Fatma Ali Mohamed
By Alfred Lobawoi
Worth Noting
“Msukumo wangu wa kutunga mashairi niliupata kwa kusikiliza taarabu. Hususan burudani la mwambao kipindi ambacho kilikuwa kinaendeshwa nchini Kenya. Niliwapenda sana waimbaji wa Kenya hususan Juma Balo. Kwa Zanzibar waimbaji walionivutia sana na kunifanya nipende mashairi na nitunge pia ni Fatma Issa.
Baadhi ya faida nilizopata katika utunzi wa mashairi ni kuwa jaji/mwamuzi wa sanaa katika mashindano ya Elimu Bila Malipo Zanzibar, kuanzia ngazi ya Kanda, wilaya mkoa hadi taifa. Hivyo kunakuwa na posho tunalipwa.
Watunzi wanaoibukia katika ulingo wa ushairi, kwanza nawashauri wasome sana kazi za magwiji wa ushairi watapata kujuwa mengi.”
- Tueleze kwa kifupi Fatma Ali Mohamed ni nani?
Fatma Ali Mohamed ni Mtanzania aliyezaliwa Pemba katika wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kwa sasa ni mwalimu wa skuli ya Sekondari Limbani
- Msukumo wako wa kutunga mashairi ulitoka wapi?
Msukumo wangu wa kutunga mashairi niliupata kwa kusikiliza taarabu. Hususan burudani la mwambao kipindi ambacho kilikuwa kinaendeshwa nchini Kenya. Niliwapenda sana waimbaji wa Kenya hususan Juma Balo. Kwa Zanzibar waimbaji walionivutia sana na kunifanya nipende mashairi na nitunge pia ni Fatma Issa. Bakari Abeid na Sabaha Salum. Kwa kweli waimbaji hawa wamechangia sana katika utunzi wangu wa mashairi.
- Je, mazingira uliyomo yalikuchochea vipi katika utunzi?
Katika mazingira ambayo naishi yalinichochea sana katika utunzi. Hii ni kwa sababu madras ambayo nilikuwa nasoma tulikuwa tunaadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) kwa kutunga kaswida na tenzi mbalimbali za kumsifu yeye hivyo yalinisaidia sana katika utunzi wangu. Vilevile tunatunga mashairi na tenzi za kuwafunza wari wanaotaka kuolewa ili wakaishi vyema na waume zao. Vilevile tunatunga mashairi, tenzi, nyimbo kwa ajili ya kushiriki Tamasha la Elimu Bila Malipo linaloadhimishwa mwezi wa tisa kila mwaka. Mazingira haya yamenisaidia kiasi.
- Ni matukio yapi ambayo unayakumbuka katika safari yako ya utunzi?
Kuna matukio mbalimbali ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo ambayo yalinifanya nitamauke kutunga ushairi. Unaweza kutunga shairi lako zuri, siku hiyo umejikaza katika utunzi. Ukatuma kwenye makundi ya ushairi, wakazuka baadhi ya watu wakakuponda hadharani, hii inavunja moyo kwa kweli.
Vilevile unatunga shairi lako zuri lenye kutumia jazanda kwa ajili ya mashindano ya Elimu Bila Malipo na mghani akalighani vizuri tu lakini kwa utashi wa majaji ukakoseshwa ushindi na kupewa mtu mwengine kisa kujuana. Hii inatamausha sana.
- Kando na utunzi, wajishughulisha na nini kingine?
Kando na utunzi mimi ni mwalimu ambae nimeajiriwa na Serikali Ya Mapinduzi Zanzibar. Nafundisha katika Skuli ya Limbani Sekondari. Vilevile tumeanzisha kikundi cha kutoa mafunzo na kuwaombea dua watoto wetu ambao wanataka kuolewa.
- Ushairi unakufaidi vipi wewe kama mtunzi?
Ama kwa upande wa faida kwenye utunzi wa ushairi si kubwa wala si nyingi. Ila kwa vile ushairi umo kwenye nafusi zetu tunatunga ili nyoyo ziburudike. Baadhi ya faida nilizopata katika utunzi wa mashairi ni kuwa jaji/mwamuzi wa sanaa katika mashindano ya Elimu Bila Malipo Zanzibar, kuanzia ngazi ya Kanda, wilaya mkoa hadi taifa. Hivyo kunakuwa na posho tunalipwa. Vilevile mimi ni Katibu wa michezo na sanaa katika Kanda ya mjini pia ni mjumbe wa baraza la michezo na sanaa la mkoa. Katika mkoa wetu wa Kaskazini Pemba. Hivyo tunakuwa tunapata posho tunapoendesha shughuli zetu. Pia huwa napata tenda za kutunga tenzi na mashairi katika shughuli mbalimbali kama vile za mapinduzi, shughuli za mwenge wa uhuru, kwa hio kupitia tenda hizo napata hela si haba. Pia katika diwani yangu niliyoitowa hivi karibuni nimeanza kuvuna kazi ya mikono yangu alhamdulillah.
- Ni changamoto zipi ambazo umekumbana nazo katika utunzi?
Changamoto nilizokumbana nazo katika utunzi wa mashairi ni kukatishwa tamaa na watu wanaojuwa ushairi. Baada ya kukuelekeza basi wao wanakubomoa.
- Unawashauri vipi watunzi wanaoibukia katika ulingo wa ushairi?
Watunzi wanaoibukia katika ulingo wa ushairi, kwanza nawashauri wasome sana kazi za magwiji wa ushairi watapata kujuwa mengi. Vilevile wanapokatishwa tamaa basi wasitamauke, waendelee kutunga na iko siku watatoboa tu, pia wasikasirike wakati wanaporekebishwa, kwani anayekufunza anakutaka na wewe ujuwe.
- Anayetaka kufaidi kazi zako atazipataje?
Anaetaka kufaidi kazi zangu basi anunuwe diwani yangu ya kwanza ya UHONDO WA NGOMA humo atapata faida nyingi. Vilevile atafaidi kupitia makundi mbali mbali ya ushairi.