Mfahamu Oscah Mwalimu Omusikoyo

Oscah Mwalimu Omusikoyo

By: Wanjohi. P. Mugambi

  1. Hebu tueleze mengi kukuhusu.
Oscah Mwalimu Omusikoyo

Naitwa Oscah Mwalimu Omusikoyo. Nimezaliwa katika kijiji cha Ebubule Mumias.

Nimesomea katika shule ya msingi ya Ahong’injo kisha shule ya upili ya Ahong’injo kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Musanda ambapo nilifanyia mtihani wa kitaifa (KCSE) mnamo mwaka wa 2023. Baada ya kufua dafu katika mitihani huo nilijiunga na Chui Kikuu cha Rongo kusomea taaluma ya uanahabari mpaka sasa.

  1. Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?

Kilichonichochea hasa kuzama katika tasnia hii ni mwito kutoka kwa Mwenyezi Mungu maanake nilihishi kuwa ninacho kipaji kikubwa katika uandishi pamwe na uanahabari. Basi nikaamua kujiendeleza katika mkondomaisha uo huo. Isitoshe, wazazi wangu ambao ni walimu na waandishi pia walinichochea kuwa mwandishi kwa kuwa siku zote walihakikisha kuwa nazingatia nidhamu ya lugha. Halikadhalika, walininunulia vitabu vya kila nui ili niweze kujichotea ubunifu. Waliniambia kuwa ubunifu huchotwa vitabuni; haufunzwi. Kuanzia hapo mambo yakaanza kujipa. Ama kweli kinolewacho hukata.

  1. Siku yako huwa vipi kunapokucha?

Kwa hakika siku yangu humezwa na mzo wa shughuli za hapa na pale ikizingatiwa kuwa mimi ni mwanafunzi wa uanahabari. Sina budi kuzuru maeneo mbalimbali ili kujua yaliyotokea. Isitoshe, mara nyingi najitumbukiza katika mitandao ya kijamii ambayo kwa hakika ni malighafi ya habari hai na ubunifu.

  1. Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?

Kwanza kabisa nachangamkia kufanya kazi katika mazingira ya kiburudani. Aidha, nafanya kazi nikijifunza kutokana na wengine waliobobea zaidi ya ziada. Chuma hunoa chuma.

  1. Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?

Changamoto kubwa ni wakati na fedha. Mara nyingi wakati huyoyoma na kutaka kufungia baadhi ya shughuli za shajara yangu nje. Pesa ambazo huvunja nguu milima ikalala nazo ni adimu kama wali mweupe. Nataka kufanya mengi ila zanibana. Hata hivyo ninaamini fika kuwa Mwenyezi Mungu atafungua milango ya baraka mnamo siku za usoni.

  1. Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.

Changamoto ni tele jinsi zilivyo faida na manufaa. Changamoto kubwa ni kutamaushwa na Wasemao kuwa shughuli hizi ni bure na hakuna zinapompeleka mtu. Uchechefu wa pesa za kufanya utafiti pia ni kikwazo. Mabadiliko ya mifumo ya kazi pia huathiri mno. Hata hivyo yajapo yapokee. 

  1. Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?

Bidii hunisaidia kudhibiti changamoto ambazo kwa hakika si moto unaochoma kamwe. Vilevile uvumilivu, uwajibikaji, nidhamu na maombi hunisaidia kupambana na changamoto za kila nui. Najua kuwa penye milango ndipo penye mawimbi.

  1. Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia.

Naam, mara nyingi natangaza kazi zangu mitandaoni kwa kuwa utandawazi umerahisisha mambo. Ulimwengu mzima umekuwa kama kijiji cha teknolojia tu. Mambo ni papai kwa kijiko. Mitandaoni kunao utitiri wa watu. Watu hao ndio wateja watarajiwa. Isitoshe, hueneza kazi zangu kupitia kwa jamaa, ndugu na marafiki wema. Wao ndio ngazi ya mafanikio kwangu. Siku zote nashirikiana na wengine kwa kuwa mtu ni watu. Najifunza mengi kutoka kwao nami nikiwasambazia nijuayo huku tukitangaza na kusambaza kazi zetu.

  1. Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe.

Wosia wangu kwa yeyote ambaye angependa kuwa kama mimi ni kuwa na upendo wa dhati katika taaluma yako. Pia, ni vyema kufanya utafiti unaowiana na utakayo kufanya ili ujue ni ubora na mapungufu ya wengine ambao tayari wako sokoni. Nidhamu na uwajibikaji ni viambajengo muhimu kwa yeyote anayepania kuwa kama mimi Oscah Mwalimu. Mwisho kabisa ni bidii. ikumbukwe kuwa bidii ni mali. Mtu asitamani kukwea ngazi ya mafanikio kwa ndoto na usingizi wa pono. Azindukane na kutekeleza ili kutimiza ndoto. Ole wao wanaokumbatia uzembe. Wajuao husema kuwa acha kitanda ili kutanda.

  1. Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?

Nikipata nafasi ya kuubadilisha ulimwengu na kuleta mabadiliko kwanza kabisa nitapakata teknolojia maanake ndiyo inayojua kuendeleza ulimwengu wanguwangu. Pili nitawashirikisha watu wote katika keki ya maisha ili kusiwe na wenye vingi kupindukia wala vichache kukithiri. Nitausawazisha ulimwengu kwa misingi ya hadhi, jinsia, maeneo na kadhalika. Naamini kuwa watu wote ni sawa na wanaweza ilimradi wawezeshwe.

  1. Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?

Kwa yule ambaye angependa kuona au kupata kazi zangu azuru mitandaoni na atajipatia lishe bora. Pia anaweza kuwasiliana nami kupitia baruapepe na namba za simu zifuatazo: Barua pepe-“mwalimuoscar@gmail.com,nambari ya simu-0796437188.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

By Wanjohi P. Mugambi

Wanjohi. P. Mugambi

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *