Nukuu
“Niliendelea na kundi la uanahabari na hata kuigiza tofauti na shule zingine nilianza kushindana na shule tofauti hadi nikafika kiwango cha kitaifa na nikapewa cheti cha ‘best narrator’. Hakuna jambo linalonitia moyo kama kumjengea mtu siku yake. Watu wengi hupitia magumu katika maisha ya kila siku, kwa hivyo ni bora kuwapa sababu ya kutabasamu ili msongo wa mawazo usiwaandame.”
- Tueleze mengi kukuhusu.
Jina langu ni Brayo Ibra ama kijana Vibes home and Away; mzaliwa wa kaunti ya Narok.
Masomo yangu yalianza kaunti ya Nakuru, ambapo nikiwa darasa la sita nilianza kuigiza. Kilichonifanya nijiunge na uigizaji ni tangu nikiwa mtoto nimekua mwenye vituko na ucheshi mno hivyo basi kwa usaidizi wa mwalimu nikajiunga na chama cha kuigiza. Michezo hii ilinijengea jina na kunifanya nifahamike zaidi hadi nikafanywa mkubwa wa michezo yenyewe. Masomo yangu ya msingi niliyamalizia kaunti ya Narok shule ya Narianta Primary School. Kisha nikajiunga na shule ya upili ya St. Gabriel Boy’s Lanet kule Nakuru hapa kwa mara ya kwanza nikaanza kutangaza na kujiunga na chama cha wanahabari, jambo ambalo najivunia hadi sasa.
Nikiwa kidato cha pili niliweza kufukuzwa kwa sababu ya kujiunga na kundi baya jambo ambalo liliadhiri masomo yangu pakubwa. Hapa nilianza kujuta sababu ya kujiunga na makundi mabaya ila kwa bahati nzuri nilipata shule nyingine na kujiunga nayo. Niliendelea na kundi la uanahabari na hata kuigiza tofauti na shule zingine nilianza kushindana na shule tofauti hadi nikafika kiwango cha kitaifa na nikapewa cheti cha ‘best narrator’. Nilimaliza masomo yangu ya upili mwaka wa 2019. Nikaanza kujiunga na kundi la kaunti ya Narok la burudani nikafanya michezo kadha wa kadha.
Kanisa la katoliki pia liliweza kupiga jeki kukuza talanta yangu kwani bado nilijiandikisha kwenye kundi la kuigiza na nikapata cheti na bahati ya kwenda kaunti mingi kushindana kama vile Baringo, Nakuru, Meru na zinginezo. Hapo niliamua kusomea uanahabari ili niendelee kukuza kipaji changu na nikajiunga na chuo cha kiufundi cha NIBS.
Isitoshe, najihisi kuwa nilizaliwa ili niweze kuburudisha watu kupitia burudani yenyewe, nifunze, nionye, niwatie watu ambao wamekata tamaa tumaini. Safari haijawa rahisi lakini wasemavyo ni kuwa, hata dhahabu lazima ipitie kwenye moto ili ing’ae.
Sasa hivi niko karibu kutamatisha masomo yangu ya uanahabari na mimi bado niko kwenye kundi lile lile la kuigiza . Nimenoa makali ya kipaji changu na bado safari ni ndefu na niko tayari kusafiri. Ningetaka sana kupiga hatua na kuwa kama muigizaji Abel Mutua ama Njungush kwani hao ndio nawafuatilia sana. Sasa hivi mimi nafanya kipindi maarufu sana chuoni, ambacho ni NIBS Asubuhi kwenye Nibs Radio nikiamini kwamba bidii zangu hazitaenda kapa katu. Ipo siku hiyo nisiyoijua itakuja mazuri.
- Ni nini hasa kilikuchochea katika tasnia hii?
Kilichonivutia haswa ni ile hali ya kuwafanya watu watabasamu kila ninapoigiza . Hakuna jambo linalonitia moyo kama kumjengea mtu siku yake. Watu wengi hupitia magumu katika maisha ya kila siku kwa hivyo ni bora kuwapa sababu ya kutabasamu ili msongo wa mawazo usiwaandame.
- Siku yako huwa vipi kunapokucha?
Siku yangu huanza saa kumi na mbili asubuhi pale ambapo mimi hupanga ratiba ya siku hiyo, masomo yangu huanza saa nne ila mimi huingia shule saa moja unusu ili niweze kuingia studio kupiga makasia ya kwangu. Napeperusha kipindi cha asubuhi ndani ya Nibs radio kipindi chenyewe ni Nibs Asubuhi. Huwa tunakiendesha kipindi chenyewe na Alfred Lobawoi. Kisha, baadaye mmi huanza masomo yangu saa nne hadi saa kumi na moja unusu, kisha naungana na wenzangu kufanya mazoezi tofaouti kama vile mahojiano, kupeperusha vipindi hewani, kurekodi vipindi na uandishi wa vipindi na mambo mengineyo.
- Ni kitu kipi kinakupendeza katika kazi yako?
Kinachonipendeza zaidi ni kupewa nafasi ya kuzungumza na kutangamana na watu tofauti . Hii hunisaidia kujikuza na kujua mengi na hata kupata marafiki wapya kila siku.
- Ni kitu kipi kigumu kwa yale ambayo unafanya?
Hisia zako za kibinafsi na za kazini hazifai kuchangia jinsi unaifanya kazi yako. Wanaokusikiliza wanatarajia uwe bora hata kama unayapitia magumu gani.
- Umewahi kupata changamoto katika kazi yako? Tuambie kuihusu.
Kuna wakati nilikua naugua ila nilikua nalazimika kuigiza, ilikua vigumu ila mwisho wa siku lazima kazi ifanyike au sio?
- Ni kitu kipi kinakusaidia kupambana na changamoto hizo?
Sasa hivi sauti yangu ni dhahabu kwangu hivyo basi lazima niichunge kivyovyote vile. Wakati mwingine maji ya ndimu hunisaidia kuhakikisha sauti yangu iko sawa.
- Huwa unatangaza kazi zako? Tuambie hatua hiyo inavyokusaidia.
Kipindi cha Nibs asubuhi sasa hivi kimekua na mashabiki wengi sana sababu ya kazi nzuri tunayoifanya na pia kukitangaza kwenye mitambo yetu ya kijamii. Pia kuwapo mashabiki wetu nafasi ya kupiga simu ama kutuma ujumbe mfupi imetusaidia kupiga hatua mbele.
- Ni wosia upi utampa yule ambaye angetaka kuwa kama wewe.
Wasia siku zote ni ‘sio lazima utukane ili ujulikane’ pia ‘ ukiona umefanikiwa usione wenzako kama ghoighoi ni muda wao hujafika ila ipo siku na wao watafanikiwa.
- Ukipatiwa nafasi ya kubadilisha ulimwengu na kujibadilisha wewe mwenyewe utalete mabadiliko yapi?
Nikipata nafasi ya kubadilisha mambo hapatakua na makabila yoyote yaani sote tutakua sawa. Ukabila umeharibu mambo humu nchini na kukosanisha mandugu.
- Kwa yule ambaye angependa kuona kazi zako, atazipataje?
Kwenye mitandao yote ya kijamii ni Brian ibra , pia usikose kuskiza NIBS FM, Kipindi cha NIBS Asubuhi, upate burudani naye Alfred Lobawoi na mmi hapa Brian Ibra; Kijana vibes home and away shukran