Wanjohi. P. Mugambi
Siachi mimi kulia, Fabian nikumuwaza
Ameitoka dunia, bila sisi kutujuza
Heri angetupungia, mkono akitwongoza
Lala walalapo wema, Fabiani wa Usamba
Tangu tulipojuana, mwaka huu septemba
Naamba hili bayana, mengi sisi tuliamba
Tulipanga mengi sana, ayatimiza Muumba
Lala walalapo wema, Fabiani wa Usamba
Hili hatukuliwaza, ya kwamba ungetutoka
Miguu imelegeza, kwake wewe kuondoka
Machozi yanatuliza, kila tukiwaza fika
Lala walalapo wema, Fabiani wa Usamba
Kifo tunalia kifo, ni lini utatosheka
Nawe ulale fofofo, jinsi wengine hakika
Twauliza mbona kifo, Makau wetu kuteka
Lala walalapo wema, Fabian wa Usamba
Ndiyo maisha safari, nawe umetangulia
Uliyekuwa mahiri, na mwenye upendo sawia
Leo imegika shari, ameipenda Jalia
Lala walalapo wema, Fabiani wa Usamba
Hadi tukipatana, ma’na tunakuja pia
Akakufae Rabana, peponi ukatulia
Nasi tunaongozana, yetu ikajatimia
Lala walalapo wema, Fabian wa Usamba
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni