university meru association, Karate, MUT kamba football club (Elite stars) na Chama Cha Kiswahili Cha Chuo Kikuu Cha Kiteknolojia Cha Murang’a (CHAKIMUT)
Katika CHAKIMUT, ndipo nilijigundua kama mtunzi mwema na hadi sasa nipo katika tasnia hii ya utunzi wa mashairi baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti Bwana Vincent Mutunga na mhariri wangu Bwana Raphael Mugi (Tuju). Sasa hivi mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo Kikuu Cha Kiteknolojia Cha Murang’a! Na mtunzi maarufu wa mashairi,Nina mashairi kadhaa ambayo yameweza kuchapishwa katika gazeti la Taifa Leo,jambo ambalo najivunia!
- Ni nini haswa kilikuchochea katika tasnia hii?
Tasnia hii ya ushairi kusema ukweli ina historia ndani yangu. Nilipokuwa kidato cha nne mara ya kwanza. Nimewahi kuufanya mtihani wa kiswahili nikafeli Sana ila nilipita ushairi! Jambo hili lilinifanya nikapenda sana kusoma mashairi na kutaka kuyaelewa yalivyokuwa, haswa ule urari wa vina na mwingiliano wa maudhui ulinipendeza sana na nikawa na shauku ya kuandika pia!
Ustadh Nuhu Bakari,ni mmoja kati ya watu walionichochea kuingia katika tasnia hii japo si moja Kwa moja maana sijapata kutagusana naye! Nilizipenda kazi zake alizowasilisha katika Runinga ya Citizen kila ijumaa. Nilifurahi sana kumsikiliza na hata wa leo, Nuhu hunipa hamu zaidi ya kutunga mashairi nifike kiwango chake!
- Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Niamkapo shughuli za kawaida huchukua mkondo wake! Mimi ni mwanafunzi Kwa hiyo kuhudhuria madarasa, hutangulia! Haswa semia hii ambayo Nina madarasa mengi asubuhi! Pia,upishi na usafishaji wa vyombo,chumba na mavazi huambatana katika ratiba yangu ya kila siku! Napenda muziki, Kwa hiyo kila siku kuna muda natulia nasikiliza muziki tu! Mazoezi muhimu, huwa najiunga na wanakarate wenzangu katika mazoezi kuanzia saa kumi hadi saa kumi na mbili na nusu! Siku nyingine najiunga na wanasoka nafanya mazoezi pamoja nao!
- Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Naam, kikubwa zaidi kinachonioendeza katika kazi hii ya utunzi wa mashairi ni jinsi ninavyopata nafasi ya kujuana na wapenda lugha wengi ambao kama sio katika utunzi basi nisingeliwajua! Wapenda lugha hawa ni pamoja na Kevin Akuti (Mwana wa Walibora), Mwandishi Timothy Omusikoyo Sumba na wengine wengi!
Pia kule kuchapishwa kwa mashairi yangu katika gazeti la Taifa Leo ni Jambo linalonipendeza sana katika kazi hii kwani huwa najua ndoto yangu ya kutamba na kujulikana, ishang’oa nanga! Kule kuona jina langu na kazi zangu zinasomwa na wakenya wote katika gazeti hunifurahisha sana na kunipa motisha zaidi ya kuendelea na kazi hii!
- Ni kitu kipi kigumu Kwa yale ambayo unafanya?
Uandishi mgumu kweli! Uandishi unataka uaminifu kama mpenzi! Usishike mengine huwe ni uandishi pekee ndio uwe rahisi! Lakini kwangu unakuwa mgumu maana nina masomo nahitaji kusoma,Nina mitihani nahitaji kufanya. Nina shughuli zingine na nahitaji muda wa mazoezi. Hivyo basi, kuishia kutokuwa mwaminifu na uandishi hivyo kuwa mgumu kwangu!
- Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu
Naam,changamoto nimepatana nayo kubwa katika kazi yangu ni Ile ya kukosa hela ya kulipia Ada ya miradi Fulani ya uandishi inapotokea! Mradi mzuri unatokea natunga mashairi lakini ikifika ni hela,nalazimika kuavya mradi huo na kuusahau kabisaa! Pia changamoto za muda na kukinzana Kwa matukio! Unapata matukio yanatukia meengi kwa muda mmoja mpaka nashindwa kuelewa, lipi muhimu lipi si muhimu. Kuchanganyikiwa kunachelewesha utunzi kiasi kwamba ninapotunga. Ujumbe wa shairi langu unakuwa umepitwa na muda! Katika utunzi wangu, maneno ya kutunga hunijia ghafla. Yanapotaka, mahali popote na nisipoyanakili huja nikayasahau kabisa! Pia ninapoyaandika mtu akiniongelesha huja nikasahau maneno yaliyostahili kufuatia hivyo kulazimika kuachana na shairi hilo na kusubiri muda mwingine! Jambo hili hunitatiza sana!
- Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Kikubwa zaidi ni kutafuta njia zangu mwenyewe za kupata maokoto zaidi na kuyahifadhi ili miradi inapotokea niwe na ada yake! Pia tangu nilipogundua kwamba utunzi wangu unahitaji mazingira tulivu ili niweze kuandika na kukamilisha tungo zangu huwa nahakikisha popote niendapo nina kalamu na kitabu na ninaposikia kuna maneno yananijia na nafaa kuyaandika huwa najiondoa penye watu nikaenda nikatulia mwenyewe nikaandika! Na Kwa njia hii nasuluhisha matatizo yangu
- Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia
Naam! Huwa natangaza kazi zangu! Kwenye vikundi vyetu vya shule vya wasapu huwa nazituma kazi zangu pale na kuwafahamisha wenzangu kuzihusu na jinsi wanavyoweza kuzipata.Hatua unipa nafasi ya kutagusana na wengi wanaopendezwa na kazi zangu na wengine kuzilipie niwatumie wazisome kila ninapozitunga! Pia napata nafasi kuwa nao ambao naweza nikawaita wateja wangu Ambao wanapokuwa na shughuli au sherehe wananialika kuwasilisha kazi zangu au wananiagiza niwatungie mashairi! Jambo ambalo naliridhia mno!
- Ni wosia gani utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe?
Mungu huwalisha ndege wa angani,lakini hawapi viotani mwao! Lazima watoke nje ndiposa wapate riziki asilaze damu ajikaze zaidi kwani Mimi huwa siamini eti kuna bahati kwa mzembe, kulingana na mimi bahati ni matokeo ya jitihada! Pamoja na hivyo,azidi kutia dua Kwa Mungu kwani ndiye mpaji wa vyote! Asife moyo. IPO SIKU!
- Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yepi?
Ningebadilisha jinsi ulimwengu unavyowatelekeza wasanii wachanga na kukumbatia wasanii wa kale ambao Kwa sasa wanastahili kuwapa wasanii wachanga nafasi Kwa madai eti hwa wachanga hawana tajriba,wasipowapa nafasi sasa hivi wataitoa wapi? Wao tajriba yenyewe waliitoa wapi! Wasanii wachanga wapewe nafasi! Nami nikawa wakujibadilisha basi ningependa kujibadilisha nifae kila mada inayohitajika na jamii na niweze kuiwahi katika muda mwafaka na pia ningejibadili niwe wa kuhifadhi maneno ya utunzi akilini punde yanaponijia kisha nikatunga baadaye!
- Kwa yuke ambaye angependa kuona kazi zako atazipataje?
Kwa yeyote ambaye angehitaji kuona kazi zangu anijie wasapu kupitia nambari:0795849077
Au apige simu:0705974656
Au tuzungumze pale Facebook najiita Japheth Nzomo,au anitumie baruapepe kupitia japhethnzomo8@gmail.com na atasaidika!
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- Mt Kenya Times ePAPER August 4, 2026
- Court orders release of MP Kaguchia on KSh100,000 cash bail amid hate speech probe
- Sifuna’s moment: The senator who wants to rewrite Kenya’s political script
- Political hate speech: Are we learning from our past, or walking into another dangerous chapter?
- Workers cry foul at Laikipia flower farm