Wanjohi. P. Mugambi
Wako wapi wako wapi,watu walojaa utu
Nijuzeni wako wapi, ambao kweli ni watu
Kwa ukweli wako wapi, wenye nyoyo ziso kutu
Wako wapi?
Wako wapi wako wapi, waliyoyashinda haya
Ndooni mseme wapi, wako wasoona haya
Mimi niwapate wapi, waloiweza duniya
Wako wapi?
Wako wapi wako wapi, watetezi wa wanyonge
Niwapate hao wapi, wasodhulumu mnyonge
Nikawaambie wapi, leo mwanyonga wanyonge
Wako wapi?
Wako wapi wako wapi, wale kweli marafiki
Nitambue wako wapi, waloacha unafiki
Hao mashakiki wapi, nijuzeni niafiki
Wako wapi?
Wako wapi wako wapi, wale walezi azizi
Walolea wako wapi, wakijua pia kazi
Si wa leo wako wapi, kwao si bora malezi
Wako wapi?
Wako wapi wako wapi, sijui kwa kweli wapi
Nijuzeni wako wapi, niwapate huko wapi
Ili nikijua wapi, wapate haya mafupi
Wako wapi?
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni
Similar Posts by The Mt Kenya Times:
- KEMSA chief tells Ruto medicine order fill rate has more than doubled in four years
- IEBC commissioner urges shared responsibility for credible 2027 poll
- KENAPCO chair calls for skills revolution to drive Kenya’s economic growth
- Nairobi’s diplomatic circuit becomes Ole Sereni’s fastest growing business frontier
- Mt Kenya Times ePAPER August 18, 2026