Winjoy Gacheri

Leo ninasema wazi,yaliyo moyoni mwangu

Visanga vy siku hizi,vinatikisa rohongu

Vimekua kama jonzi,naapa mbele ya mungu

Vitoto hivi vya Leo ,vinayo maradhi Gani?

 

Zama zetu Nakumbuka,tulipokua sikuli

Tukionywa twaonyeka,ghulamu na wanawali

Adabu tulishika ,ikapenya Kwa miili

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Tuliheshimu wazazi,vile vile majirani

Kutii tulimaizi,ni dhahabu aushini

Tulikemea ajizi,kiamboni na darasani

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Mabinti wa siku zile,walijua kutulia

Wangenyoshewa kidole,machozi wangeyatoa

Waliustawi ukale,wachumba kujipatia

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Oneni hivi vya Leo,vyajiita vidijito

Vyaishia Kwa nyingi ndweo,duniani na kindoto

Havitunzi Mili Yao,ilozidiwa na joto

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Vyatembea vikiringa,ety wao mashangingi

Hata havifungi kanga,mapaja marangirangi

Ukifumbua maninga,taona vyavuta bangi

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Vyapenda kuhanja hanja,kujifanyia wasomaji

Midomo vyakunjakunja,magalacha usagaji

Usipokuwa mjanja,vitakutosa Kwa maji

Vitoto hivi vya Leo, vinayo maradhi Gani?

 

Vyachukia ushauri ,mashikio Yana pamba

Vimejaa ushauri,jinsi vinavyojigamba

Vyazurura kijasiri,usiku sawa na mamba

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Havijali maisha ,chochote vyaparamia

Visipojirekebisha,wallahi vitajutia

Malenga vimenichosha,moliwa naviachia

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Ukingoni nmefika,chini napiga magoti

Machozi yanitoka,nikipanga mikakati

Wapendwa twahitajika,tukiokoe kizati

Vitoto hivi vya Leo,vinayo maradhi Gani?

 

Malenga:Winjoy Gacheri

Lakabu: mtoto wa Meru

Chuo kikuu Cha MKU

By The Mount Kenya Times

We are The Mount Kenya Times. For customer care, 📨 info@mountkenyatimes.co.ke or 📞 +254700161866 For feedback to editorial, 📨 news@mountkenyatimes.co.ke or 📞 +254705215262 or WhatsApp +254714090155

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *