A section of guests at the Kiswahili Day celebrations in London. Photo SHAMLAL PURI
By Alfred Lobawoi
@themtkenyatimes
Worth Noting
“Kiswahili ni kati ya lugha zinazozungumzwa na watu zaidi ya million 200 duniani, hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini zenye wazungumzaji wengi. Vilevile ni lugha ambayo inatumika mno katika mawasiliano ya Kimataifa na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa.
Ni dhahiri shairi kwamba kwa sasa lugha hii ashirafu ya Kiswahili imepiga hatua si haba kutokana na uzungumzwaji wake wa mara kwa mara. Shuleni wanafuzi hutumia lugha hii katika mawasiliano na pia hutumika kama lugha mojawapo ya kufunza somo la Kiswahili
Mashaka ya ukuaji wa Kiswahili ni kama vile ukosefu wa matumizi sahihi ya lugha sanifu. Ni wengi hawapendi kujikita katika uzungumzaji wa Kiswahili sanifu kwa kukwepa ngeli. Wengine hukiona kama lugha ya wasio kubwa na Elimu ya juu. Kiswahili si kigumu bali ni rahisi mno. Ajifunzaye huishi kujua na asiyeuliza hana ajifunzalo.”
Mnamo Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO ilibuni tarehe saba mwezi wa saba kuwa siku ya Kiswahili duniani kuanzia 2022. Tangu wakati huo, maadhimisho yamekuwa yakifanyika kila mwaka ikiwemo vikao vya kimataifa kama EAC, kwa lengo la kukuza matumizi ya Kiswahili katika Elimu, Utamaduni na Amani.
Kupitia UNESCO ndipo tunatambua ukweli kuwa Kiswahili ni kati ya lugha zinazozungumzwa na watu zaidi ya million 200 duniani, hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini zenye wazungumzaji wengi. Vilevile ni lugha ambayo inatumika mno katika mawasiliano ya Kimataifa na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa. Hii ni nafasi ya kutambua historia ya Kiswahili, kuenzi kazi za wanafasihi na walimu wa Kiswahili na pia kukuza matumizi aula ya Kiswahili katika sekta rasmi na zile ambazo si rasmi.
Aidha katika pumzi zizo hizo, siku hii mahususi ilitengwa na shirika hilo kwa madhumuni ya kulinda haki ya lugha ambapo watu hupata haki ya kujieleza katika lugha yao na kuhakikisha usikilizaji wa masuala yao. Jambo jingine ni kuimarisha Elimu na uwajibikaji; kwayo linasisitiza matumizi rasmi ya Kiswahili kwenye sekta mbalimbali kama vile za sheria, huduma za afya, mahakama na utumishi wa umma. Kukuza utangamano na Amani, kupitia lugha ya Kiswahili ndipo mazungumzo baina ya watu huimarika na kulete uwiano miongoni mwa watu ambao awali walikuwa na uhusiano mbaya.
Ni dhahiri shairi kwamba kwa sasa lugha hii ashirafu ya Kiswahili imepiga hatua si haba kutokana na uzungumzwaji wake wa mara kwa mara. Shuleni wanafuzi hutumia lugha hii katika mawasiliano na pia hutumika kama lugha mojawapo ya kufunza somo la Kiswahili. Sokoni pia hutumika katika matangazo ya kunadi bei ya bidhaa ambapo dalali hutangaza bidhaa yake akitumia Kiswahili. Hatua hii huwawezesha wanunuzi kuelewa moja kwa moja kinachozungumziwa na kupendezwa na bidhaa yenyewe. Kwenye ulingo wa kisiasa pia vilevile hakijaachwa nyuma kutokana na matumizi ya mara kwa mara ambapo wanasiasa hukitumia kueleza sera zao. Kauli mbiu na azimio ya vyama vingi vya kisiasa pia huandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Lililopo ndilo lisemwalo.
Pamoja na hayo wanalugha wengi wanaokitumia Kiswahili wamepata nafasi tolatola ya ufunzaji kwenye mataifa ya kigeni. Nafasi hizi zinaletwa na hiki Kiswahili ambapo walimu wengi hupata kazi ya kufunza, wengine wakapata nafasi ya kufanya tafsiri au ukalimani pamoja na kupata kazi ya utangazaji miongoni mwa mengine. Titi la mama li tamu, jingine halishi hamu.
Mitandao ya kijamii ni uwanja mwingine ambao umechangia pakubwa kwenye makuzi ya Kiswahili. Katika ulimwengu huu wa teknolojia ambapo vijana wengi wametumbukia kwenye teknolojia ya mitandao kama vile tiktok, Facebook na mtandao wa X; wao hutuma video ambazo wamerekodi kwa lugha ya Kiswahili. Mbali na hayo midahalo mbalimbali na matangazo mbalimbali ambayo wao hufanya ni kwa kutumia lugha hii ashirafu.
Vyombo vya Habari pia vipo mstari wa mbele katika mataifa mengi hasa kushadidia matumizi ya lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo huviendesha vipindi vya Kiswahili kupitia wanahabari wanaokichapukia na kuienzi lugha kwa ajili ya kuwashirikisha walimu, wanafunzi na hata wakereketwa wanaopenda Kiswahili. Magazeti pia ni njia nyingine ambayo imetumika mno katika makuzi ya Kiswahili. Mijadala, barua kwa mhariri, Makala na maswali ya somo la Kiswahili huchapishwa sana kwa ajili ya kukiendeleza Kiswahili. Pamoja na hayo pia wataalamu na walimu wanaofunza lugha hupewa nafasi ya kutoa mchango wao gazetini.
Yote hayo ni tisa, kumi ni kwamba kando na lugha hii adhimu kupiga hatua bado kuna mikingamo ambayo imetatiza ukuaji wake. Sheng si mojawapo. Mosi, narejelea lugha ya Sheng kwa kutambuliwa kuwa kero ya kutatiza Kiswahili ilhali ni lugha ya msimu. Ndiyo vijana wengi hutumia Sheng lakini wajua kwamba vijana hao hawawezi kuzungumza bila kuzungumza angalau neno moja la Kiswahili? Basi jua hivyo. Kupitia njia hiyo wao hukuza Kiswahili. Iwapo vijana wangegutuka gonezini na kuchapisha kamusi ya misamiati ya Sheng, basi hapo wangekuwa wamepiga hatua.
Mashaka ya ukuaji wa Kiswahili ni kama vile ukosefu wa matumizi sahihi ya lugha sanifu. Ni wengi hawapendi kujikita katika uzungumzaji wa Kiswahili sanifu kwa kukwepa ngeli. Wengine hukiona kama lugha ya wasio kubwa na Elimu ya juu. Kiswahili si kigumu bali ni rahisi mno. Ajifunzaye huishi kujua na asiyeuliza hana ajifunzalo. Mashaka mengine ni ukosefu wa misamiati faafu ambapo huwafanya watu kuzungumza na kubananga lugha pasipo kuelewa lipi ni lipi. Ili kuyashinda haya yote uhamasishaji wa lugha hii adhimu inastahili kujengewa msingi thabiti ili walimu, wanafunzi na hata wakereketwa waelewe zaidi matumizi ya Kiswahili fasaha si tu katika mazungumzo bali pia katika elimu na hata maisha ya kila siku. Safari ni hatua.
Ni wito kwa Wakereketwa wa Kiswahili na walimu kushinikiza serikali yetu ya Kenya kuasisi Baraza la Kiswahili. Ili kuweka mikakati kabambe ya kuieneza lugha hii, kuitukuza na kuishadidia; lazima pawe na baraza maalum ambalo litakuwa linatoa miongozo hiyo. Kiswahili ni lugha ya taifa na sisi sote tunafaa kuwa mstari wa mbele ja mfuko wa shati. Nadhani tukipiga hatua kama Tanzania (BAKITA) na Zanzibar (BAKIZA) kubuni baraza basi kazi itakuwa kwetu. Jipe leo changamoto ya kujifunza misamiati miwili ya Kiswahili kisha utumie katika sentensi. Ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo. Wasalaam!